ZANZIBAR.
Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa uwekezaji
wa hoteli za kisasa zenye hadhi ya Kimataifa, utaisaidia Zanzibar kujitangaza
kiutalii, na kuwafanya watalii wa hadhi ya juu na viongozi wa kimataifa
kushawishika kuitembelea Zanzibar.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo wakati
akitembelea mradi wa ujenzi wa hoteli ya kisasa ya Grand Hyatt unaosimamiwa na
Kampuni ya Dubai katika eneo la Shangani, mkabala na jengo la Mambo msige mjini
Zanzibar.
Amesema kuwa kwa kipindi kirefu Zanzibar imekua
na upungufu wa Hoteli zenye hadhi ya kimataifa, na kwamba kukamilika kwa ujenzi
huo itakuwa faraja kwa Zanzibar, nakuhamasisha wawekezaji wengine katika sekta
mbali mbali za kiuchumi.
Katika ziara hiyo Maalim Seif alifuatana na
viongozi mbali mbali wakiwemo Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati,
Ramadhan Abdallah Shaaban pamoja na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko
Nassor Ahmed Mazrui.
Akitoa ufafanuzi kuhusiana na ujenzi huo,
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mkongwe Issa Sarboko Makarani amesema kuwa ujenzi huo
umezingatia viwango vya Kimataifa na umeridhiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa
la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Amesema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya
mazungumzo ya muda mrefu na shirika hilo linalojishughulisha na urithi wa
Kimataifa, ambapo Mji Mkongwe za Zanzibar ni sehemu ya urithi huo.
Amesema kuwa hoteli hiyo itakapokamilika
mwishoni mwa mwaka huu, itakuwa na uwezo wa kuwahudumia watalii wa hadhi ya juu
pamoja na viongozi mashuhuri wa kimataifa wakiwemo Marais.
Bw. Makarani amefahamisha kuwa hoteli hiyo ya
kisasa ambayo itakuwa na maegesho yaliyo chini ya jengo hilo itakuwa hoteli ya
kwanza ya aina yake kuwahi kujengwa Zanzibar.
Ujenzi wa hoteli hiyo unaotarajiwa kukamilika
mwishoni mwa mwaka huu, utagharimu dola milioni 35 za kimarekani, ambapo ujenzi
wake tayari umefikia zaidi ya asilimia 90.
No comments:
Post a Comment