tangazo

tangazo

Wednesday, February 3, 2016

TAARIFA  KWA VYOMBO VYA  HABARI  KATIKA

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
  
                                                                       
                               
TAARIFA  KWA VYOMBO VYA  HABARI  KATIKA SHAMRA SHAMRA ZA MAAZIMISHO YA MIAKA 39 YA KUZALIWA KWA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
Awali ya yote, kwa niaba ya Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya juu CCM – Zanzibar, naomba tuanze kwa kumshukuru Mweneyezi Mungu kwa kutujaalia sote uhai na afya njema na nchi yetu kuwa katika   hali ya amani na utulivu.
Pili, tunachukua fursa hii  kuwashukuru nyinyi  ndugu zetu wawakilishi wa vyombo vya  habari  kwa  kujumuika nasi ili kutusikiliza tuliyonayo leo hii kwa madhumuni ya kuufikishia taarifa hii umma  wa jamii yetu na wengine wanaofuatilia kwa makini masuala ya nchi yetu, Zanzibar.
Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya juu CCM –    Zanzibar ni moja kati ya Jumuiya nne (4) za Chama Cha Mapinduzi (CCM).  Kama mnavyofahamu, CCM, chama kikongwe kabisa cha siasa nchini, kilizaliwa tarehe 5/2/1977 hapa Zanzibar na sasa kinatimiza miaka 39. Hiki ni kipindi kirefu kwa Chama cha siasa na ni vyema kutafakari tulikotoka, tulipo na tuendako ili kuweza kuendelea kutumikia jamii yetu hasa kwa kuongoza Serikali. Nyakati zinabadilika, watu wanabadilika na mahitaji yao kijamii na hivyo kisiasa pia yanabadilika.
Sote tunaelewa kuwa CCM ni matokeo ya kuunganishwa kwa vyama vya Ukombozi nchini mwetu, Tanganyika African National Union (TANU) kwa Tanzania Bara na Afro Shirazi Party (ASP) kwa upande wa Zanzibar.
Baada ya kutimiza azma ya kuweka huru watu wa nchi hizi, kupitia kudai uhuru kwa Tanganyika na Mapinduzi kwa Zanzibar, lengo kuu la CCM kwa kipindi chote tokea kuundwa kwake ni kudumisha uhuru wetu. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania sote tubaki huru milele. Tusitawaliwe tena. Lengo la pili ni kuendeleza mapinduzi ya kiuchumi na kijamii ili Watanzania sote tuishi maisha yaliyo bora, na kwa kadiri inavyowezekana, maisha ya kisasa. 
Kwa upande wa Zanzibar, sisi  wanataluma tunaona fakhari kutokana na mafanikio  na  maendeleo yaliopatikana hadi sasa kwa usimamizi wa Serikali zinazoongozwa na ASP na baadae CCM, kuanzia awamu ya Jemedari  Hayati  Abeid Karume hadi awamu tulionayo sasa ya DK. Ali Mohamed Shein.
Leo hii, tunapenda kutambua mafanikio machache kama  ifuatavyo:
i.      Kudumishwa kwa uhuru wetu: Uhuru wa kweli wa Zanzibar ni ule uliotokana na Mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964. Tunasema kuwa ndio uhuru wa kweli kwani ndio uliokamlisha kuwaweka wananchi wote wa Zanzibar kuwa huru, ikiwemo Waafrika walio wengi.
ii.   Kudumisha Umoja wa Wananchi: Katika kipindi chote cha uongozi wa ASP, na kipindi cha miaka 39 ya uongozi wa CCM, Serikali zilizoundwa zimeendelea kusimamia na kuimarisha umoja wa Wananchi wake. Pamoja na tofauti zozote za kijamii na kisiasa zilizopo, kwa jitihada maalumu za Serikali za CCM bado Wazanzibari ni wamoja.
iii.Kupiga vita ubaguzi: Usawa wa binaadamu wote umeendelea kuwa msingi mkuu wa Mapinduzi ya Zanzibar kupitia itikadi ya ASP iliyoenziwa na CCM katika uhai wake wa miaka 39 tunayoiadhimisha. Nasaba, rangi ya ngozi na Imani ya dini ya mtu sio vigezo katika uanachama wala kushika uongozi katika CCM. Matokeo ya kuenziwa msingi huu wa usawa wa binaadamu wote ni kuwa leo hii sura ya mchanganyiko wa viongozi na wagombea wenye asili tofauti ni kubwa katika CCM kuliko ilivyo katika chama chengine chochote cha siasa hapa nchini. Sisi wanataaluma tunajivunia msingi huu wa usawa usio na ubaguzi.

