tangazo

tangazo

Wednesday, October 21, 2015

KAMPENI ZA NYUMBA KWA NYUMBA ZAZUSHA BALAA

Watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametwangana makonde hadharani kwa kile kinachodaiwa kugombania kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba.

 Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita maeneo ya Lukobe na Kihonda Maghorofani, baada ya wafuasi wanaodhaniwa kuwa ni wa Chadema kuwakamata wafuasi wa CCM waliokuwa wakipita nyumba hadi nyumba kwa madai walikuwa wakiandikisha vitambulisho vya kupigia kura.

 Akizungumzia kuhusu tukio hilo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro, Fikiri Juma, alisema waliopigwa ni wanachama wa CCM ambao walikuwa wakifanya kampeni za nyumba kwa nyumba.

Hata hivyo, Juma alisema kampeni za namna hiyo si kosa na mgombea yeyote anaruhusiwa kuzifanya.

Alisema kuwa wakiwa katika shughuli hizo za kampeni eneo la Kihonda Maghorofani, kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chadema, waliwavamia wanachama hao na kuanza kuwapiga.

 Hata hivyo, alisema tayari taarifa hizo zimetolewa katika Kituo Kikuu cha Polisi na Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watu waliofanya tukio hilo.

 “Vijana wangu wamepigwa wakiwa kwenye kampeni, lakini tumeshatoa taarifa kwenye vyombo vya usalama na tunaviachia vyombo hivyo viwatafute wahusika waliotenda kosa hilo,” alisema Juma.

 Akizungumzia madai hayo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Morogoro, James Mkude, alisema watu hao wanaodhaniwa kuwa ni wa CCM walikuwa wakiwalaghai wananchi kwa kuandikisha vyama vyao vya siasa, namba zao za shahada za kupigia kura, namba zao za simu pamoja na kero zinazowakabili kwenye eneo hilo. Mkude amelitaka Jeshi la Polisi kutenda haki ili kuepusha uvunjifu wa amani.

Alisema kuwa tayari wametoa taarifa za matukio hayo ya uandikishaji wa shahada za kupigia kura kwa mtendaji wa kata hiyo ambaye alisema hana taarifa za kufanyika kwa shughuli hiyo na ndipo walipoamua kuwakamata wafuasi hao wa CCM.

Hata hivyo Mkude alisema licha ya viongozi wa Chadema kutoa taarifa za ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi unaofanywa na CCM, lakini wahusika hawachukuliwi hatua zozote.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Morogoro Mjini, Theresia Mahongo, alisema sheria hairuhusu kwa mtu yeyote kukusanya shahada za kupigia kura na kuvitaka vyama vya siasa kufuata sheria za uchaguzi.

Alisema kitendo hicho ni kosa la jinai na kwamba adhabu yake ni faini ya kati ya Sh.100,000 na 200,000 au kifungo cha miaka miwili ama vyote na kuwaonya wananchi kuacha kufanya hivyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment