tangazo

tangazo

Friday, May 30, 2014

VIJANA WAWILI WAPELEKWA RUMANDE KWA WIZI WA MAZAO


Wilaya ya Micheweni .

 

Mahakama ya Wilaya Konde imewapeleka rumande kwa muda wa wiki mbili vijana wawili wakaazi wa Wilaya ya Wete kwa tuhuma za wizi wa mazao .

 

Vijana hao ni Shaban Rajab Hamad  mkaazi wa Bopwe  na Khalfan Shaban Ali Mkaazi wa Mtambwe ambao wanadaiwa kuiba nazi saba zenye thamani ya shilingi 3,500 mali ya Faki Ali Faki Mkaazi wa Taifu wilaya ya Micheweni.

 

Mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo Abdalla Yahya Shamuhuna , mwendesha mashtaka wa serikali Ali Amour ameiambia mahakama kuwa watuhumiwa hao wametenda kosa hilo mei 26 mwaka huu majira ya saa saba za mchana .

 

Baada ya kusomewa shitaka lao , Mtuhumiwa Shaban Rajab Hamad amekubali kutenda kosa hilo wakati Khalfan Shaban Ali amekana kutenda kosa hilo .

 

Hata hiyo watuhumiwa wote wako rumande hadi tarehe 09 mwezi ujao kesi yao itakapokuja kutajwa tena .

 

Wakati huo huo mahakama hiyo pia imempeleka rumande hadi tarehe 03 mwezi ujao kijana Ali Gharib Hamad mkaazi wa Tumbe akituhumiwa kupatikana na majani makavu yanayosadikiwa kuwa ni bangi .

 

Kijana huyo alikamatwa akiwa na majani hayo tarehe 25 mwezi huu majira ya saa kumi na moja na nusu za jioni katika eneo la Saninga .

UWEKEZAJI KATIKA MAHOTELI YA KITALII KUTASAIDIA KUITANGAZA ZANZIBAR


ZANZIBAR.

 

Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar  Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa uwekezaji wa hoteli za kisasa zenye hadhi ya Kimataifa, utaisaidia Zanzibar kujitangaza kiutalii, na kuwafanya watalii wa hadhi ya juu na viongozi wa kimataifa kushawishika kuitembelea Zanzibar.

 

Maalim Seif ametoa kauli hiyo wakati akitembelea mradi wa ujenzi wa hoteli ya kisasa ya Grand Hyatt unaosimamiwa na Kampuni ya Dubai katika eneo la Shangani, mkabala na jengo la Mambo msige mjini Zanzibar.

 

Amesema kuwa kwa kipindi kirefu Zanzibar imekua na upungufu wa Hoteli zenye hadhi ya kimataifa, na kwamba kukamilika kwa ujenzi huo itakuwa faraja kwa Zanzibar, nakuhamasisha wawekezaji wengine katika sekta mbali mbali za kiuchumi.

 

Katika ziara hiyo Maalim Seif alifuatana na viongozi mbali mbali wakiwemo Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ramadhan Abdallah Shaaban pamoja na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Mazrui.

 

Akitoa ufafanuzi kuhusiana na ujenzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mkongwe  Issa Sarboko Makarani amesema kuwa ujenzi huo umezingatia viwango vya Kimataifa na umeridhiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

 

Amesema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya mazungumzo ya muda mrefu na shirika hilo linalojishughulisha na urithi wa Kimataifa, ambapo Mji Mkongwe za Zanzibar ni sehemu ya urithi huo.

 

Amesema kuwa hoteli hiyo itakapokamilika mwishoni mwa mwaka huu, itakuwa na uwezo wa kuwahudumia watalii wa hadhi ya juu pamoja na viongozi mashuhuri wa kimataifa wakiwemo Marais.

 

Bw. Makarani amefahamisha kuwa hoteli hiyo ya kisasa ambayo itakuwa na maegesho yaliyo chini ya jengo hilo itakuwa hoteli ya kwanza ya aina yake kuwahi kujengwa Zanzibar.

 

Ujenzi wa hoteli hiyo unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, utagharimu dola milioni 35 za kimarekani, ambapo ujenzi wake tayari umefikia zaidi ya asilimia 90.