Nje ya nchi, CCM kinatambulika kwa mwelekeo wake thabiti na usioyumba wa kuhimiza muungano wa Afrika kwa maslahi ya Waafrika wote. Afrika ina watu wenye asili tofauti, Waarabu upande wa Kaskazini, mchanganyiko wa weusi na weupe Kusini mwa Afrika na weusi na wenye asili ya Asia kwa maeneo yaliyobakia. CCM imeendelea kuhimiza umoja, mshikamano na muungano Waafrika wote bila ya kujali tofauti hizo.
iv.  Mfano wa Demokrasia: CCM katika uhai wake wote wa miaka 39 kimeendelea kuwa kioo cha misingi ya demokrasia, sio tu ndani ya chama bali hata nje. CCM ndio chama ambacho uongozi wake wa ngazi zote umebadilika sana kwa njia za kidemokrasia kuliko chama chochote nchini tokea kurejeshwa siasa za ushindani wa vyama vingi. Utaratibu wa kupata uongozi ndani ya Chama umeendelea kuwa wa wazi, wenye kutoa fursa sawa kwa kila mwanachama na pamoja na kuleta changamoto kwa uwazi wake, umeendelea kukipatia Chama, na Serikali kinazounda, viongozi imara.
v.    Huduma za Jamii: Pamoja na idadi ya wananchi wa Zanzibar kuongezeka kwa kasi kubwa sana katika uhai wan chi yetu na uongozi wa CCM, bado CCM imeunda na kusimamia Serikali zilizoweka mkazo katika kutoa huduma bora kwa wananchi wote. Kwa sisi wanashirikisho la elimu ya vyuo vikuu, tunashukuru kuwa chini ya Serikali za CCM, watoto wa wanyonge tumeendelea kupata elimu hadi ya chuo kikuu. Inajulikana kuwa kabla ya Mapinduzi fursa za Elimu hazikua sawa ambapo wananchi walio wengi walitengwa, kwa njia mbalimbali, na hivyo kutofaidika na huduma hii muhimu kwa kumkomboa mwanaadamu.
Sisi wanataaluma tunatambua kuwa chama cha mapinduzi kimeleta maendeleo kupia sekta mbali mbali ikiwemo makaazi bora, huduma za afya, kuimarika kwa miundombinu, upatikanaji wa habari, maji safi na salama, michezo, sanaa n.k
  Ndugu wanahabari,
Pamoja na mafanikio yote hayo ya kijamii na kisiasa, bado tunahitaji Amani, umoja na utulivu katika nchi yetu. Kwamba jana tumekuwa navyo sio uhakika kuwa na kesho vitakuwepo. Vinapaswa kulindwa na wananchi sote. Kwa mnasaba huu, naomba kugusia kidogo hali ya kisiasa na kijamii iliyojitokeza nchini kutokana na Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana, 2015 ambao kwa sababu zilizoelezwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Mhe. Jecha Salim Jecha, matokeo yake yalifutwa. Sote tumesikia taarifa ya Tume hiyo ya Uchaguzi kuwa sasa uchaguzi huo utafanyika tena tarehe 20 Machi mwaka huu. Kwa mtazamo wetu, uamuzi huu wa Tume ya Uchaguzi unatoa fursa ya kurekebisha kasoro zote zilizotajwa na Tume na kupelekea kufuta matokeo ya uchaguzi wa awali. Pia, unatoa fursa kwa nchi yetu kuendelea kupata uongozi wa miaka mitano ijayo kwa njia ya kidemokrasia.
Tumesikia baadhi ya vyama vya siasa vikisema kuwa havitashiriki uchaguzi huo. Kama sehemu muhimu ya jamii yetu, tunaomba vyama hivyo vitafakari tena kauli zake hizo na matokeo na athari yake kwa mustakabali wa Amani na utulivu wetu. Wananchi, na hasa sisi vijana, tusidanganywe tena na wanasiasa. Tunapaswa pia kujali maisha yetu na familia zetu na kutoshajiika na aina yoyote ya vitendo vya uvunjifu wa amani. Wanashirikisho tumefurahishwa na kauli ya CCM inayosema kuwa kitashiriki uchaguzi huo. Kwetu, kauli hii inathibitisha udhati wa CCM wa kupenda amani na utulivu wa nchi na wananchi wake.
