30 Oktoba, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu waandishi,
tumewaita hapa ili kuzungumza nanyi juu ya jambo moja muhimu linalohusu nchi yetu. Kama mnavyojua kuwa juzi tarehe 28 Oktoba, 2015 alikaririwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Bwana Jecha Salim Jecha kupitia vyombo vya Habari kuwa matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar yamefutwa na kwamba kuna haja ya kufanyika Uchaguzi mwengine.
Ndugu Waandishi,
Tamko hilo limekuja wakati Tume ikiwa inaendelea na zoezi la Kufanya Majumuisho ya Kura za Urais na Jamii ya Wazanzibari na wadau wengine ndani na nje ya Nchi wakiwa wanasubiria kutangazwa kwa Mshindi wa kiti cha Urais katika uchaguzi uliofanyika Tarehe 25 Oktoba. 2015. Katika Tamko lake, Mwenyekiti alitoa sababu 9 zilizopelekea kuchelewa kwa utoaji wa Matokeo hayo na ambazo ndio zilizomfanya Mwenyekiti Huyo kuufuta Uchaguzi huo. Sisi, Kama Chama Cha Wanasheria Zanzibar tumefadhaishwa na uamuzi huo hasa kwa kuzingatia mamlaka aliyonayo Mwenyekiti huyo kisheria katika kufikia Uamuzi kama huo. Chama cha Wanasheria kimepitia kwa umakini Katiba ya Zanzibar ya 1984 na Sheria ya Uchaguzi Nambari 11 ya 1984 ili kujiridhisha kama Mwenyekiti anao uwezo wa Kufuta matokeo ya Uchaguzi kama alivyoeleza kwenye tamko lake na kama sababu zilizoelezwa zinakidhi kufutwakwaUchaguzi Nchi nzima.
Ndugu Waandishi,
Kwa Mujibu wa Ibara ya 119 (1) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984, Tume ni Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wengine Sita kama walivyoanishwa na ibara hiyo na kwamba maamuzi yoyote ya Tume lazima yaungwe Mkono na wajumbe waliowengi. Taarifa iliyotolewa na wajumbe wawili wa Tume Ndugu Nassor Khamis na Ndugu Ayoub Bakari kwa Waandishi wa Habari kuwa hakukuwa na kikao chochote kilichokaa na kufikia maamuzi ya Kufuta Uchaguzi wa Zanzibar kauli ambayo haijapingwa mpaka sasa na wajumbe wengine wa Tume, kinaleta taswira ya wazi kuwa Maamuzi hayo hayakuwa ya Tume bali ni ya Mtu mmoja ambaye ni Mwenyekiti, Hivyo kuyafanya kuwa ni Batili mbele ya macho ya Sheria.
Ndugu Waandishi
, Kanuni ya 41(1) imeweka wazi utaratibu kufutwa kwa siku ya uchaguzi na kutangazwa siku nyengine na namna uamuzi huo utakavyofikiwa na sio kufuta matokeo ya Uchaguzi au Uchaguzi wenyewe. Ni kwa bahati mbaya sana Mwenyekiti katika Tamko lake hakueleza kama utaratibu umefatwa. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa Sheria.
Ndugu Waandishi,
katika Tamko lake Mwenyekiti ameeleza kufuta matokeo yote ya Uchaguzi wa Zanzibar jambo ambalo ni kinyume na Sheria na Katiba. Kwa mfano katika ngazi ya Majimbo kwa uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la wawakilishi na Madiwani, Tume inawakilishwa na Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Wilaya ambae kwa Mujibu wa Sheria ndio mwenye mamlaka ya kutangaza Mshindi katika Uchaguzi wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani na Kwa Mujibu wa Sheria Tume haina uwezo wala Mamlaka ya kufuta matokeo yaliyokwisha tangazwa na ambapo mgombea ameshapewa shahada ya kuchaguliwa. Wajibu wa Tume ni kuchapisha matokeo hayo kwenye gazeti la serikali kama kanuni ya 59 (4) na kifungu cha 88 (c) cha Sheria ya Uchaguzi vinavyoeleza na kama kuna Mgombea ambae hajaridhika na matokeo au maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi basi anatakiwa kwenda Mahakama Kuu kwa mujibu wa kifungu cha 86 cha Sheria ya Uchaguzi na Ibara ya 72 (1) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 ambayo ndio yenye Mamlaka ya kufuta uchaguzi na matokeo yake kwa Mujibu.
Ndugu waandishi,
athari ya Tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar yanaweza kuiingiza Nchi katika mgogoro wa Mkubwa wa Kikatiba katika maeneo yafuatayo:- 1.
Muda wa kushika madaraka yaUrais Kikatiba:
Ibara ya 28 (2) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 inaeleza wazi kuwa Rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia tarehe alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais. Tafsiri yake yake nikuwatangu Rais wa Zanzibar alipokula kiapo cha uaminifu na Kiapo cha kuwa Rais siku ya Tarehe 3 Novemba, 2010 atakuwa ametimiza miaka mitano siku ya Tarehe 3 Novemba, 2015. Hivyo akiendelea kushikilia madaraka ya Urais zaidi ya Tarehe hiyo itakuwa kinyume na Katiba ya Nchi. Upo mjadala katika jamii kuwa Rais anao uhalali wa kuendelea kuwa Rais chini ya Ibara ya 28 (1) (a). Maoni ya Chama cha Wanasheria Zanzibar ni kuwa maudhui ya Ibara hiyo ni kumpa uwezo wa Kikatiba Rais kuendelea ili kutoa nafasi ya maandalizi ya kula kiapo kwa Rais mpya(anaefuata) tu na sio kuendelea kukaa madarakani bila ya kufanyika kwa Uchaguzi au kwa sababu ya Uchaguzi kufutwa. 2.
Nchi kuendeshwa bila ya Baraza la Wawakilishi
: Katika mazingira tuliyonayo ni wazi kuwa Nchi itaendeshwa muda mrefu bila ya kuwepo kwa Baraza la Wawakilishi ambalo ni mhimili muhimu katika uendeshaji wa Serikali. Katiba yetu imeruhusu hali ya kuendesha Nchi bila ya Baraza la Wawakilishi kwa muda usiozidi siku tisini (90) tu kuanzia siku Baraza lilipovunjwa. Kwa mazingira tuliyonayo, siku tisini (90) zinazokubalika kikatiba zinaishia tarehe 12 Novemba, 2015 kwa kuwa Baraza la Wawakilishi lilivunjwa tarehe 13 Agosti, 2015. 3.
Hatari ya kuwa na Rais ambaye yuko juu ya Sheria na Katiba ya Nchi
: Ibara ya 37 ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 inaipa Mamlaka Baraza la Wawakilishi kuondoa kinga ya Rais kutoshtakiwa anapokuwa madarakani kama inavyotolewa na Ibara ya 36 ya Katiba. Katika mazingira tuliyonayo ambapo ifikapo tarehe 12 Novemba, 2015 ambapo Baraza la Wawakilishi halitakuwepo na haliwezi kuitishwa kikatiba, ni wazi kuwa ikiwa Rais atafanya matendo yoyote yenye kuvunja katiba ya Nchi na kukiuka Kiapo chake, hakutakuwa na Mamlaka nyengine yoyote yenye uwezo wa kuhoji matendo ya Rais. Hii inatengeneza hatari ya kuwa na Serikali inayoongozwa na Dikteta.
SULUHISHO:
Ndugu Waandishi,
Chama cha Wanasheria Zanzibar kinaungana na wadau wengine wa ndani na nje ya Nchi ya kutoa wito kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar na wadau wengine kufanya yafuatayo:- 1.
Kufuta Tamko la Mwenyekiti wa Tume la kujaribu kufuta uchaguzi na matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwa kuwa halina nguvu kisheria na linaweza kuhatarisha Amani ya nchi. 2.
Kuendelea kutoka pale ilipoishia katika kazi ya kufanya majumuisho ya Kura za Urais ili mshindi halali wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 apatikane na kutangazwa kuwa Rais 3.
Rais aone haja ya kuunda Tume ya kumchunguza Mwenyekiti dhidi ya madai ya kushindwa kufanya kazi zake na ikiwa madai hayo yakithibitika, basi amuondoe mara moja. 4.
Vyombo vya Dola vichunguze, wawakamate na hatimae kuwafikisha Mahakamani watu wote waliohusika kumshinikiza Mwenyekiti kutoa tamko la kufuta uchaguzi na matokeo yake. 5.
Viongozi wote wa vyama vya siasa kujitathmini wajibu wao katika kuheshimu maamuzi ya wananchi yanayofanywa kwa njia ya demokrasia ili kujenga misingi mizuri ya utawala bora.
MWISHO:
Ni matumaini ya Chama cha Wanasheria Zanzibar kuwa Rais wetu wa Zanzibar atang’amua mtego huu
unaokusudia kumuweka katika Historia ya Rais wa Zanzibar aliewahi kuvunja Katiba ya Nchi na kumuondolea rekodi nzuri aliyonayo ya kuheshimu sheria na Katiba ya Nchi na Utawala Bora
CHANZO ZANZIBAR YETU
No comments:
Post a Comment