tangazo

tangazo

Wednesday, February 3, 2016

TAARIFA  KWA VYOMBO VYA  HABARI  KATIKA

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
  
                                                                       
                               
TAARIFA  KWA VYOMBO VYA  HABARI  KATIKA SHAMRA SHAMRA ZA MAAZIMISHO YA MIAKA 39 YA KUZALIWA KWA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
Awali ya yote, kwa niaba ya Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya juu CCM – Zanzibar, naomba tuanze kwa kumshukuru Mweneyezi Mungu kwa kutujaalia sote uhai na afya njema na nchi yetu kuwa katika   hali ya amani na utulivu.
Pili, tunachukua fursa hii  kuwashukuru nyinyi  ndugu zetu wawakilishi wa vyombo vya  habari  kwa  kujumuika nasi ili kutusikiliza tuliyonayo leo hii kwa madhumuni ya kuufikishia taarifa hii umma  wa jamii yetu na wengine wanaofuatilia kwa makini masuala ya nchi yetu, Zanzibar.
Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya juu CCM –    Zanzibar ni moja kati ya Jumuiya nne (4) za Chama Cha Mapinduzi (CCM).  Kama mnavyofahamu, CCM, chama kikongwe kabisa cha siasa nchini, kilizaliwa tarehe 5/2/1977 hapa Zanzibar na sasa kinatimiza miaka 39. Hiki ni kipindi kirefu kwa Chama cha siasa na ni vyema kutafakari tulikotoka, tulipo na tuendako ili kuweza kuendelea kutumikia jamii yetu hasa kwa kuongoza Serikali. Nyakati zinabadilika, watu wanabadilika na mahitaji yao kijamii na hivyo kisiasa pia yanabadilika.
Sote tunaelewa kuwa CCM ni matokeo ya kuunganishwa kwa vyama vya Ukombozi nchini mwetu, Tanganyika African National Union (TANU) kwa Tanzania Bara na Afro Shirazi Party (ASP) kwa upande wa Zanzibar.
Baada ya kutimiza azma ya kuweka huru watu wa nchi hizi, kupitia kudai uhuru kwa Tanganyika na Mapinduzi kwa Zanzibar, lengo kuu la CCM kwa kipindi chote tokea kuundwa kwake ni kudumisha uhuru wetu. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania sote tubaki huru milele. Tusitawaliwe tena. Lengo la pili ni kuendeleza mapinduzi ya kiuchumi na kijamii ili Watanzania sote tuishi maisha yaliyo bora, na kwa kadiri inavyowezekana, maisha ya kisasa. 
Kwa upande wa Zanzibar, sisi  wanataluma tunaona fakhari kutokana na mafanikio  na  maendeleo yaliopatikana hadi sasa kwa usimamizi wa Serikali zinazoongozwa na ASP na baadae CCM, kuanzia awamu ya Jemedari  Hayati  Abeid Karume hadi awamu tulionayo sasa ya DK. Ali Mohamed Shein.
Leo hii, tunapenda kutambua mafanikio machache kama  ifuatavyo:
i.      Kudumishwa kwa uhuru wetu: Uhuru wa kweli wa Zanzibar ni ule uliotokana na Mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964. Tunasema kuwa ndio uhuru wa kweli kwani ndio uliokamlisha kuwaweka wananchi wote wa Zanzibar kuwa huru, ikiwemo Waafrika walio wengi.
ii.   Kudumisha Umoja wa Wananchi: Katika kipindi chote cha uongozi wa ASP, na kipindi cha miaka 39 ya uongozi wa CCM, Serikali zilizoundwa zimeendelea kusimamia na kuimarisha umoja wa Wananchi wake. Pamoja na tofauti zozote za kijamii na kisiasa zilizopo, kwa jitihada maalumu za Serikali za CCM bado Wazanzibari ni wamoja.
iii.Kupiga vita ubaguzi: Usawa wa binaadamu wote umeendelea kuwa msingi mkuu wa Mapinduzi ya Zanzibar kupitia itikadi ya ASP iliyoenziwa na CCM katika uhai wake wa miaka 39 tunayoiadhimisha. Nasaba, rangi ya ngozi na Imani ya dini ya mtu sio vigezo katika uanachama wala kushika uongozi katika CCM. Matokeo ya kuenziwa msingi huu wa usawa wa binaadamu wote ni kuwa leo hii sura ya mchanganyiko wa viongozi na wagombea wenye asili tofauti ni kubwa katika CCM kuliko ilivyo katika chama chengine chochote cha siasa hapa nchini. Sisi wanataaluma tunajivunia msingi huu wa usawa usio na ubaguzi.

Nje ya nchi, CCM kinatambulika kwa mwelekeo wake thabiti na usioyumba wa kuhimiza muungano wa Afrika kwa maslahi ya Waafrika wote. Afrika ina watu wenye asili tofauti, Waarabu upande wa Kaskazini, mchanganyiko wa weusi na weupe Kusini mwa Afrika na weusi na wenye asili ya Asia kwa maeneo yaliyobakia. CCM imeendelea kuhimiza umoja, mshikamano na muungano Waafrika wote bila ya kujali tofauti hizo.
iv.  Mfano wa Demokrasia: CCM katika uhai wake wote wa miaka 39 kimeendelea kuwa kioo cha misingi ya demokrasia, sio tu ndani ya chama bali hata nje. CCM ndio chama ambacho uongozi wake wa ngazi zote umebadilika sana kwa njia za kidemokrasia kuliko chama chochote nchini tokea kurejeshwa siasa za ushindani wa vyama vingi. Utaratibu wa kupata uongozi ndani ya Chama umeendelea kuwa wa wazi, wenye kutoa fursa sawa kwa kila mwanachama na pamoja na kuleta changamoto kwa uwazi wake, umeendelea kukipatia Chama, na Serikali kinazounda, viongozi imara.
v.    Huduma za Jamii: Pamoja na idadi ya wananchi wa Zanzibar kuongezeka kwa kasi kubwa sana katika uhai wan chi yetu na uongozi wa CCM, bado CCM imeunda na kusimamia Serikali zilizoweka mkazo katika kutoa huduma bora kwa wananchi wote. Kwa sisi wanashirikisho la elimu ya vyuo vikuu, tunashukuru kuwa chini ya Serikali za CCM, watoto wa wanyonge tumeendelea kupata elimu hadi ya chuo kikuu. Inajulikana kuwa kabla ya Mapinduzi fursa za Elimu hazikua sawa ambapo wananchi walio wengi walitengwa, kwa njia mbalimbali, na hivyo kutofaidika na huduma hii muhimu kwa kumkomboa mwanaadamu.
Sisi wanataaluma tunatambua kuwa chama cha mapinduzi kimeleta maendeleo kupia sekta mbali mbali ikiwemo makaazi bora, huduma za afya, kuimarika kwa miundombinu, upatikanaji wa habari, maji safi na salama, michezo, sanaa n.k
  Ndugu wanahabari,
Pamoja na mafanikio yote hayo ya kijamii na kisiasa, bado tunahitaji Amani, umoja na utulivu katika nchi yetu. Kwamba jana tumekuwa navyo sio uhakika kuwa na kesho vitakuwepo. Vinapaswa kulindwa na wananchi sote. Kwa mnasaba huu, naomba kugusia kidogo hali ya kisiasa na kijamii iliyojitokeza nchini kutokana na Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana, 2015 ambao kwa sababu zilizoelezwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Mhe. Jecha Salim Jecha, matokeo yake yalifutwa. Sote tumesikia taarifa ya Tume hiyo ya Uchaguzi kuwa sasa uchaguzi huo utafanyika tena tarehe 20 Machi mwaka huu. Kwa mtazamo wetu, uamuzi huu wa Tume ya Uchaguzi unatoa fursa ya kurekebisha kasoro zote zilizotajwa na Tume na kupelekea kufuta matokeo ya uchaguzi wa awali. Pia, unatoa fursa kwa nchi yetu kuendelea kupata uongozi wa miaka mitano ijayo kwa njia ya kidemokrasia.
Tumesikia baadhi ya vyama vya siasa vikisema kuwa havitashiriki uchaguzi huo. Kama sehemu muhimu ya jamii yetu, tunaomba vyama hivyo vitafakari tena kauli zake hizo na matokeo na athari yake kwa mustakabali wa Amani na utulivu wetu. Wananchi, na hasa sisi vijana, tusidanganywe tena na wanasiasa. Tunapaswa pia kujali maisha yetu na familia zetu na kutoshajiika na aina yoyote ya vitendo vya uvunjifu wa amani. Wanashirikisho tumefurahishwa na kauli ya CCM inayosema kuwa kitashiriki uchaguzi huo. Kwetu, kauli hii inathibitisha udhati wa CCM wa kupenda amani na utulivu wa nchi na wananchi wake.
Sisi wana shirikisho hatuoni njia nyengine mbadala, ya salama na ya mkato, ya kupata ufumbuzi wa hali iliyopo sasa. Hata vyama vikiongea kwa muda mrefu kiasi gani vitapaswa hatimae kurudi tena kwenye utaratibu wa Kikatiba, wa kuchagua viongozi kupitia sanduku la kura.
Tunaomba kuchukua fursa hii kutoa wito kwa vyama vyote, viongozi na wanachama wake, kuonesha ukomavu wa kisiasa, utayari wa kuongoza - dola na Wazanzibari sote - kwa kuacha jazba za kisiasa na malumbano yasio na tija na badala yake kushiriki tena uchaguzi wa marejeo kwa tarehe iliyopangwa na Tume. Wananchi, wanachama na wapenzi wa kila mgombea watawapigia kura na kumaliza sintofahamu iliyojitokeza na kupata washindi halali kwa majimbo yote.
Ni matumaini yetu Tume ya Uchaguzi na taasisi zote za Kidemokrasia zimesharekebisha kasoro zote zilizobainishwa katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 na kwamba maandalizi ya uchaguzi wa marejeo yatakamilishwa vyema.
Kwa jamii ya Kimataifa, tunaamini pia kuwa hali ya kisiasa ya Zanzibar na kwengineko barani Afrika inaendelea kutoa somo muhimu katika mashirikiano yetu. Somo hili ni kwamba haifai kwa jumuiya hiyo kushabikia na kuegemea upande wowote katika siasa za ndani za nchi, hata nchi ndogo kama Zanzibar. Tumesikia maazimio ya Chama kimoja cha Siasa likiwemo linalolitaka Jumuiya hiyo eti kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua watu wanaofanya uvunjifu wa Amani hapa Zanzibar. Kama jumuiya hiyo ipo makini kama inavyopaswa iwe, tunaamini ina matukio na ushaidi wote wa matukio ya uvunjifu huo wa amani, na inawajua wahusika wake wakuu. Sote tunajua kuwa matukio haya hayakutokea wakati wa uchaguzi huu tu, yapo muda mrefu na tunayo orodha yake. Tuko tayari kuisaidia Jumuiya makini ya Kimataifa ikihitaji kufanya uchunguzi uliyoombwa.
Kwa kumalizia, naomba nikumbushe tena kuwa sisi tumo katika maadhimisho miaka 39 ya uhai na uwepo wa Chama chetu, CCM. Naomba kutaarifu umma, hususan vijana, kuwa katika kuadhimisha kutimia miaka 39 ya CCM, Shirikisho la vyuo vya Elimu ya juu CCM – Zanzibar limeandaa kongamano la aina yake litakalofanyika katika ukumbi wa Salama wa hoteli ya Bwawani siku ya Alkhamis tarehe 4 Februari mwaka huu, 2015. Lengo la Kongamano hilo ni kutathmini hali ya kisiasa na Chama, tulikotoka, tulipo na tuendako. Ni vyema kufuatilia yatakayoendelea katika Kongamano hilo tunalotarajia kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari.
Nawatakia Wanachama na wapenzi wote wa CCM na wapenda Amani nchini maadhimisho mema ya miaka 39 ya CCM na uchaguzi wa Amani na salama tarehe 20 Machi mwaka huu.
Ahsanteni kwa kuniskiliza

Taarifa hii imetolewa na Shirikisho la Vyuo Vya Elimu ya Juu CCM- Zanzibar
3 Februari 2015.

“KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI”

Saturday, January 30, 2016

makabidhiano ya bajaji

 naibu katibu mkuu wizara ya ustawi wa jamii jinsia wanawake na watoto msham abdallah khamis akizungumza kabla ya makabidhiano ya bajaji kutoka save the chidren

 naibu katibu mkuu msham akitia saini pembeni yake bi mali
 bi mali kutoka save the children zanzibar akijaribu bajaji


 katibu msham akikabidhiwa funguo
katibu msham akijaribu kuendesha bajaji

jumla ya bajaji mbili zenye thamani ya milioni12 na laki 3 zimetolewa na save the children kwa ajili ya kusaidia kuongeza mapambano katika ufatiliaji wa kesi za udhalilishaji ambapo moja etapelekwa kaskazini na nyengine itatumika mjini katika kitengo cha hifadhi ya mtoto

Friday, January 15, 2016

KMKM WASAINI KINDA, BUSHIR ASEMA HUYU NI ZAIDI YA BAGAWAI WA YANGA




Na Abubakar Khatib (Kisandu)  , Zanzibar.

Timu ya mabaharia ya KMKM inayoshiriki ligi kuu soka visiwani zanzibar , leo hii imethibitisha rasmi kumsajili mlinzi wa kushoto kinda kutoka timu ya Muembe Beni United ambae anaitwa Adam Abdallah na watu wengi humwita BAGAWAI wakimfananisha na mlinzi wa kushoto wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na Yanga Mwinyi Haji Ngwali kwa alivofanana uchezaji wake na mlinzi huyo.

 Mtandao huu tumeongea na kocha Ali Bushir wa KMKM na akithibitisha kumsajili kinda huyo katika dirisha hili dogo la usajili la ligi kuu soka zanzibar huku kocha huyo akiamini mtoto huyo mwenye miaka 16 atamshinda MWINYI wa Yanga kwa mafanikio.

“ Ni kweli nimemsajili huyu kijana Adam na kwasasa ni rasmi ni mchezaji wa KMKM, huyu kijana ana kipaji sana na naamini atafika mbali mana yupo kama Mwinyi wa Yanga”. Alisema Bushir.

Hatukuishia hapo tukapiga hodi moja kwa moja mpaka kwenye klabu ya Muembe Beni United inayoshiriki ligi za madaraja ya vijana Wilaya ya Mjini na tukazungumza na kocha wa timu hiyo Suleiman Hamid (Mzee Ole) na kuthibitisha kuwa kweli leo wamemalizana na KMKM kuhusu mchezaji wao ambae ni BAGAWAI two.

“ Ni kweli leo tumemalizana na KMKM kuhusu Adam, naamini huko alipoenda atafanya vizuri mana kocha Bushir anajua kukuza vipaji”. Alisema Mzee Ole.

Tukamtafuta mchezaji mwenyewe huyo Adam Abdallah ambae leo rasmi KMKM wamemsajili huku akifurahi kucheza timu hiyo na amesema kuwa atapambana katika klabu ya KMKM kwenye ligi kuu soka ya zanzibar.

“ Nimefurahi kusajiliwa na KMKM na ntaweza kucheza nikipewa nafasi mana Muharami wa Black Sailors ameweza na mimi ntaweza , Kocha Bushir ameniona kwenye timu yang undo kanisajili, nimefurahi kusajiliwa KMKM pia nawashukuru makocha wangu akiwemo Vigema, Mzee Ole na Kocha THEO mana wote wamenisaidia”. Alisema BAGAWAI TWO.

shaka hamdu shaka kaimu katibu mkuu uvccm taifa akizungumzia juu ya bango liloleta sintofahamu zanzibar


CHIMBENI KHERI AWA MSHAURI WA RAIS MAMBO YA UTAMADUNI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amemwapisha Bwana Chimbeni Heri Chimbeni kuwa Mshauri wa Rais Masuala ya Utamaduni kufuatia uteuzi alioufanya hapo jana ambapo aliteua pia watendaji wengine wa serikali.

Watendaji wengine walioapishwa leo ni Bwana Juma Hassan Juma Reli kuwa Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango, Bwana Mdungi Makame Mdungi kuwa Katibu Kamisheni ya Utumishi wa Umma na Bwana Kai Bashir Mbarouk kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria.

Bwana Reli ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania anachukua nafasi ya Bi Amina Khamis Shaaban ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kabla ya uteuzi wa kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma bwana Mdungi alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba Sheria.

Kwa upande wa Bwana Kai Bashir kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Wizara hiyo.

Hafla hiyo fupi iliyofanyika Ikulu ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Said Hassan Said.


Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman, Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Maalim Abdulla Mwinyi na Makatibu na Manaibu Katibu wakuu wa wizara mbalimbali.

Wednesday, January 13, 2016

MKWASA AWAPA DOZI YA SIKU 1 MAKOCHA ZANZIBAR



Na: Abubakar Khatib (Kisandu), Zanzibar.

Kocha mkuu wa Timu ya soka Taifa ya Tanzania (Taifa Stars)  Charles Boniface Mkwasa Juzi alitembelea  kwenye darasa wanalokutana makocha mbali mbali wa Soka visiwani Zanzibar  katika skuli ya Sekondari ya Haile Selasies na kuwapiga msasa wa siku moja pamoja na kubadilishana mawazo na makocha hao.

Mkwasa alifurahishwa mno baada ya kupata mualiko kutoka kwa Chama cha Makocha Zanzibar (ZAFCA) kwa kuwatembelea makocha hao ambapo huwa na kawaida ya kukutana mara kwa mara.

“Nimefurahi kupata mualiko kama huu kukutana na makocha wenzangu wa hapa visiwani , na pia nimependa utaratibu wenu wa kukutana mara kwa mara makocha nyote wa hapa visiwani kwa kubadilishana mawazo na kupeyana elimu ya ukocha, na mimi ntawashauri wenzangu kule bara tufanye kama hivi. Alisema Mkwasa.

Mbali na kuwapiga msasa makocha hao mtandao huu ukataka kujua kwa mwalimu huyo kuhusu kombe la Mapinduzi lililohitimishwa leo hii kati ya Mtibwa Sugar na URA ya Uganda huku akikiri  kuwa kweli vipaji vipo visiwani kwenye michuano hiyo pia akiipa tano timu ya JKU.

“ Vipaji vipo vingi sana hapa Zanzibar, kuna vijana nimewaona na ntawaita muda utakapofika, nimewaona kwenye timu zote tatu zilizoshiriki Mapinduzi kutoka Zanzibar, Jamhuri wapo nimewaona, Mafunzo pia nimewaona, na hata JKU wapo wengi wana vipaji”.Alisema Mkwasa.

Thursday, January 7, 2016

TUHESHIMU NYAKATI LUQMAN MALOTO



TUHESHIMU NYAKATI
Mbwana Samatta ameitoa kimasomaso Tanzania. Watanzania waliomba na kutarajia na hakika imekuwa kweli. Hongera sana Mbwana kwa kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika kwa wachezaji wa ndani ya Bara la Afrika.
Tuzo ya Mbwana ina maana gani? Neno moja tu linatosha kujibu swali “Nyakati.”
Naam! Mbwana yupo kwenye wakati wake, ilikuwa lazima ashinde kwa sababu huu ni wakati wake, asingeshinda mwaka jana kwa sababu haukuwa wakati wake. Anaweza kushinda tuzo nyingine mwakani na kuendelea kama ni wakati wake.
Mwanamuziki Diamond Platnumz au Nasibu Abdul Juma, anatikisa Afrika kwa sasa akitokea Tanzania, ni kwa sababu huu ni wakati wake. Kila akigusa chupa, inakuwa almasi. Ni wakati wake.
Lazima kuheshimu nyakati. Na mafanikio ya Mbwana na Diamond, yawe fundisho kwa kila mmoja kutambua wakati wake na kuutumia vizuri kufika mbali na kupata mafanikio stahiki.
Wapo wengi hawakutumia vizuri nyakati zao. Alikuwepo fundi Haruna Moshi ‘Boban’, akasajiliwa Gefle IF ya Sweden mwaka 2010. Akatarajiwa kufika mbali. Haikuwa hivyo, alirejea nchini kwa kususa na alipofika Bongo, hakuwa Boban yule tena!
Ni nyakati za Floyd Mayweather! Anapigwaje sasa na wakati yupo kwenye wakati wake? Anatangaza kustaafu kisha anarejea ulingoni na hapigiki. Siku nyakati zake zikitoweka, atapigwa akiwa amelegea kama matembele.
Zilikuwepo zama za Mike Iron Tyson! Ilikuwa kabla hujaingia ulingoni, hakikisha umepima ubongo wako, maana ngumi yake ni kama bomu. Ikiwa ubongo wako haupo imara, akikupiga ngumi ya kichwa unakuwa mwendawazimu. Msome Frank Bruno yaliyomkuta.
Tyson alikuwa anamaliza pambano na kuingiza mpaka dola milioni 50 ndani ya sekunde 27. Aliyejifanya sugu na kusogea naye mpaka raundi 12, alikiona cha mtema kuni. Ila zilifika nyakati Tyson akawa akifika raundi ya sita anapigwa kirahisi kama mlenda. Yupo wapi Muhammad Ali? Zama zake zilishapita!
Unawakumbuka magolikipa tishio ulimwenguni kama Peter Schmeichel na Oliver Kahn? Walikuwa habari nyingine kila mtu katika wakati wake. Ni jambo zuri kuwa kila mmoja aliutendea haki wakati wake.
Ni kama Lionel Messi leo anavyoutendea haki wakati wake, kama ilivyo kwa Cristiano Ronaldo.
Zimepita zama za Ronaldinho Gaucho na Ricardo Kaka. Pamoja na kutikisa dunia lakini ukweli usiopingika ni kuwa hawakuzitendea haki nyakati zao, maana walidumu kwa kitambo kifupi mno kuliko viwango walivyokuwa navyo.
Wapi Zinedine Zidane ‘Zizzou’ na Ronaldo de Lima? Uliza kuhusu Luis Figo, Rivaldo, David Beckham na Thierry Henry? Je, maveterani Pele, Garrincha, Maradona, Romario, Lothar Matthäus, Marco Van Basten, Roberto Baggio na wengine?
Zilipowadia zama za George Weah, alichomoza kutoka Liberia, taifa lililokuwa na machafuko ya kivita, lisilo na rekodi ya soka, lakini alifika mpaka kileleni, akawa Mchezaji Bora wa Dunia, Mchezaji Bora wa Ulaya na Mchezaji Bora wa Afrika. Tuzo tatu kwa mkupuo mwaka 1995. Usichezee na nyakati!
Golini kabla ya Juma Kaseja, walimtangulia akina Mohamed Mwameja, Idd Pazi ‘Father’, Peter Manyika, Juma Pondamali, Athuman Mambosasa, Omar Mahadhi na wengineo. Ni nyakati!
Zama za Edibily Lunyamila, ungesema nini kwenye soka la Tanzania? Kama ilivyokuwa kwa Zamoyoni Mogella. Zilishakuwepo zama za mashuti ya Said Sued ‘Scud’ na Dua Said. Alitisha James Tungaraza mpaka akaitwa Boli Zozo.
Joseph Kaniki yupo jela Ethiopita, akitumia adhabu ya kunaswa na madawa ya kulevya. Ila nyakati zake alikuwa anafunga magoli popote kutokana na uwezo mkubwa wa kupiga mashuti. Watanzania walimwita Golota.
Na hii ndiyo sababu walishakuwepo akina Sunday Manara ‘Computer’, walipoondoka wakafuata akina Malota Soma, Edward Chumila, Hussein Marsha, na wengine, walipopisha walifuata akina Muso, Mgosi, Tegete, Ngassa na wengine! Ni kupishana kwa nyakati!
Walikuwepo Tupac Shakur na Notorious BIG, wakaimbwa ulimwengu mzima. Hip Hop iliwatazama wao tu! Walifuata akina Nas, Mase, DMX, Ja Rule, Eminem, 50 Cent na wengine! Jay Z anaendelea kucheza na nyakati, watu sasa hawaambiwi kitu kuhusu Kanye West, Lil Wayne, Wiz Khalifa, Kendrick Lamar, Drake na wengine!
Unawezaje kusahau zama za Bow Wow na Lil Romeo, walivyochuana kutengeneza fedha wakiwa watoto? Huwezi bila shaka kusahau vipindi vitamu vya wakubwa, Dre, Snoop Dog, hayati Big Punisher, Fat Joe, Coolio, LL Cool J, Ice Cube, Scarface na wengine.
Huu ni muda wa Justin Bieber, Chris Brown, The Weekend na wengine. Usher Raymond na Timbelake wanarudirudi. Hutasahau kuwa walikuwepo akina Baby Face, Joe Thomas, Lionel Richie na wengine! Yupo wapi Mfalme Michael Jackson?
Kipindi hiki Rihanna akionekana ndiye malkia, unadhani anafikia robo ya makeke ya Jennifer Lopez alipokuwa kwenye kiwango chake? Anafua dafu kwa Britney Spears na Christina Aguilera? Walikuwepo malkia wengine kama Janet Jackson, Whitney Houston, Mariah Carey na wengineo.
Wakati zikijadiliwa stori za nani anaweza sana ‘kuchana’ kati ya Nick Minaj na Iggy Azalea, kabla yao walikuwepo wakali kama Left Eye, Missy Eliot, Da Brat, Lil Kim na wengine.
Adolph Hitler kwa wakati wake alitawala dunia. Saddam Hussein alipokuwa kwenye wakati wake, alishambuliwa na mataifa zaidi ya 10, yakiongozwa na Marekani mwaka 1991 katika Vita ya Ghuba ya Uajemi, lakini hawakumuweza. Mwaka 2003, Marekani na Uingereza peke yake walimng’oa na ikawa sababu ya kukamatwa kisha kunyongwa. Ni kwamba mwaka 2003 hazikuwa zama za Saddam ndiyo maana alipigwa kirahisi.
Zilikuwepo zama za Michael Jordan na Magic Johnson kwenye kikapu, kabla yao walikuwepo akina Larry Bird, Moses Malone na wengine. Baadaye walifuata akina Shaquille O'Neal, Allen Iverson, Tim Duncan, Steve Nash, Kobe Bryant, LeBron James na sasa Stephen Curry ameshavuta kiti na ameketi.
Siasa za nchi kwa sasa zinamtazama Rais John Magufuli lakini kabla yake alikuwepo Jakaya Kikwete, kama alivyotanguliwa na Benjamin Mkapa, Ali Hassan Mwinyi na Baba wa Taifa, Julius Nyerere.
Upinzani leo wanatazamwa Edward Lowassa, Zitto Kabwe, Freeman Mbowe, Tundu Lissu na wengine, kabla yao walitikisa akina Augustino Mrema, Willibroad Slaa, marehemu Christopher Mtikila, Ibrahim Lipumba na wengineo. Ni nyakati!
CHUKUA SOMO
Juhudi huvuta bahati na bahati ndiyo itakufanya ufike kwenye kipindi chako cha mafanikio.
Muongozo ni wewe kujituma na utakapofika kwenye wakati wako, hakikisha unautumia vizuri ili utakapopita, watu waseme “alikuwepo fulani bwana!”
Pambana kwenye eneo lako ili utengeneze wakati wako mzuri. Utakuwa mwenye kupendwa na kuheshimika sana kama utafikia wakati wako na kufanya kile kinachohitajika.
Huu ni wakati wa Mbwana Samatta, kama ilivyo Diamond Platnumz na Ali Kiba. Hongera nyingi kwao.
Ijumaa Kareem.
Ndimi Luqman Maloto