Sisi wana shirikisho hatuoni njia nyengine mbadala, ya salama na ya mkato, ya kupata ufumbuzi wa hali iliyopo sasa. Hata vyama vikiongea kwa muda mrefu kiasi gani vitapaswa hatimae kurudi tena kwenye utaratibu wa Kikatiba, wa kuchagua viongozi kupitia sanduku la kura.
Tunaomba kuchukua fursa hii kutoa wito kwa vyama vyote, viongozi na wanachama wake, kuonesha ukomavu wa kisiasa, utayari wa kuongoza - dola na Wazanzibari sote - kwa kuacha jazba za kisiasa na malumbano yasio na tija na badala yake kushiriki tena uchaguzi wa marejeo kwa tarehe iliyopangwa na Tume. Wananchi, wanachama na wapenzi wa kila mgombea watawapigia kura na kumaliza sintofahamu iliyojitokeza na kupata washindi halali kwa majimbo yote.
Ni matumaini yetu Tume ya Uchaguzi na taasisi zote za Kidemokrasia zimesharekebisha kasoro zote zilizobainishwa katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 na kwamba maandalizi ya uchaguzi wa marejeo yatakamilishwa vyema.
Kwa jamii ya Kimataifa, tunaamini pia kuwa hali ya kisiasa ya Zanzibar na kwengineko barani Afrika inaendelea kutoa somo muhimu katika mashirikiano yetu. Somo hili ni kwamba haifai kwa jumuiya hiyo kushabikia na kuegemea upande wowote katika siasa za ndani za nchi, hata nchi ndogo kama Zanzibar. Tumesikia maazimio ya Chama kimoja cha Siasa likiwemo linalolitaka Jumuiya hiyo eti kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua watu wanaofanya uvunjifu wa Amani hapa Zanzibar. Kama jumuiya hiyo ipo makini kama inavyopaswa iwe, tunaamini ina matukio na ushaidi wote wa matukio ya uvunjifu huo wa amani, na inawajua wahusika wake wakuu. Sote tunajua kuwa matukio haya hayakutokea wakati wa uchaguzi huu tu, yapo muda mrefu na tunayo orodha yake. Tuko tayari kuisaidia Jumuiya makini ya Kimataifa ikihitaji kufanya uchunguzi uliyoombwa.
Kwa kumalizia, naomba nikumbushe tena kuwa sisi tumo katika maadhimisho miaka 39 ya uhai na uwepo wa Chama chetu, CCM. Naomba kutaarifu umma, hususan vijana, kuwa katika kuadhimisha kutimia miaka 39 ya CCM, Shirikisho la vyuo vya Elimu ya juu CCM – Zanzibar limeandaa kongamano la aina yake litakalofanyika katika ukumbi wa Salama wa hoteli ya Bwawani siku ya Alkhamis tarehe 4 Februari mwaka huu, 2015. Lengo la Kongamano hilo ni kutathmini hali ya kisiasa na Chama, tulikotoka, tulipo na tuendako. Ni vyema kufuatilia yatakayoendelea katika Kongamano hilo tunalotarajia kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari.
Nawatakia Wanachama na wapenzi wote wa CCM na wapenda Amani nchini maadhimisho mema ya miaka 39 ya CCM na uchaguzi wa Amani na salama tarehe 20 Machi mwaka huu.
Ahsanteni kwa kuniskiliza

Taarifa hii imetolewa na Shirikisho la Vyuo Vya Elimu ya Juu CCM- Zanzibar
3 Februari 2015.

“KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI”