tangazo

tangazo

Friday, October 30, 2015

MWENYEKITI WA TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR ATAKIWA AJIUZULU

Vyama sita vya siasa vimemtaka Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha kujiuzulu kwa kukiuka katiba ya uchaguzi na kutaka kuiingiza nchi katika machafuko.

Vyama hivyo ni pamoja na Demokrasia Makini, SAU, CHAUMA, NRA, Jahazi Asilia, na DP ambao wamezungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa hoteli ya Grand Palace iliyopo Malindi Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Akizungumza na katika mkutano huo Mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CHAUMA, Abdallah Kombo Khamis alisema wao kama wana siasa na ni wazanzibari hawapo tayari kuona demokrasia inavizwa wakakaa bila ya kutoa tamko lolote.

“Kwa vyovyote vile iwavyo, hatutakubali uvizwaji wa demokrasia wa aina yoyote, kwamba kwa kuwa matokeo tulioyoyataja kutokwenda sambamba na matarajio ya CCM, mwenyekiti wa ZEC amekubali kutumika kukinusuru chama cha CCM ambacho yeye ni mwanachama aliyewahi kuwania ubunge kupitia chama hicho”  alisema Mgombea huyo.

Wamesema sababu alizozotoa Mwneyekiti wa tume ambazo zimepelekea kufutwa kwa uchaguzi huo zilikuwemo ndani ya uwezo wa tume yake kuzifanyia marekebisho hata kabla hazijaathiri zoezi la uchaguzi wote katika hatua ya mwisho.

Alisema Mwenyekiti huyo ameshindwa kuchukua hatua mwafaka muda uliofaa katika mambo yaliokuwa ndani ya mamlaka yake unatia mashaka juu ya ukweli wa hoja zake.

“Zaidi ya yote ametoa maelezo jumla jumla hakuainisha ni eneo lipi hasa lililohusika ili na wadau wengine wakajiridhisha na maelezo yake, hili linatia shaka” alisema.

Mgombea huyo ambaye aliambatana na wagombea wenzake wa vyama vilivyounda umoja huo kwa ajili ya kutoa yamko lao la kupingana na Mwenyekiti wa Tume  mbali ya kulaani tukio la Mwneyekiti lakini pia wanaona uamuzi wake huo utaathiri matokeo ya uchaguzi wa Muungano.

“Huku demokrasia ikipindwa katika kiwango hicho, mitaani wananchi wamekuwa wakipata mateso ya kupigwa na kuumizwa vibaya pasipo na sababu kunakofanywa na vikosi vya ulinzi, vitendo hivi ni uvunjifu mkubwa wa haki za binaadam na haki za watu hivyo tunaiomba serikali ichukua hatua kusitisha mara moja mateso kwa raia zake” aliongea kwa uchungu Khamis.

Walisema khofu yao uchaguzi utakaofutwa na kurejeshwa tena hali ya wananchi itakuwa tete zaidi nap engine kupelekea mauaji kama yaliowahi kutokea katika chaguzi zilizopita.

“Sisi tukiwa miongoni mwa wagombea urais wa Zanzibar hatujaridhika na maamuzi pweke ya Jecha na hivyo tunaitaka ZEC ikae katika kikao halali cha tume iyoe tamko ya kufuta kauli ya Mwenyekiti wao na kueleza umaliziaji wa hatua iliyobaki ya majumuisho na matangazo ya uchaguzi wa nafasi ya urais wa Zanzibar ili aliyeshinda apewe haki yake katika njia ya kidemokrasia ili nchi yetu idumu hali ya Amani na utulivu” aliongeza.

Mgombea huyo alisema suala la uchaguzi lina gharama kubwa ambapo Zanzibar imetumia shilingi bilioni 7.5 kwa ajili ya uchaguzi hivyo kuijeresha tena Zanzibar ndani ya uchaguzi ni kuingia tena kwenye gharama kuliangamiza taifa.

“Tunaziomba jumuiya za kimataifa na taasisi nyengine kusaidia kulimaliza tatizo la uchaguzi huu kwa kuhakikisha kuwa aliyeshinda anapewa haki yake ili Amani iendelee kudumu Zanzibar” alisema Khamis.

Aidha mgombea huo aliitaka tume ya uchaguzi Zanzibar kuendelea na mchakato na kutangaza matokeo ya uchaguzi huo kwa mujibu wa fomu zilizokusanywa katika vituo vya kupigia kura.

Pia mgombea huyo aliiomba tume ya kimataifa na mashirika ya maendeleo kuingilia kati suala hilo kwa kutumia waangalizi wa jumuiya mbali mbali zilizoshiriki katika uchaguzi huu ambapo wao wanaweza kupata taarifa kamili na za uhakika.

Katika kutoa wito wamewataka wazanzibari wote bila ya kujali itikadi za kisiasa kuwa tayari kupigania haki zao na kuhakikisha demokrasia inachukua nafasi yake kwa lengo la kuimarisha na kukuza ustawi wa Zanzibar na watu wake.

CHANZO ZANZIBAR YETU

No comments:

Post a Comment