tangazo

tangazo

Tuesday, July 8, 2014


Historia ya Sheikh Ahmed Al Khalili

Sheikh: Ahmed bin Hamed bin Suleiman Al-Khalili. Mwanachuoni mkubwa (mtaalamu),na bahari ya wino uliojaa elimu yeye ni ulimwengu kwa elimu yake. ALLAH amuhifadhi.

Mwanachuoni mkubwa sheikh Ahmed bin Hamed bin Suleiman Al-khalili, ni mtu mwenye elimu anaejulikana ulimwenguni anatoka wilaya ya Bahla Oman katika mkoa wa Oman ndani.

 

Yeye anatokana na uko wenye wema na fadhila na uwarabu safi. Baba yake alikuwa maarufu kwa wema wake na kumuogopa ALLAH, babu yake alikuwa kadhi (hakimu) wa mji wa Bahla.

 

 Baba yake alisafiri na kwenda huko Zanzibar (Afrika ya Mashariki). Na huko Zanzibar baba huyo akapata mtoto ambaye ni Sheikh Ahmed siku ya Jumatatu tarehe 12 Rajab 1361H inawafikia tarehe 27 July 1942. Baba yake akamlea malezi mema yenye fadhila na kupenda elimu ambayo imefanya mabadiliko makubwa katika maisha ya Sheikh baadaye.

 

Alipokuwa mdodgo alijiunga katika vyuo vya kusomeshwa Qur'aan kwa muda wa miaka miwili akamaliza kusoma chuoni na umri wa miaka tisa hali ya kuwa amehifadhi kitabu chote cha Mwenyezi Mungu Qur'aan.

Kisha baada ya hapo akajiunga misikitini katika kusoma elimu mikononi mwa wanavyuoni (masheikh) maarufu huko Zanzibar. Miongoni mwa hao masheikh waliomsomesha elimu ya dini katika fiqh aqida (kuamini) na lugha ya kiarabu, nahu, sarf na hesabu ni: Sheikh Issa bin Said Al-Ismaily na Sheikh Humud ibn Said Al-Kharusy na Sheikh Ahmed bin Zahran bin Ahmed Al-Riyamy. Na Sheikh Ahmed Al-khalili aliwahi kujiunga katika vikao vya elimu alivyoukuwa Allama (mwanachuoni mkubwa) Abi Is'haaq Ibrahim Ettfaishy akisomesha alipoitembelea Zanzibar. Na Sheikh Ahmed hajawahi kujiunga na shule ili apate nafasi ya kuzama ndani zaidi katika nyanda za elimu ya dini.

 

Alitafuta elimu kwa kusoma kila wakati na kusaidiwa na bongo lake ambalo lilikuwa ni rahisi kufahamu na kuhifadhi vitu, michororo ya mito ya elimu na hekima ikachorozeka kutoka kifuani mwake.

 

Na kubainisha hoja kukamiminika kutoka kwenye ulimi wake na kwa kufahamu kifua chake elimu tafauti na maarifa akaruzikiwa pendo baina ya watu akawa kila anaemuona anampenda na hizi ni fadhila za Mola anampa ampendae na amtakae katika waja wake.


Sheikh Ahmed hata kama alikuwa akitafuta elimu lakini, alikuwa akifanya biashara bega kwa bega yeye na baba yake, na katika mwaka 1384H unaosadifia mwaka wa 1964 Mwenyezi Mungu akajaalia mapinduzi ya kuipindua serikali ya ki-Oman yakatokea huko Zanzibar.

 

Mapinduzi haya yakasababisha Sheikh Ahmed pamoja na baba yake na familia yake warejee katika nchi yao ya asili Oman.

Hapa Sheikh akafikia wilayani kwao huko Bahla hapo watu wa Oman wakafahamu unyenyekevu wake na elimu yake wakamuomba awasomeshe elimu mbali mbali alizokuwa amesoma huko Zanzibar.

 

Sheikh Ahmed akasomesha kwa muda wa miezi kumi katika msikiti mkubwa huko Bahla, kisha Masheikh wakubwa wanaoishi Muscat wakapata habari kutoka kwa Sheikh Ibrahim bin Said Al-Abry kuwa kuna kijana ana elimu na maarifa makubwa kuhusu dini, hapo ndio Masheikh wa Muscat wakamuomba aje mjini ili awasomeshe na wakamchagua awe imama wa msikiti wa Al-Khoor Muscat mpaka 1391H. Na kutokea mwaka huu akaombwa awe kadhi (hakimu)katika mahakama kuu ya Muscat, akawa Sheikh Ahmed anafanya kazi ya ukadhi (uhakimu) na huku anaendelea kujisomesha na kupanua maarifa yake kuhusu dini yeye mwenyewe bila ya kutegemea mtu.

 

Baada ya hapo akachaguliwa kuwa mkubwa wa mambo yanayowahusu waislamu katika wizara ya mambo ya uadilifu na waqfu na dini ya kiislamu. Na katika mwaka 1395H unaosadifia mwaka 1975 ikatolewa sheria kutoka kwa Mfalme wa Oman Sultan Qaboos bis Said kuwa Sheikh Ahmed awe ni Mufti Mkuu wa Oman baada ya kufariki Sheikh Ibrahim bin Said Al-Abry. Na katika mwaka 1987 akapewa jukumu la kuwa ni kiongozi wa vyuo vya kusomesha dini ya kiislamu katika Oman akawa na cheo cha daraja ya mawaziri wa serikali.

KUELEKEA KWAKE KIELIMU NA KUITANGAZA DINI:

Sheikh Ahmed alizundukana usingizini baada ya kujuwa kuwa ALLAH amempa elimu na amemuwafikisha toka alipokuwa mdogo mpaka akapata vyeo vikubwa dharuara ya kuitangaza dini ya ALLAH kwa watu na kuwaepusha watu (umma wa kisslamu) na ujahili waliokuwa nao. Sheikh Akawa ndiye mwenye kuupa upya sura nzuri uislamu katika jamii ya Oman.

 

 Shekh akatizama jamii ya watu wa Oman na ulimwengu wa kiislamu mtizamo wa kweli akaanza kuongoza watu kwa njia ya kutoa mihadhara na khutba za Ijumaa mbali mbali.

 

 Pia akashiriki katika mikutano mbali mbali ya dini ndani ya Oman na nje akawa mashuhuri katika ulimwengu wa kiislamu, watu wenye elimu mbali mbali wakanza kushuhudia elimu yake na kumsifu na kumpa cheo na heshima mbele za watu.

Na tukitaka kuchambua maisha yake katika kutangaza dini na elimu aliyokuwa nayo. Inatosha kusema kuwa maisha yake yote ameyapoteza katika kuitangaza dini na kutafuta na kutoa elimu ya ALLAH kwa watu. Lakini ni bora kueleza baadhi ya pirika zake katika kuitangaza dini ya ALLAH, nazo ni:

1) Waadhi (mawaidha) na kuelekeza watu mema: Sheikh alitowa mawaidha kwa njia ya kutoa mihadhara na khutuba za sala ya Ijumaa, na kutoa nasiha zilizowazi kwa watu wote.

 

Na kanda zake nyingi za mawaidha ziko masokoni na Baadhi ya watu wanachapisha mawaidha yake kuwa kama vile vitabu vidogo ili watu wapate kusoma.

2) Fatawi: Cheo chake cha kuwa Sheikh (Mufti) Mkuuu wa Oman kulimsaidia kupokea masuala na kuyajibu masuala mengi ambayo si rahisi kujuwa idadi yake kwa wingi wake. Masuala hayo yalikuwa yakigusa kila aina ya matatizo ya maisha ya waislamu katika wakati wetu huu.

 
 Mara nyingi watu huwa wanamuuliza masuali yao popote wanapomuona ikiwa ni njiani au misikitini au nyumbani kwake Sheikh. Fatawi nyingi za Sheikh zimehifadhiwa kwenye ofisi ya kutoa fatawi katika Wizara Ya Mambo Ya Dini-Oman.

3) Kushiriki katika mikutano mbali mbali ya dini ulimwenguni: Jambo la msingi alilozingatia Sheikh katika mikutano hii alipokuwa akikutana na wanavyuoni wakubwa wakubwa na maarufu ulimwenguni lilikuwa ni umoja wa waislamu. Akawa kila akipewa nafasi na akisimama katika jukwaa anawausia wanavyuoni na kuwasisitiza waislamu wawe kitu kimoja, jambo hili likamfanya awe ni bendera iliyo juu mbele ya wanavyuoni hawa na kujulikana kuwa ni kiingozi na mwanachuoni mkubwa wa madhehemu ya kiibadhi ulimwenguni.

4) Darasa za kutafsiri Qur'aan: Sheikh anatoa darsa za kutafsiri Qur'aan kwa wanafunzi wa chuo cha waadhi na kukataza mabaya katika Msikiti mkubwa wa Ruwi. Na darsa hizi anazitumia Sheikh katika kuandika kitabu chake maarufu cha tafsiri ya Qur'aan (JAWAHER AL-TAFSEER ANWAAR MIN BAYAN AL-TANZEEL) na mpaka hii leo juzuu tatu za kitabu hichi zimekwisha kamilika na ziko madukani zinauzwa.

5) Darsa katika ussul al-fiqh (asili katika fiqh): Sheikh aliwahi kuwasomesha na kuwafa fanulia wanafunzi wanaotafuta elimu ya dini baadhi ya mambo yaliyokuwemo kwenye kitabu cha (SHAMS AL-USSUL) cha Sheikh Nuur Deen Al-Salmi Mwenyezi Mungu amrehemu. Na hizi darsa ziko kwenye kanda za kaseti na zinauzwa madukani.

6) Kushiriki katika vikao vya kubadilishana mawazo ya elimu: Katika vikao hivi alitoa mihadhara ya uhakiaka kuhusu watu muhimu katika uislamu na mambo muhimu kuhusu historia ya kiislamu. Moja katika vikao hivyo ni kushiriki kwake katika kiako cha "ulimwengu wetu" na mihadhara mengi aliyoitoa katika mwaka 1994 "mwaka wa utamaduni wa watu wa Oman".

7) Darsa katika akida na fikra: Sheikh anatoa darsa hizi kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Oman (Qaboos University). Na darsa hizi zimerikodiwa na huenda zikachapishwa kuwa kama vile vitabu vidogo ili watu wapate kusoma. Na kila wakati Sheikh anakwenda chuo kikuu na kutoa mihadhara kwa wanafunzi wa kike wa chuo hicho.

8) Majibu ya elimu: Sheikh amesima kideti mbele ya wanao utukana uislam kwa kuwajibu na kuwapa hoja zilizo wazi kwa kurikodi kanda na kuzitambaza kwa hao watu ili wapate kujua lipi ni la haki. Pia Sheikh mara nyingi anawajibu kwa njia ya ukweli na upole wote wale ambao wanayatukana madhehebu ya Kiibadhi, na juu ya jamo hili ipo kanda aliyomjibu Sheikh Abdulaziz bin Baaz (Mufti wa Saudi Arabia) alipowakufurisha maibadhi na kuwahukumia kuuliwa. Na pia alimjibu Sheikh Abdulrahim Al-Tahhan alipojaribu kuivuruga Qur'aan karim kwa kuipa tafsiri isiyoambatana na maana ya baadhi za aya katika Qur'aan. Na Sheikh alimjibu mkiristo wa kiarabu alipojaribu kuutukana uislamu.

9) Kitabu cha "AL-HAQ AL-DAAMIGH": katika jambo hilo hilo la kujibu watu wanaoutukana uislam Sheik ameandika kitabu hichi kwa njia ya elimu iliyo juu kabisa kuhusu mambo matatu katika akida (kuamini) ya kiibadhi, hapa Sheikh anawajibu kuhusu kuto onekana kwa ALLAH Mola aliyetukuka siku ya qiyama, na kukaa motoni milele yule aliyefanya madhambi makubwa, na kuumbwa kwa Qu'aan Al-karim. Hichi kitabu kimejumuisha pia vipi madhehebu ya kiibadhi imeshikilia msimamo wa kusamehe ndugu zao waislamu ikiwa kuna kutofahamiana baina yao na madhehebu nyingine yeyote ile ya kiislamu. Na mwisho wa kitabu hichi Sheikh ameweka baadhi ya ushahidi wa kusifiwa madhehebu ya kiibadhi na viongozi wakubwa wakubwa wa dini ya kiislamu ulimwenguni.

10) Na sheikh ana maandishi na vitabu muhimu vingine kama vile: kitabu alichochambua tafsiri ya kitabu cha Sheikh Nuur Deen Al-Salmi, kitabu hicho kinaitwa "SHARH GHAAYAT AL-MURAAD" na maandishi aliyo andika kwa anuani ya "WAHYI AL-SUNNA FIY KHUTBATAY AL-JUMMA"

BAADHI YA MAJUKUMU (VYEO) ALIVYOKUWA NAVYO SHEIKH AHMED AL-KHALILI:

A) Vyeo vyake vya kazi zake za kawaida ndani ya Oman:

1) Mufti (Sheikh) mkuu wa Oman.

2) Mkubwa wa idara ya college za Sultan Qaboos katika kusomesha dini ya kiislamu.

3) Mkubwa wa college ya makadhi na na waadhi na kuamrisha mema.

4) Mwanachama katika bodi ya kukataza kudhulumiana (bodi kubwa ya mahakama Oman).

5) Raisi wa kuchunguza na kuhakikisha usahihi wa uchapishaji wa vitabu katika Wizara Ya Utamduni.

B) Vyeo vyake vya kazi zake za kawaida nje ya Oman:

1) Mwanachama wa jumuiya kuu ya fiqh ya kiislamu iliyoko chini ya Umoja wa nchi za kiislamu.

2) Mwanachama wa AAL-BAIT (Office kuu ya ufalme wa Jordan katika kufanya uchunguzi wa maendeleo ya kiislamu).

3) Mwanachama wa katiba ya chuo kikuu cha AAL-BAIT huko Jordan.

4) Mwanachama wa chuo kikuu cha uislam kinachoitwa (AL-Jamiat Al-islamia Al-Alamia) huko Pakistan.