Najua mnataka kubadilisha maisha yenu, lakini Dk. Shein alishindwa kufanya hivyo na ili kuonyesha kuwa naweza kuwaboreshea maisha yenu...
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ameahidi kuwa kama atachaguliwa kushika nafasi hiyo, ataongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kufikia Sh. 450,000 kutoka Sh. 150,000 kwa mwezi.
Maalim Seif ambaye pia anaungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambavyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi na NLD, alisema atawaboreshea maisha wananchi wa visiwani Zanzibar wakiwamo Polisi na wanajeshi ili wafanye kazi kwa ufanisi.
Alitoa ahadi hiyo wakati akifunga kampeni za urais Zanzibar kwenye uwanja wa Tibirizi kiswani Pemba jana.
Kadhalika, aliahidi kuongeza kima cha chini cha pensheni ya wazee na kufikia Sh. 200,000 kwa mwezi pamoja na kuwajengea nyumba za kuishi.
“Najua mnataka kubadilisha maisha yenu, lakini Dk. Shein alishindwa kufanya hivyo na ili kuonyesha kuwa naweza kuwaboreshea maisha yenu, nitahakikisha mishahara ya watumishi wa serikali inapanda hadi kufikia Sh. 450,000 kwa kima cha chini, pamoja na kuhakikisha wazee wanalipwa pensheni zao kuanzia Sh. 200,000 tofauti na wanavyopata sasa Sh. 20,000,” alisema Maalim Seif.
Aidha, alisema vijana wa Zanzibar wasio na ajira wanafikia 300,000, hivyo atahakikisha wote wanapata shughuli za kufanya.
Alisema kwanza atajenga bandari kubwa mbili, moja ya Pemba na Mkokotoni ambazo zote zitakuwa na uwezo wa kupokea mizigo moja kwa moja kutoka mataifa mengine.
“Wananchi wa Zanzibar wana umasikini uliopitiliza, nitahakikisha ninakuza uchumi imara, lengo ni kuifanya Zanzibar kuwa kama Singapore,” alisema.
Singapore ni miongoni mwa nchi tano iliyopiga hatua nzuri kimaendeleo katika Bara la Asia.
Pia aliahidi kuhakikisha serikali yake inajenga shule za kutosha ili wanafunzi wapate elimu bora pamoja na nyumba za walimu.
“Nitaboresha kuanzia shule za chekechea ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na pia walimu wa madarasa wataajiriwa na serikali ili waendelee kutoa elimu ya dini badala ya kutegemea wazee,” alisema Maalim Seif.
Vile vile, aliwaeleza kuwa ataendeleza Katiba mpya na kwa kuweka kipengele cha muundo wa Serikali Tatu badala ya mbili.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment