tangazo

tangazo

Saturday, October 31, 2015

CHAMA CHA WANANCHI CUF CHATOWA SIKU TATU KWA ZEC

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Chama hicho Mtendeni mjini Zanzibar

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema hakuna malalamiko yoyote yaliyowasilishwa katika siku ya upigaji kura.

Maalim Seif ambaye ni Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo taarifa kuwa mawakala wa CCM wameitwa pamoja na maofisa wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) katika kiwanda cha Makonyo Wilaya ya Chake Chake, kwa ajili ya kujazishwa fomu za malalamiko ili ziweze kutumika kudai kuwa yalikuwepo malalamiko katika zoezi hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Chama hicho zilizoko Mtendeni Mjini Zanzibar, Maalim Seif amesema njama hizo za CCM wameshazigundua na kawatozikubali.

Amesema njia pekee ya kuondosha utatanishi wa uchaguzi huo ni kukamilisha uhakiki wa majumuisho na kutangaza matokeo ya uchaguzi huo.

Amesema kwa upande wake pamoja na Chama chake, wataendeleza jitihada za kulipatia ufumbuzi suala hilo kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa, ili kukamilisha uhakiki wa majumuisho ya kura kwa majimbo 14 yaliyobaki na hatimaye kutangazwa mshindi wa Urais si zaidi ya tarehe 02/11/2015.

Hata hivyo amesema iwapo hakutokuwa na hatua zozote zilizochukuliwa kukamilisha uchaguzi huo na kuheshimu maamuzi ya wananchi walio wengi hadi ifikapo tarehe 01/11/2015, viongozi wa CUF wataondoa mkono wao na kuwaachia wananchi waweze kutafuta haki yao kwa njia za amani.

Katika hatua nyengine Maalim Seif ameelezea kusikitishwa na vitendo vinavyofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama kwa kuwatesa na kuwapiga raia wasiokuwa na hatia katika makaazi yao.

Amesema matukio hayo yamekuwa yakiripotiwa zaidi katika Wilaya za Magharibi “A na B”, na katika tukio la hivi karibuni amesema nyumba za raia wasiokuwa na hatia zimechomwa moto katika kisiwa cha Tumbatu na kuwafanya wananchi kuanza kupoteza uvumilivu.

Friday, October 30, 2015

 
 30 Oktoba, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu waandishi,
 tumewaita hapa ili kuzungumza nanyi juu ya jambo moja muhimu linalohusu nchi yetu. Kama mnavyojua kuwa juzi tarehe 28 Oktoba, 2015 alikaririwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Bwana Jecha Salim Jecha kupitia vyombo vya Habari kuwa matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar yamefutwa na kwamba kuna haja ya kufanyika Uchaguzi mwengine.
Ndugu Waandishi,
Tamko hilo limekuja wakati Tume ikiwa inaendelea na zoezi la Kufanya Majumuisho ya Kura za Urais na Jamii ya Wazanzibari na wadau wengine ndani na nje ya Nchi wakiwa wanasubiria kutangazwa kwa Mshindi wa kiti cha Urais katika uchaguzi uliofanyika Tarehe 25 Oktoba. 2015. Katika Tamko lake, Mwenyekiti alitoa sababu 9 zilizopelekea kuchelewa kwa utoaji wa Matokeo hayo na ambazo ndio zilizomfanya Mwenyekiti Huyo kuufuta Uchaguzi huo. Sisi, Kama Chama Cha Wanasheria Zanzibar tumefadhaishwa na uamuzi huo hasa kwa kuzingatia mamlaka aliyonayo Mwenyekiti huyo kisheria katika kufikia Uamuzi kama huo. Chama cha Wanasheria kimepitia kwa umakini Katiba ya Zanzibar ya 1984 na Sheria ya Uchaguzi Nambari 11 ya 1984 ili kujiridhisha kama Mwenyekiti anao uwezo wa Kufuta matokeo ya Uchaguzi kama alivyoeleza kwenye tamko lake na kama sababu zilizoelezwa zinakidhi kufutwakwaUchaguzi Nchi nzima.
Ndugu Waandishi,
 Kwa Mujibu wa Ibara ya 119 (1) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984, Tume ni Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wengine Sita kama walivyoanishwa na ibara hiyo na kwamba maamuzi yoyote ya Tume lazima yaungwe Mkono na wajumbe waliowengi. Taarifa iliyotolewa na wajumbe wawili wa Tume Ndugu Nassor Khamis na Ndugu Ayoub Bakari kwa Waandishi wa Habari kuwa hakukuwa na kikao chochote kilichokaa na kufikia maamuzi ya Kufuta Uchaguzi wa Zanzibar kauli ambayo haijapingwa mpaka sasa na wajumbe wengine wa Tume, kinaleta taswira ya wazi kuwa Maamuzi hayo hayakuwa ya Tume bali ni ya Mtu mmoja ambaye ni Mwenyekiti, Hivyo kuyafanya kuwa ni Batili mbele ya macho ya Sheria.
Ndugu Waandishi
, Kanuni ya 41(1) imeweka wazi utaratibu kufutwa kwa siku ya uchaguzi na kutangazwa siku nyengine na namna uamuzi huo utakavyofikiwa na sio kufuta matokeo ya Uchaguzi au Uchaguzi wenyewe. Ni kwa bahati mbaya sana Mwenyekiti katika Tamko lake hakueleza kama utaratibu umefatwa. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa Sheria.


Ndugu Waandishi,
 katika Tamko lake Mwenyekiti ameeleza kufuta matokeo yote ya Uchaguzi wa Zanzibar  jambo ambalo ni kinyume na Sheria na Katiba. Kwa mfano katika ngazi ya Majimbo kwa uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la wawakilishi na Madiwani, Tume inawakilishwa na Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Wilaya ambae kwa Mujibu wa Sheria ndio mwenye mamlaka ya kutangaza Mshindi katika Uchaguzi wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani na Kwa Mujibu wa Sheria Tume haina uwezo wala Mamlaka ya kufuta matokeo yaliyokwisha tangazwa na ambapo mgombea ameshapewa shahada ya kuchaguliwa. Wajibu wa Tume ni kuchapisha matokeo hayo kwenye gazeti la serikali kama kanuni ya 59 (4) na kifungu cha 88 (c) cha Sheria ya Uchaguzi vinavyoeleza na kama kuna Mgombea ambae hajaridhika na matokeo au maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi basi anatakiwa kwenda Mahakama Kuu kwa mujibu wa kifungu cha 86 cha Sheria ya Uchaguzi na Ibara ya 72 (1) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 ambayo ndio yenye Mamlaka ya kufuta uchaguzi na matokeo yake kwa Mujibu.
Ndugu waandishi,
 athari ya Tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar yanaweza kuiingiza Nchi katika mgogoro wa Mkubwa wa Kikatiba katika maeneo yafuatayo:- 1.

Muda wa kushika madaraka yaUrais Kikatiba:
 Ibara ya 28 (2) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 inaeleza wazi kuwa Rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia tarehe alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais. Tafsiri yake yake nikuwatangu Rais wa Zanzibar alipokula kiapo cha uaminifu na Kiapo cha kuwa Rais siku ya Tarehe 3 Novemba, 2010 atakuwa ametimiza miaka mitano siku ya Tarehe 3 Novemba, 2015. Hivyo akiendelea kushikilia madaraka ya Urais zaidi ya Tarehe hiyo itakuwa kinyume na Katiba ya Nchi. Upo mjadala katika jamii kuwa Rais anao uhalali wa kuendelea kuwa Rais chini ya Ibara ya 28 (1) (a). Maoni ya Chama cha Wanasheria Zanzibar ni kuwa maudhui ya Ibara hiyo ni kumpa uwezo wa Kikatiba Rais kuendelea ili kutoa nafasi ya maandalizi ya kula kiapo kwa Rais mpya(anaefuata) tu na sio kuendelea kukaa madarakani bila ya kufanyika kwa Uchaguzi au kwa sababu ya Uchaguzi kufutwa. 2.

Nchi kuendeshwa bila ya Baraza la Wawakilishi
: Katika mazingira tuliyonayo ni wazi kuwa Nchi itaendeshwa muda mrefu bila ya kuwepo kwa Baraza la Wawakilishi ambalo ni mhimili muhimu katika uendeshaji wa Serikali. Katiba yetu imeruhusu hali ya kuendesha Nchi bila ya Baraza la Wawakilishi kwa muda usiozidi siku tisini (90) tu kuanzia siku Baraza lilipovunjwa. Kwa mazingira tuliyonayo, siku tisini (90) zinazokubalika kikatiba zinaishia tarehe 12 Novemba, 2015 kwa kuwa Baraza la Wawakilishi lilivunjwa tarehe 13 Agosti, 2015. 3.

Hatari ya kuwa na Rais ambaye yuko juu ya Sheria na Katiba ya Nchi
: Ibara ya 37 ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 inaipa Mamlaka Baraza la Wawakilishi kuondoa kinga ya Rais kutoshtakiwa anapokuwa madarakani kama inavyotolewa na Ibara ya 36 ya Katiba. Katika mazingira tuliyonayo ambapo ifikapo tarehe 12 Novemba, 2015 ambapo Baraza la Wawakilishi halitakuwepo na haliwezi kuitishwa kikatiba, ni wazi kuwa ikiwa Rais atafanya matendo yoyote yenye kuvunja katiba ya Nchi na kukiuka Kiapo chake, hakutakuwa na Mamlaka nyengine yoyote yenye uwezo wa kuhoji matendo ya Rais. Hii inatengeneza hatari ya kuwa na Serikali inayoongozwa na Dikteta.

SULUHISHO:

Ndugu Waandishi,
 Chama cha Wanasheria Zanzibar kinaungana na wadau wengine wa ndani na nje ya Nchi ya kutoa wito kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar na wadau wengine kufanya yafuatayo:- 1.

Kufuta Tamko la Mwenyekiti wa Tume la kujaribu kufuta uchaguzi na matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwa kuwa halina nguvu kisheria na linaweza kuhatarisha Amani ya nchi. 2.

Kuendelea kutoka pale ilipoishia katika kazi ya kufanya majumuisho ya Kura za Urais ili mshindi halali wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 apatikane na kutangazwa kuwa Rais 3.

Rais aone haja ya kuunda Tume ya kumchunguza Mwenyekiti dhidi ya madai ya kushindwa kufanya kazi zake na ikiwa madai hayo yakithibitika, basi amuondoe mara moja. 4.

Vyombo vya Dola vichunguze, wawakamate na hatimae kuwafikisha Mahakamani watu wote waliohusika kumshinikiza Mwenyekiti kutoa tamko la kufuta uchaguzi na matokeo yake. 5.

Viongozi wote wa vyama vya siasa kujitathmini wajibu wao katika kuheshimu maamuzi ya wananchi yanayofanywa kwa njia ya demokrasia ili kujenga misingi mizuri ya utawala bora.
MWISHO:
Ni matumaini ya Chama cha Wanasheria Zanzibar kuwa Rais wetu wa Zanzibar atang’amua mtego huu
unaokusudia kumuweka katika Historia ya Rais wa Zanzibar aliewahi kuvunja Katiba ya Nchi na kumuondolea rekodi nzuri aliyonayo ya kuheshimu sheria na Katiba ya Nchi na Utawala Bora

CHANZO ZANZIBAR YETU

MWENYEKITI WA TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR ATAKIWA AJIUZULU

Vyama sita vya siasa vimemtaka Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha kujiuzulu kwa kukiuka katiba ya uchaguzi na kutaka kuiingiza nchi katika machafuko.

Vyama hivyo ni pamoja na Demokrasia Makini, SAU, CHAUMA, NRA, Jahazi Asilia, na DP ambao wamezungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa hoteli ya Grand Palace iliyopo Malindi Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Akizungumza na katika mkutano huo Mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CHAUMA, Abdallah Kombo Khamis alisema wao kama wana siasa na ni wazanzibari hawapo tayari kuona demokrasia inavizwa wakakaa bila ya kutoa tamko lolote.

“Kwa vyovyote vile iwavyo, hatutakubali uvizwaji wa demokrasia wa aina yoyote, kwamba kwa kuwa matokeo tulioyoyataja kutokwenda sambamba na matarajio ya CCM, mwenyekiti wa ZEC amekubali kutumika kukinusuru chama cha CCM ambacho yeye ni mwanachama aliyewahi kuwania ubunge kupitia chama hicho”  alisema Mgombea huyo.

Wamesema sababu alizozotoa Mwneyekiti wa tume ambazo zimepelekea kufutwa kwa uchaguzi huo zilikuwemo ndani ya uwezo wa tume yake kuzifanyia marekebisho hata kabla hazijaathiri zoezi la uchaguzi wote katika hatua ya mwisho.

Alisema Mwenyekiti huyo ameshindwa kuchukua hatua mwafaka muda uliofaa katika mambo yaliokuwa ndani ya mamlaka yake unatia mashaka juu ya ukweli wa hoja zake.

“Zaidi ya yote ametoa maelezo jumla jumla hakuainisha ni eneo lipi hasa lililohusika ili na wadau wengine wakajiridhisha na maelezo yake, hili linatia shaka” alisema.

Mgombea huyo ambaye aliambatana na wagombea wenzake wa vyama vilivyounda umoja huo kwa ajili ya kutoa yamko lao la kupingana na Mwenyekiti wa Tume  mbali ya kulaani tukio la Mwneyekiti lakini pia wanaona uamuzi wake huo utaathiri matokeo ya uchaguzi wa Muungano.

“Huku demokrasia ikipindwa katika kiwango hicho, mitaani wananchi wamekuwa wakipata mateso ya kupigwa na kuumizwa vibaya pasipo na sababu kunakofanywa na vikosi vya ulinzi, vitendo hivi ni uvunjifu mkubwa wa haki za binaadam na haki za watu hivyo tunaiomba serikali ichukua hatua kusitisha mara moja mateso kwa raia zake” aliongea kwa uchungu Khamis.

Walisema khofu yao uchaguzi utakaofutwa na kurejeshwa tena hali ya wananchi itakuwa tete zaidi nap engine kupelekea mauaji kama yaliowahi kutokea katika chaguzi zilizopita.

“Sisi tukiwa miongoni mwa wagombea urais wa Zanzibar hatujaridhika na maamuzi pweke ya Jecha na hivyo tunaitaka ZEC ikae katika kikao halali cha tume iyoe tamko ya kufuta kauli ya Mwenyekiti wao na kueleza umaliziaji wa hatua iliyobaki ya majumuisho na matangazo ya uchaguzi wa nafasi ya urais wa Zanzibar ili aliyeshinda apewe haki yake katika njia ya kidemokrasia ili nchi yetu idumu hali ya Amani na utulivu” aliongeza.

Mgombea huyo alisema suala la uchaguzi lina gharama kubwa ambapo Zanzibar imetumia shilingi bilioni 7.5 kwa ajili ya uchaguzi hivyo kuijeresha tena Zanzibar ndani ya uchaguzi ni kuingia tena kwenye gharama kuliangamiza taifa.

“Tunaziomba jumuiya za kimataifa na taasisi nyengine kusaidia kulimaliza tatizo la uchaguzi huu kwa kuhakikisha kuwa aliyeshinda anapewa haki yake ili Amani iendelee kudumu Zanzibar” alisema Khamis.

Aidha mgombea huo aliitaka tume ya uchaguzi Zanzibar kuendelea na mchakato na kutangaza matokeo ya uchaguzi huo kwa mujibu wa fomu zilizokusanywa katika vituo vya kupigia kura.

Pia mgombea huyo aliiomba tume ya kimataifa na mashirika ya maendeleo kuingilia kati suala hilo kwa kutumia waangalizi wa jumuiya mbali mbali zilizoshiriki katika uchaguzi huu ambapo wao wanaweza kupata taarifa kamili na za uhakika.

Katika kutoa wito wamewataka wazanzibari wote bila ya kujali itikadi za kisiasa kuwa tayari kupigania haki zao na kuhakikisha demokrasia inachukua nafasi yake kwa lengo la kuimarisha na kukuza ustawi wa Zanzibar na watu wake.

CHANZO ZANZIBAR YETU

Msajili wa vyama vya siasa Tanzania Jaji Francis Mutungi, amesema kuna umuhimu kwa viongozi wa vyama vya siasa Zanzibar kukutana, ili kutatua mzozo wa kisiasa uliojitokeza.

Amesema Zanzibar ni nchi amani, hivyo hakuna haja ya kuruhusu migogoro ya aina hiyo ambayo inaweza kupelekea kuvurugika kwa amani na kuipotezea sifa Zanzibar katika jamii ya Kimataifa.<

Jaji Mutungi akiambatana na baadhi ya wajumbe wa ofisi hiyo ya msajili pamoja na msajili wa vyama kwa upande wa Zanzibar Bw. Rajab Baraka, ametoa ushauri huo wakati akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, nyumbani kwake Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Amesema kuna kila sababu ya kulinusuru taifa kuingia katika migogoro isiyokuwa ya lazima, na kutaka juhudi za makusudi zichukuliwe ili kumaliza tatizo hilo.

Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ni mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF, amesema amekuwa akichukua juhudi binafsi kukutana na wagombea wenzake kuzungumzia tatizo hilo, lakini baadhi yao wanaonekana kutokuwa tayari kulizungumza.

Amesema hapendi kuona Zanzibar inaingia katika machafuko yanayoweza kuepukwa, na kwamba viongozi wengine pia wanapaswa kufikiria amani na maslahi ya Zanzibar kuliko maslahi binafsi.

Katika hatua nyengine Maalim Seif amemshutumu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Bw. Jecha Salim Jecha kwa kuiingiza nchi katika migogoro ya kisiasa na kikatiba.


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akigana na baadhi ya wajumbe wa Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa Tanzania baada ya mazungumzo yao, nyumbani kwake Mbweni Zanzibar

Akinukuu vipengele vya Katiba ya Zanzibar, Maalim Seif amesema kipindi cha Urais wa Zanzibar ni miaka mitano kuanzia tarehe ya kuapishwa, hivyo kuanzia tarehe 02/11/2015 kipindi cha Urais wa Zanzibar awamu ya saba kitakuwa kimemalizika.

Hivyo amesema bila ya kuchukuliwa juhudi za dharura, kuanzia tarehe 02 mwezi ujao kwa mujibu wa katiba, Zanzibar itakuwa haina Rais, Serikali wala Baraza la Wawakilishi.

Tuesday, October 27, 2015

WAANGALIZI WA KIMATAIFA WASEMA KWA KIASI UCHAGUZI UMEENDA VIZURI

Waangalizi wa Umoja wa Ulaya wamesema uchaguzi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa umeendeshwa vizuri lakini kasoro kadhaa zimesababisha baadhi ya wanasiasa kutilia shaka uhuru wa Tume za Uchaguzi NEC na ZEC.
Katika tamko lao la awali mbele ya waandishi wa habari waangalizi hao wamesema kuwa uchaguzi wa mara hii ulikuwa na ushindani mkali huku kukishuhudiwa idadi kubwa ya watu wakijitokeza kupiga kura katika hali ya utulivu na amani.Waangalizi hao wamesema kuwa pamoja na kwamba tume hizo zilijiandaa vyema kufanikisha uchaguzi huo lakini kutokuwepo kwa dhana ya uwazi na kukosekana kwa maelezo muafaka kuhusu daftari la kudumu la wapiga kura kumesababisha kujitokeza kwa hisia mbaya kwa vyama vya siasa juu ya tume hiyo. Waangalizi hao wamesema kuwa mambo hayo kumesababisha pia kwa vyama vya siasa kupoteza imani juu ya mchakato huo wa uchaguzi.
Akisoma tamko hilo, Mwangalizi Mkuu wa Umoja huo wa Ulaya, Judith Sargentini, alisema kuwa alikaribisha namna ushindani mkubwa uliojitokeza kwenye uchaguzi wa safari hii, lakini akasisitiza kuwa tamko hilo ni la awali kwa vile bado shughuli za uchaguzi zinaendelea. “Napenda kusisitiza hili kwamba, taarifa hii inatolewa wakati ambapo kazi ya kujumlisha matokeo ingali ikiendelea, hivyo ifahamike kwamba taarifa hii siyo tamko la mwisho kuhusiana na tathmini ya waangalizi wa Umoja wa Ulaya," alisema Sargentini. "Tunavyozungumza waangalizi wetu wanaendelea kufuatilia zoezi la ujumlishaji wa matokeo.”
Umoja wa Ulaya ni sehemu ya waangalizi wa kimataifa walioko nchini kwa ajili ya kufuatilia uchaguzi huu ambao pia umeshuhudia baadhi ya vigogo wa kisiasa wakiangushwa kwenye majimbo yao. Waangalizi wengine ni pamoja na Umoja wa Afrika na wale kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC. Ama waangalizi hao wa Ulaya wamesema wataendelea kusalia nchini hadi hapo Novemba 15, katika kipindi hicho itajihusisha na majukumu kadhaa ikiwamo kukutana na vyama vya siasa, maofisa wa uchaguzi wa asasi za kiraia. Umoja huo umetuma jumla ya waangalizi 141 waliosambazwa katika vituo vyote 625 vya upigaji wa kura. Huu ni ujumbe mkubwa zaidi kuwahi kutumwa na umoja huo kufuatilia uchaguzi wa Tanzania.
CHANZO DW
Chama Cha Wananchi (CUF) kimemuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha juu ya ucheleweshaji wa utangazaji wa matokeo ya uchaguzi ambapo inaingia siku ya tatu sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya chama hicho Mtendeni Mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui alisema lengo la barua hiyo ni kutaka kujua lini na saa ngapi tume hiyo itatangaza matokeo yote pamoja na kumtangaza mshindi wa nafasi ya urais wa Zanzibar.
“Tunataka kujua ni lini  na saa ngapi mshindi wa nafasi ya urais wa Zanzibar atatangazwa” alisema Mazrui.
Kwa mujibu wa kifungu cha 42 (4) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanapaswa kutangazwa ndani ya kipindi cha siku tatu tokea siku ya kupiga kura.
“Tumemwambia Mwenyekiti wa tume kwenye barua yetu kwamba ni vyema sasa tukajua siku na wakati wa kutangaza matokeo hayo ili tujitayarishe na hatua zinazofuata, tumemwambia tunapenda pia kujua utaratibu wa kumuapisha Rais mpya mara baada ya matokeo kutangazwa” alisema Mazrui.
Hata hivyo CUF imemtaka Mwenyekiti awapatie majibu yanayoridhisha katika hatua hizo zilizobaki za uchaguzi mkuu huku wakitambua macho na masikio yote ya walimwengu yakiwaangalia na kusikiliza uchaguzi huu wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wake.
“Ulimwengu wote unatusikiliza sisi jinsi tutakavyokamilisha uchaguzi huu na kuheshimu maamuzi ya wananchi kupitia sanduku la kura.” Alisema.
Katika hatua nyengine chama hicho kimetoa wito kwa wanachama na wafuasi wa chama hicho na wazanzibari wote kwa ujumla kuendelea kubaki watulivu na kutunza Amani ya nchi, wakati CUF ikijiandaa kufanya kazi na kila mzanzibari bila ya kujali itikadi yake kwa lengo la ujenzi wa Zanzibar mpya.
Aidha chama hicho kimesema kimepata taarifa kwamba juzi usiku majira ya saa tatu usiku Mwneyekiti wa tume ya uchaguzi Zanzibar alisema anaumwa na hivyo kudai hawezi kusaini fomu za matokeo yaliokwisha kuhakikiwa na maafisa wa tumen a mawakala wa wagombea urais.
“Baada ya hapo Mwneyekiti akasita kuendelea na kazi ya kutangaza matokeo. Hadi jana (juzi) usiku ni matokeo ya majimbo 13 tu yaliokwisha kutangazwa” alisema Mazrui.
Alisema wameona kuna mkakati wa makusudi kwamba matokeo yote yaliotangazwa hadi sasa ni yale yanayotoka katika majimbo ambayo CCM iliongoza.
“Kati ya majimbo 13 yaliotangazwa matokeo jana, ni jimbo la Malindi tu ambalo CUF iliongoza ndilo ililiotangazwa, inashtaajabisha kuwa hadi sasa tume haijatangaza matokeo hata jimbo moja la Pemba” aliongeza Mazrui.
Alisema matokeo ya majimbo mengine maneno ya Unguja ambayo pamoja na lile la Malindi CUF imeongoza ambapo alisema jambo hilo haliashirii nia njema na wanaamini lina lengo la kuwafanya watu waamini kwamba CCM inaongoza uchaguzi huo jambo ambalo sio la kweli.
“Pengine kuna lengo la kuja kuyachakachua matokeo ya majimbo ambayo CUF iliongoza ili kulazimisha ushindi wa CCM ambao haupo” alisema.
CUF wanasema ucheleweshaji huo unaofanywa na tume ya uchaguzi hauna sababu yoyote na una lengo la kuwatia khofu wananchi wa Zanzibar na kuiweka nchi katika wasiwasi pasipo na sababu.
“Kama tunavyojua, kutokana na utaratibu uliowekwa na tume wa kupatikana kila chama kilichoweka mgombea, kupitia mawakala wetu nakala ya matokeo ya kila kituturi cha kupigia kura na nakala ya fomu ya majumuisho kwa kila jimbo sisi CUF tunayo” alisema Mazrui.
CUF ilisema haino sababu ya ucheleweshaji wa matokeo hasa kwa kuzingatia kura zilishahesabiwa na fomu za vituoni na za majumuisho kwa majimbo yote ya Unguja na Pemba kupatikana ambapo kila chama kimepewa nakala zake.
“Wananchi wa Zanzibar wamefanya maamuzi yao kwenye visanduku vya kura na sasa wana hamu ya kujua matokeo ya kazi yao nzuri” alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Wednesday, October 21, 2015

Najua mnataka kubadilisha maisha yenu, lakini Dk. Shein alishindwa kufanya hivyo na ili kuonyesha kuwa naweza kuwaboreshea maisha yenu...

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ameahidi kuwa kama atachaguliwa kushika nafasi hiyo, ataongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kufikia Sh. 450,000 kutoka Sh. 150,000 kwa mwezi.

Maalim Seif ambaye pia anaungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambavyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi na NLD, alisema atawaboreshea maisha wananchi wa visiwani Zanzibar wakiwamo Polisi na wanajeshi ili wafanye  kazi kwa ufanisi.

Alitoa ahadi hiyo wakati akifunga kampeni za urais Zanzibar kwenye uwanja wa Tibirizi kiswani Pemba jana.

Kadhalika, aliahidi kuongeza kima cha chini cha pensheni ya wazee na kufikia Sh. 200,000 kwa mwezi pamoja na kuwajengea nyumba za kuishi.

“Najua mnataka kubadilisha maisha yenu, lakini Dk. Shein alishindwa kufanya hivyo na ili kuonyesha kuwa naweza kuwaboreshea maisha yenu, nitahakikisha mishahara ya watumishi wa serikali inapanda hadi kufikia Sh. 450,000 kwa kima cha chini, pamoja na kuhakikisha wazee wanalipwa pensheni zao kuanzia Sh. 200,000 tofauti na wanavyopata sasa Sh. 20,000,” alisema Maalim Seif.

Aidha, alisema vijana wa Zanzibar wasio na ajira wanafikia 300,000, hivyo atahakikisha wote wanapata shughuli za kufanya.

Alisema kwanza atajenga bandari kubwa mbili, moja ya Pemba na Mkokotoni ambazo zote zitakuwa na uwezo wa kupokea mizigo moja kwa moja kutoka mataifa mengine.

“Wananchi wa Zanzibar wana umasikini uliopitiliza, nitahakikisha ninakuza uchumi imara, lengo ni kuifanya Zanzibar kuwa kama Singapore,” alisema.

Singapore ni miongoni mwa nchi tano iliyopiga hatua nzuri kimaendeleo katika Bara la Asia.

Pia aliahidi kuhakikisha serikali yake inajenga shule za kutosha ili wanafunzi wapate elimu bora pamoja na nyumba za walimu.

“Nitaboresha kuanzia shule za chekechea ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na pia walimu wa madarasa wataajiriwa na serikali ili waendelee kutoa elimu ya dini badala ya kutegemea wazee,” alisema Maalim Seif.

Vile vile, aliwaeleza kuwa ataendeleza Katiba mpya na kwa kuweka kipengele cha muundo wa Serikali Tatu badala ya mbili.

CHANZO: NIPASHE

KAMPENI ZA NYUMBA KWA NYUMBA ZAZUSHA BALAA

Watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametwangana makonde hadharani kwa kile kinachodaiwa kugombania kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba.

 Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita maeneo ya Lukobe na Kihonda Maghorofani, baada ya wafuasi wanaodhaniwa kuwa ni wa Chadema kuwakamata wafuasi wa CCM waliokuwa wakipita nyumba hadi nyumba kwa madai walikuwa wakiandikisha vitambulisho vya kupigia kura.

 Akizungumzia kuhusu tukio hilo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro, Fikiri Juma, alisema waliopigwa ni wanachama wa CCM ambao walikuwa wakifanya kampeni za nyumba kwa nyumba.

Hata hivyo, Juma alisema kampeni za namna hiyo si kosa na mgombea yeyote anaruhusiwa kuzifanya.

Alisema kuwa wakiwa katika shughuli hizo za kampeni eneo la Kihonda Maghorofani, kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chadema, waliwavamia wanachama hao na kuanza kuwapiga.

 Hata hivyo, alisema tayari taarifa hizo zimetolewa katika Kituo Kikuu cha Polisi na Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watu waliofanya tukio hilo.

 “Vijana wangu wamepigwa wakiwa kwenye kampeni, lakini tumeshatoa taarifa kwenye vyombo vya usalama na tunaviachia vyombo hivyo viwatafute wahusika waliotenda kosa hilo,” alisema Juma.

 Akizungumzia madai hayo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Morogoro, James Mkude, alisema watu hao wanaodhaniwa kuwa ni wa CCM walikuwa wakiwalaghai wananchi kwa kuandikisha vyama vyao vya siasa, namba zao za shahada za kupigia kura, namba zao za simu pamoja na kero zinazowakabili kwenye eneo hilo. Mkude amelitaka Jeshi la Polisi kutenda haki ili kuepusha uvunjifu wa amani.

Alisema kuwa tayari wametoa taarifa za matukio hayo ya uandikishaji wa shahada za kupigia kura kwa mtendaji wa kata hiyo ambaye alisema hana taarifa za kufanyika kwa shughuli hiyo na ndipo walipoamua kuwakamata wafuasi hao wa CCM.

Hata hivyo Mkude alisema licha ya viongozi wa Chadema kutoa taarifa za ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi unaofanywa na CCM, lakini wahusika hawachukuliwi hatua zozote.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Morogoro Mjini, Theresia Mahongo, alisema sheria hairuhusu kwa mtu yeyote kukusanya shahada za kupigia kura na kuvitaka vyama vya siasa kufuata sheria za uchaguzi.

Alisema kitendo hicho ni kosa la jinai na kwamba adhabu yake ni faini ya kati ya Sh.100,000 na 200,000 au kifungo cha miaka miwili ama vyote na kuwaonya wananchi kuacha kufanya hivyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

CHANZO: NIPASHE

Saturday, October 17, 2015

Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania, (JWTZ), wanaolinda Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi, wanatuhumiwa kuwatesa na kuwachapa viboko madereva na makondakta wa daladala wanaotumia kituo cha abiria cha Kisonge, mjini hapa.

Malalamiko hayo yamejitokeza siku moja tangu askari hao walipoanza ulinzi katika maeneo nyeti ya huduma za jamii.
Ulinzi huo umeanza siku chache kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.

Maeneo yanayolindwa na jeshi hilo ni kituo cha matangazo cha televisheni na radio vya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Bandari, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Mnara wa Kumbukumbu wa Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na Uwanja wa Michezo wa watoto, Kariakoo.

Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya madereva na makondakta wa daladala, walisema walianza kukamatwa na kupigwa jana saa 12:50 asubuhi, wakati magari ya abiria yaliposimama kuteremsha abiria katika kituo cha Kisonge, jirani na mnara huo katika mtaa wa Michenzani.

Walisema kila gari iliyosimama katika kituo hicho, abiria walitakiwa kuteremka na kutembea, kumalizia safari zao.
Shuhuda wa tukio hilo, Issa Hassan Shabani, mkazi wa Michenzani alisema, baada ya kuteremshwa dereva na kondakta walibaki na kuanza kuteswa wakitakiwa kuruka kichura na baadae kuchapwa viboko.

Watu walikusanyika kama wanatizama sinema wakati madereva wanachapwa na kupewa    adhabu      ya      kuruka      kichura, alisema.

Dereva Ali Hamd Faki, mkaazi wa Kinuni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, alisema alipofika katika kituo cha abiria cha Kisonge alitakiwa na askari wa JWTZ kuteremka pamoja na kondakta wake na kuulizwa kwanini amesimamisha gari karibu na eneo la mnara.

Tunapigwa na kuteswa bila hatia kama kituo cha abiria Kisonge kimefungwa kwanini serikali imeshindwa kutangaza wananchi tukapata kufahamu, alihoji Faki.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud,  alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema hana taarifa yoyote ya madereva na makondakta kupigwa na askari hao.

Alisema suala la kupanga vituo vya abiria ni jukumu linalosimamiwa na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ.

Kama kuna mabadiliko yoyote basi wao ndiyo watakuwa wanafahamu, alisema Waziri Aboud ambaye ni msemaji mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Hakuna mabadiliko ya vituo yaliyofanyika na suala vituo vya daladala vinaratibiwa na kusimamiwa na baraza la manispaa ndiyo wahusika, alisema Naibu waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Gavu.
Alisema mabadiliko yoyote ya vituo yanapofanyika lazima serikali itangaze kabla ya kuanza kutumika ili kuondosha usumbufu kwa wananchi.

Upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir, alisema hawana taarifa yoyote ya kufanyika kwa mabadiliko ya vituo vya Daladala    katika        Manispaa ya Mji wa Zanzibar.

Kabla ya JWTZ kuanza kulinda maeneo hayo, yalikuwa yakilindwa na askari wa Kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), ambapo pia huduma za kibenki zimeathirika kwa watu wanaotumia mashine za ATM, zilizowekwa katika mnara huo.
CHANZO: NIPASHE