KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KATIKA SHAMRA SHAMRA ZA MAAZIMISHO YA MIAKA 39 YA KUZALIWA KWA CHAMA CHA
MAPINDUZI (CCM)
Awali ya yote, kwa niaba
ya Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya juu CCM – Zanzibar, naomba tuanze kwa kumshukuru
Mweneyezi Mungu kwa kutujaalia sote uhai na afya njema na nchi yetu kuwa
katika hali ya amani na utulivu.
Pili, tunachukua fursa
hii kuwashukuru nyinyi ndugu zetu wawakilishi wa vyombo vya habari
kwa kujumuika nasi ili
kutusikiliza tuliyonayo leo hii kwa madhumuni ya kuufikishia taarifa hii
umma wa jamii yetu na wengine
wanaofuatilia kwa makini masuala ya nchi yetu, Zanzibar.
Shirikisho la Vyuo vya Elimu
ya juu CCM – Zanzibar ni moja kati ya
Jumuiya nne (4) za Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kama mnavyofahamu, CCM, chama kikongwe kabisa
cha siasa nchini, kilizaliwa tarehe 5/2/1977 hapa Zanzibar na sasa kinatimiza
miaka 39. Hiki ni kipindi kirefu kwa Chama cha siasa na ni vyema kutafakari
tulikotoka, tulipo na tuendako ili kuweza kuendelea kutumikia jamii yetu hasa
kwa kuongoza Serikali. Nyakati zinabadilika, watu wanabadilika na mahitaji yao
kijamii na hivyo kisiasa pia yanabadilika.
Sote tunaelewa kuwa CCM
ni matokeo ya kuunganishwa kwa vyama vya Ukombozi nchini mwetu, Tanganyika
African National Union (TANU) kwa Tanzania Bara na Afro Shirazi Party (ASP) kwa
upande wa Zanzibar.
Baada ya kutimiza azma ya
kuweka huru watu wa nchi hizi, kupitia kudai uhuru kwa Tanganyika na Mapinduzi
kwa Zanzibar, lengo kuu la CCM kwa kipindi chote tokea kuundwa kwake ni
kudumisha uhuru wetu. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania sote tubaki
huru milele. Tusitawaliwe tena. Lengo la pili ni kuendeleza mapinduzi ya
kiuchumi na kijamii ili Watanzania sote tuishi maisha yaliyo bora, na kwa
kadiri inavyowezekana, maisha ya kisasa.
Kwa upande wa Zanzibar,
sisi wanataluma tunaona fakhari kutokana
na mafanikio na maendeleo yaliopatikana hadi sasa kwa
usimamizi wa Serikali zinazoongozwa na ASP na baadae CCM, kuanzia awamu ya
Jemedari Hayati Abeid Karume hadi awamu tulionayo sasa ya DK.
Ali Mohamed Shein.
Leo hii, tunapenda
kutambua mafanikio machache kama ifuatavyo:
i. Kudumishwa kwa uhuru wetu: Uhuru wa kweli wa Zanzibar ni ule uliotokana na Mapinduzi ya
tarehe 12 Januari 1964. Tunasema kuwa ndio uhuru wa kweli kwani ndio
uliokamlisha kuwaweka wananchi wote wa Zanzibar kuwa huru, ikiwemo Waafrika
walio wengi.
ii. Kudumisha Umoja wa Wananchi: Katika kipindi chote cha uongozi wa ASP, na kipindi cha
miaka 39 ya uongozi wa CCM, Serikali zilizoundwa zimeendelea kusimamia na
kuimarisha umoja wa Wananchi wake. Pamoja na tofauti zozote za kijamii na
kisiasa zilizopo, kwa jitihada maalumu za Serikali za CCM bado Wazanzibari ni
wamoja.
iii.Kupiga vita ubaguzi: Usawa wa binaadamu wote umeendelea kuwa msingi mkuu wa Mapinduzi ya
Zanzibar kupitia itikadi ya ASP iliyoenziwa na CCM katika uhai wake wa miaka 39
tunayoiadhimisha. Nasaba, rangi ya ngozi na Imani ya dini ya mtu sio vigezo
katika uanachama wala kushika uongozi katika CCM. Matokeo ya kuenziwa msingi
huu wa usawa wa binaadamu wote ni kuwa leo hii sura ya mchanganyiko wa viongozi
na wagombea wenye asili tofauti ni kubwa katika CCM kuliko ilivyo katika chama
chengine chochote cha siasa hapa nchini. Sisi wanataaluma tunajivunia msingi
huu wa usawa usio na ubaguzi.
Nje ya nchi, CCM kinatambulika kwa mwelekeo wake thabiti na
usioyumba wa kuhimiza muungano wa Afrika kwa maslahi ya Waafrika wote. Afrika
ina watu wenye asili tofauti, Waarabu upande wa Kaskazini, mchanganyiko wa
weusi na weupe Kusini mwa Afrika na weusi na wenye asili ya Asia kwa maeneo
yaliyobakia. CCM imeendelea kuhimiza umoja, mshikamano na muungano Waafrika
wote bila ya kujali tofauti hizo.
iv. Mfano wa Demokrasia: CCM katika uhai wake wote wa miaka
39 kimeendelea kuwa kioo cha misingi ya demokrasia, sio tu ndani ya chama bali
hata nje. CCM ndio chama ambacho uongozi wake wa ngazi zote umebadilika sana
kwa njia za kidemokrasia kuliko chama chochote nchini tokea kurejeshwa siasa za
ushindani wa vyama vingi. Utaratibu wa kupata uongozi ndani ya Chama umeendelea
kuwa wa wazi, wenye kutoa fursa sawa kwa kila mwanachama na pamoja na kuleta
changamoto kwa uwazi wake, umeendelea kukipatia Chama, na Serikali kinazounda,
viongozi imara.
v. Huduma za Jamii: Pamoja na idadi ya wananchi wa Zanzibar kuongezeka kwa kasi kubwa sana
katika uhai wan chi yetu na uongozi wa CCM, bado CCM imeunda na kusimamia
Serikali zilizoweka mkazo katika kutoa huduma bora kwa wananchi wote. Kwa sisi
wanashirikisho la elimu ya vyuo vikuu, tunashukuru kuwa chini ya Serikali za
CCM, watoto wa wanyonge tumeendelea kupata elimu hadi ya chuo kikuu. Inajulikana
kuwa kabla ya Mapinduzi fursa za Elimu hazikua sawa ambapo wananchi walio wengi
walitengwa, kwa njia mbalimbali, na hivyo kutofaidika na huduma hii muhimu kwa
kumkomboa mwanaadamu.
Sisi wanataaluma
tunatambua kuwa chama cha mapinduzi kimeleta maendeleo kupia sekta mbali mbali
ikiwemo makaazi bora, huduma za afya, kuimarika kwa miundombinu, upatikanaji wa
habari, maji safi na salama, michezo, sanaa n.k
Ndugu wanahabari,
Pamoja na mafanikio yote hayo ya
kijamii na kisiasa, bado tunahitaji Amani, umoja na utulivu katika nchi yetu.
Kwamba jana tumekuwa navyo sio uhakika kuwa na kesho vitakuwepo. Vinapaswa
kulindwa na wananchi sote. Kwa mnasaba huu, naomba kugusia kidogo hali ya
kisiasa na kijamii iliyojitokeza nchini kutokana na Uchaguzi Mkuu uliofanyika
tarehe 25 Oktoba mwaka jana, 2015 ambao kwa sababu zilizoelezwa na Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi, Mhe. Jecha Salim Jecha, matokeo yake yalifutwa. Sote
tumesikia taarifa ya Tume hiyo ya Uchaguzi kuwa sasa uchaguzi huo utafanyika
tena tarehe 20 Machi mwaka huu. Kwa mtazamo wetu, uamuzi huu wa Tume ya
Uchaguzi unatoa fursa ya kurekebisha kasoro zote zilizotajwa na Tume na
kupelekea kufuta matokeo ya uchaguzi wa awali. Pia, unatoa fursa kwa nchi yetu
kuendelea kupata uongozi wa miaka mitano ijayo kwa njia ya kidemokrasia.
Tumesikia baadhi ya vyama vya siasa
vikisema kuwa havitashiriki uchaguzi huo. Kama sehemu muhimu ya jamii yetu,
tunaomba vyama hivyo vitafakari tena kauli zake hizo na matokeo na athari yake
kwa mustakabali wa Amani na utulivu wetu. Wananchi, na hasa sisi vijana,
tusidanganywe tena na wanasiasa. Tunapaswa pia kujali maisha yetu na familia
zetu na kutoshajiika na aina yoyote ya vitendo vya uvunjifu wa amani. Wanashirikisho
tumefurahishwa na kauli ya CCM inayosema kuwa kitashiriki uchaguzi huo. Kwetu,
kauli hii inathibitisha udhati wa CCM wa kupenda amani na utulivu wa nchi na
wananchi wake.
Sisi wana shirikisho hatuoni njia
nyengine mbadala, ya salama na ya mkato, ya kupata ufumbuzi wa hali iliyopo
sasa. Hata vyama vikiongea kwa muda mrefu kiasi gani vitapaswa hatimae kurudi
tena kwenye utaratibu wa Kikatiba, wa kuchagua viongozi kupitia sanduku la
kura.
Tunaomba kuchukua fursa hii kutoa
wito kwa vyama vyote, viongozi na wanachama wake, kuonesha ukomavu wa kisiasa,
utayari wa kuongoza - dola na Wazanzibari sote - kwa kuacha jazba za kisiasa na
malumbano yasio na tija na badala yake kushiriki tena uchaguzi wa marejeo kwa
tarehe iliyopangwa na Tume. Wananchi, wanachama na wapenzi wa kila mgombea
watawapigia kura na kumaliza sintofahamu iliyojitokeza na kupata washindi
halali kwa majimbo yote.
Ni matumaini yetu Tume ya Uchaguzi na
taasisi zote za Kidemokrasia zimesharekebisha kasoro zote zilizobainishwa
katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 na kwamba maandalizi ya uchaguzi wa
marejeo yatakamilishwa vyema.
Kwa jamii ya Kimataifa, tunaamini pia
kuwa hali ya kisiasa ya Zanzibar na kwengineko barani Afrika inaendelea kutoa
somo muhimu katika mashirikiano yetu. Somo hili ni kwamba haifai kwa jumuiya
hiyo kushabikia na kuegemea upande wowote katika siasa za ndani za nchi, hata
nchi ndogo kama Zanzibar. Tumesikia maazimio ya Chama kimoja cha Siasa likiwemo
linalolitaka Jumuiya hiyo eti kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua watu
wanaofanya uvunjifu wa Amani hapa Zanzibar. Kama jumuiya hiyo ipo makini kama
inavyopaswa iwe, tunaamini ina matukio na ushaidi wote wa matukio ya uvunjifu
huo wa amani, na inawajua wahusika wake wakuu. Sote tunajua kuwa matukio haya
hayakutokea wakati wa uchaguzi huu tu, yapo muda mrefu na tunayo orodha yake.
Tuko tayari kuisaidia Jumuiya makini ya Kimataifa ikihitaji kufanya uchunguzi
uliyoombwa.
Kwa kumalizia, naomba nikumbushe tena
kuwa sisi tumo katika maadhimisho miaka 39 ya uhai na uwepo wa Chama chetu,
CCM. Naomba kutaarifu umma, hususan vijana, kuwa katika kuadhimisha kutimia
miaka 39 ya CCM, Shirikisho la vyuo vya Elimu ya juu CCM – Zanzibar limeandaa kongamano
la aina yake litakalofanyika katika ukumbi wa Salama wa hoteli ya Bwawani siku
ya Alkhamis tarehe 4 Februari mwaka huu, 2015. Lengo la Kongamano hilo ni
kutathmini hali ya kisiasa na Chama, tulikotoka, tulipo na tuendako. Ni vyema
kufuatilia yatakayoendelea katika Kongamano hilo tunalotarajia kurushwa moja
kwa moja na vyombo vya habari.
Nawatakia Wanachama na wapenzi wote
wa CCM na wapenda Amani nchini maadhimisho mema ya miaka 39 ya CCM na uchaguzi
wa Amani na salama tarehe 20 Machi mwaka huu.
Ahsanteni kwa kuniskiliza
Taarifa hii imetolewa na Shirikisho
la Vyuo Vya Elimu ya Juu CCM- Zanzibar
3 Februari 2015.
“KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI”
No comments:
Post a Comment