tangazo

tangazo

Tuesday, October 27, 2015

Chama Cha Wananchi (CUF) kimemuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha juu ya ucheleweshaji wa utangazaji wa matokeo ya uchaguzi ambapo inaingia siku ya tatu sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya chama hicho Mtendeni Mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui alisema lengo la barua hiyo ni kutaka kujua lini na saa ngapi tume hiyo itatangaza matokeo yote pamoja na kumtangaza mshindi wa nafasi ya urais wa Zanzibar.
“Tunataka kujua ni lini  na saa ngapi mshindi wa nafasi ya urais wa Zanzibar atatangazwa” alisema Mazrui.
Kwa mujibu wa kifungu cha 42 (4) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanapaswa kutangazwa ndani ya kipindi cha siku tatu tokea siku ya kupiga kura.
“Tumemwambia Mwenyekiti wa tume kwenye barua yetu kwamba ni vyema sasa tukajua siku na wakati wa kutangaza matokeo hayo ili tujitayarishe na hatua zinazofuata, tumemwambia tunapenda pia kujua utaratibu wa kumuapisha Rais mpya mara baada ya matokeo kutangazwa” alisema Mazrui.
Hata hivyo CUF imemtaka Mwenyekiti awapatie majibu yanayoridhisha katika hatua hizo zilizobaki za uchaguzi mkuu huku wakitambua macho na masikio yote ya walimwengu yakiwaangalia na kusikiliza uchaguzi huu wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wake.
“Ulimwengu wote unatusikiliza sisi jinsi tutakavyokamilisha uchaguzi huu na kuheshimu maamuzi ya wananchi kupitia sanduku la kura.” Alisema.
Katika hatua nyengine chama hicho kimetoa wito kwa wanachama na wafuasi wa chama hicho na wazanzibari wote kwa ujumla kuendelea kubaki watulivu na kutunza Amani ya nchi, wakati CUF ikijiandaa kufanya kazi na kila mzanzibari bila ya kujali itikadi yake kwa lengo la ujenzi wa Zanzibar mpya.
Aidha chama hicho kimesema kimepata taarifa kwamba juzi usiku majira ya saa tatu usiku Mwneyekiti wa tume ya uchaguzi Zanzibar alisema anaumwa na hivyo kudai hawezi kusaini fomu za matokeo yaliokwisha kuhakikiwa na maafisa wa tumen a mawakala wa wagombea urais.
“Baada ya hapo Mwneyekiti akasita kuendelea na kazi ya kutangaza matokeo. Hadi jana (juzi) usiku ni matokeo ya majimbo 13 tu yaliokwisha kutangazwa” alisema Mazrui.
Alisema wameona kuna mkakati wa makusudi kwamba matokeo yote yaliotangazwa hadi sasa ni yale yanayotoka katika majimbo ambayo CCM iliongoza.
“Kati ya majimbo 13 yaliotangazwa matokeo jana, ni jimbo la Malindi tu ambalo CUF iliongoza ndilo ililiotangazwa, inashtaajabisha kuwa hadi sasa tume haijatangaza matokeo hata jimbo moja la Pemba” aliongeza Mazrui.
Alisema matokeo ya majimbo mengine maneno ya Unguja ambayo pamoja na lile la Malindi CUF imeongoza ambapo alisema jambo hilo haliashirii nia njema na wanaamini lina lengo la kuwafanya watu waamini kwamba CCM inaongoza uchaguzi huo jambo ambalo sio la kweli.
“Pengine kuna lengo la kuja kuyachakachua matokeo ya majimbo ambayo CUF iliongoza ili kulazimisha ushindi wa CCM ambao haupo” alisema.
CUF wanasema ucheleweshaji huo unaofanywa na tume ya uchaguzi hauna sababu yoyote na una lengo la kuwatia khofu wananchi wa Zanzibar na kuiweka nchi katika wasiwasi pasipo na sababu.
“Kama tunavyojua, kutokana na utaratibu uliowekwa na tume wa kupatikana kila chama kilichoweka mgombea, kupitia mawakala wetu nakala ya matokeo ya kila kituturi cha kupigia kura na nakala ya fomu ya majumuisho kwa kila jimbo sisi CUF tunayo” alisema Mazrui.
CUF ilisema haino sababu ya ucheleweshaji wa matokeo hasa kwa kuzingatia kura zilishahesabiwa na fomu za vituoni na za majumuisho kwa majimbo yote ya Unguja na Pemba kupatikana ambapo kila chama kimepewa nakala zake.
“Wananchi wa Zanzibar wamefanya maamuzi yao kwenye visanduku vya kura na sasa wana hamu ya kujua matokeo ya kazi yao nzuri” alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Wednesday, October 21, 2015

Najua mnataka kubadilisha maisha yenu, lakini Dk. Shein alishindwa kufanya hivyo na ili kuonyesha kuwa naweza kuwaboreshea maisha yenu...

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ameahidi kuwa kama atachaguliwa kushika nafasi hiyo, ataongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kufikia Sh. 450,000 kutoka Sh. 150,000 kwa mwezi.

Maalim Seif ambaye pia anaungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambavyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi na NLD, alisema atawaboreshea maisha wananchi wa visiwani Zanzibar wakiwamo Polisi na wanajeshi ili wafanye  kazi kwa ufanisi.

Alitoa ahadi hiyo wakati akifunga kampeni za urais Zanzibar kwenye uwanja wa Tibirizi kiswani Pemba jana.

Kadhalika, aliahidi kuongeza kima cha chini cha pensheni ya wazee na kufikia Sh. 200,000 kwa mwezi pamoja na kuwajengea nyumba za kuishi.

“Najua mnataka kubadilisha maisha yenu, lakini Dk. Shein alishindwa kufanya hivyo na ili kuonyesha kuwa naweza kuwaboreshea maisha yenu, nitahakikisha mishahara ya watumishi wa serikali inapanda hadi kufikia Sh. 450,000 kwa kima cha chini, pamoja na kuhakikisha wazee wanalipwa pensheni zao kuanzia Sh. 200,000 tofauti na wanavyopata sasa Sh. 20,000,” alisema Maalim Seif.

Aidha, alisema vijana wa Zanzibar wasio na ajira wanafikia 300,000, hivyo atahakikisha wote wanapata shughuli za kufanya.

Alisema kwanza atajenga bandari kubwa mbili, moja ya Pemba na Mkokotoni ambazo zote zitakuwa na uwezo wa kupokea mizigo moja kwa moja kutoka mataifa mengine.

“Wananchi wa Zanzibar wana umasikini uliopitiliza, nitahakikisha ninakuza uchumi imara, lengo ni kuifanya Zanzibar kuwa kama Singapore,” alisema.

Singapore ni miongoni mwa nchi tano iliyopiga hatua nzuri kimaendeleo katika Bara la Asia.

Pia aliahidi kuhakikisha serikali yake inajenga shule za kutosha ili wanafunzi wapate elimu bora pamoja na nyumba za walimu.

“Nitaboresha kuanzia shule za chekechea ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na pia walimu wa madarasa wataajiriwa na serikali ili waendelee kutoa elimu ya dini badala ya kutegemea wazee,” alisema Maalim Seif.

Vile vile, aliwaeleza kuwa ataendeleza Katiba mpya na kwa kuweka kipengele cha muundo wa Serikali Tatu badala ya mbili.

CHANZO: NIPASHE

KAMPENI ZA NYUMBA KWA NYUMBA ZAZUSHA BALAA

Watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametwangana makonde hadharani kwa kile kinachodaiwa kugombania kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba.

 Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita maeneo ya Lukobe na Kihonda Maghorofani, baada ya wafuasi wanaodhaniwa kuwa ni wa Chadema kuwakamata wafuasi wa CCM waliokuwa wakipita nyumba hadi nyumba kwa madai walikuwa wakiandikisha vitambulisho vya kupigia kura.

 Akizungumzia kuhusu tukio hilo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro, Fikiri Juma, alisema waliopigwa ni wanachama wa CCM ambao walikuwa wakifanya kampeni za nyumba kwa nyumba.

Hata hivyo, Juma alisema kampeni za namna hiyo si kosa na mgombea yeyote anaruhusiwa kuzifanya.

Alisema kuwa wakiwa katika shughuli hizo za kampeni eneo la Kihonda Maghorofani, kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chadema, waliwavamia wanachama hao na kuanza kuwapiga.

 Hata hivyo, alisema tayari taarifa hizo zimetolewa katika Kituo Kikuu cha Polisi na Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watu waliofanya tukio hilo.

 “Vijana wangu wamepigwa wakiwa kwenye kampeni, lakini tumeshatoa taarifa kwenye vyombo vya usalama na tunaviachia vyombo hivyo viwatafute wahusika waliotenda kosa hilo,” alisema Juma.

 Akizungumzia madai hayo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Morogoro, James Mkude, alisema watu hao wanaodhaniwa kuwa ni wa CCM walikuwa wakiwalaghai wananchi kwa kuandikisha vyama vyao vya siasa, namba zao za shahada za kupigia kura, namba zao za simu pamoja na kero zinazowakabili kwenye eneo hilo. Mkude amelitaka Jeshi la Polisi kutenda haki ili kuepusha uvunjifu wa amani.

Alisema kuwa tayari wametoa taarifa za matukio hayo ya uandikishaji wa shahada za kupigia kura kwa mtendaji wa kata hiyo ambaye alisema hana taarifa za kufanyika kwa shughuli hiyo na ndipo walipoamua kuwakamata wafuasi hao wa CCM.

Hata hivyo Mkude alisema licha ya viongozi wa Chadema kutoa taarifa za ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi unaofanywa na CCM, lakini wahusika hawachukuliwi hatua zozote.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Morogoro Mjini, Theresia Mahongo, alisema sheria hairuhusu kwa mtu yeyote kukusanya shahada za kupigia kura na kuvitaka vyama vya siasa kufuata sheria za uchaguzi.

Alisema kitendo hicho ni kosa la jinai na kwamba adhabu yake ni faini ya kati ya Sh.100,000 na 200,000 au kifungo cha miaka miwili ama vyote na kuwaonya wananchi kuacha kufanya hivyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

CHANZO: NIPASHE

Saturday, October 17, 2015

Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania, (JWTZ), wanaolinda Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi, wanatuhumiwa kuwatesa na kuwachapa viboko madereva na makondakta wa daladala wanaotumia kituo cha abiria cha Kisonge, mjini hapa.

Malalamiko hayo yamejitokeza siku moja tangu askari hao walipoanza ulinzi katika maeneo nyeti ya huduma za jamii.
Ulinzi huo umeanza siku chache kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.

Maeneo yanayolindwa na jeshi hilo ni kituo cha matangazo cha televisheni na radio vya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Bandari, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Mnara wa Kumbukumbu wa Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na Uwanja wa Michezo wa watoto, Kariakoo.

Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya madereva na makondakta wa daladala, walisema walianza kukamatwa na kupigwa jana saa 12:50 asubuhi, wakati magari ya abiria yaliposimama kuteremsha abiria katika kituo cha Kisonge, jirani na mnara huo katika mtaa wa Michenzani.

Walisema kila gari iliyosimama katika kituo hicho, abiria walitakiwa kuteremka na kutembea, kumalizia safari zao.
Shuhuda wa tukio hilo, Issa Hassan Shabani, mkazi wa Michenzani alisema, baada ya kuteremshwa dereva na kondakta walibaki na kuanza kuteswa wakitakiwa kuruka kichura na baadae kuchapwa viboko.

Watu walikusanyika kama wanatizama sinema wakati madereva wanachapwa na kupewa    adhabu      ya      kuruka      kichura, alisema.

Dereva Ali Hamd Faki, mkaazi wa Kinuni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, alisema alipofika katika kituo cha abiria cha Kisonge alitakiwa na askari wa JWTZ kuteremka pamoja na kondakta wake na kuulizwa kwanini amesimamisha gari karibu na eneo la mnara.

Tunapigwa na kuteswa bila hatia kama kituo cha abiria Kisonge kimefungwa kwanini serikali imeshindwa kutangaza wananchi tukapata kufahamu, alihoji Faki.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud,  alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema hana taarifa yoyote ya madereva na makondakta kupigwa na askari hao.

Alisema suala la kupanga vituo vya abiria ni jukumu linalosimamiwa na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ.

Kama kuna mabadiliko yoyote basi wao ndiyo watakuwa wanafahamu, alisema Waziri Aboud ambaye ni msemaji mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Hakuna mabadiliko ya vituo yaliyofanyika na suala vituo vya daladala vinaratibiwa na kusimamiwa na baraza la manispaa ndiyo wahusika, alisema Naibu waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Gavu.
Alisema mabadiliko yoyote ya vituo yanapofanyika lazima serikali itangaze kabla ya kuanza kutumika ili kuondosha usumbufu kwa wananchi.

Upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir, alisema hawana taarifa yoyote ya kufanyika kwa mabadiliko ya vituo vya Daladala    katika        Manispaa ya Mji wa Zanzibar.

Kabla ya JWTZ kuanza kulinda maeneo hayo, yalikuwa yakilindwa na askari wa Kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), ambapo pia huduma za kibenki zimeathirika kwa watu wanaotumia mashine za ATM, zilizowekwa katika mnara huo.
CHANZO: NIPASHE

Wednesday, September 23, 2015

KUZIONA SIMBA NA YANGA NI SHILINGI ELFU SABA

Viingilio vya mchezo wa watani wa jadi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania utakaochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam vimetangazwa leo ambapo kiingilio cha chini kitakua ni shilingi elfu saba (7,000).
Katika mchezo huo kiingilio cha juu kitakua ni shilingi Elfu Thelathini (30,000) kwa viti vya VIP A, Elfu Ishirini (20,000) kwa viti vya VIP B & C, huku kiingilio cha shilingi Elfu Saba (7,000) kikiwa ni kwa viti vyenye rangi ya Blu, Kijani na Orange.
Tiketi za mchezo ho zitaanza kuuzwa siku ya Ijumaa saa 2 kamili asubuhi katika vituo vifuatavyo: Karume – Ofisi za TFF, Buguruni – Oilcom, Dar Live – Mbagala, Uwanja wa Taifa, Luther House – Posta, Ferry – Kivukoni, Mnazi Mmoja, Ubungo – Oilcom na Makumbusho – Standi ya mabasi ya daladala.
TFF inawaomba wapenzi, wadau na washabiki wa mpira wa miguu nchin kununua tiketi katika magari yaliyopo kwenye vituo vya kuuzia tiketi ili kuondokana na kuuziwa tiketi zisizo sahihi.
Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi wa kimataifa mwenye beji ya FIFA, Israel Nkongo (Dsm) akisaidiwa na Josephat Bulali (Tanga), Ferdinand Chacha (Mwanza) mwamuzi wa akiba Soud Lila (Dsm) wakati kamisaa wa mchezo huo atakua Charles Mchau kutoka Kilimanjaro.
Michezo mingine ya Ligi Kuu ya Vodacom siku hiyo ya Jumamosi itakua ni kati ya Coastal Union dhidi ya Mwadui FC katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Maafande wa jeshi la Magereza (Tanzania Prisons) watawakaribisha maafande wa Mgambo Shooting katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Maafande wa JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Stand United katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, huku wakata miwa wa Turiani Mtibwa Sugar watawakaribisha Majimjaji ya Songea katika uwanja wa Manungu wakati Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Toto Africans katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Ligi hiyo itaendelea siku ya Jumapili kwa michezo miwili ambapo waoka mikate wa Azam FC watawakaribisha Mbeya City katika uwanja wa Chamazi Complex, huku African Sports wakiwa wenyeji wa Ndanda FC kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

IJUE SHERIA YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR NO 11 YA MWAKA 1984

IJUWE SHERIA YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR NO. 11 YA MWAKA 1984.
5. Tume itakuwa na majukumu ya;
a) Usimamizi mzima wa mienendo ya jumla katika uchaguzi wa Rais, Wajumbe wa baraza la Wawakilishi, na viongozi wa serikali za mitaa kwa Zanzibar.
b) Kukuza na kuratibu elimu kwa wapiga kura.
Katika kulitekeleza hili Tume ya uchaguzi ya Zanzibar imekuwa ikifanya kila jitihada kuhakikisha inawafikia wananchi (wapiga kura) kwa karibu ilikusudi ya kuwahamasisha na kuwapatia elimu sahihi juu ya utaratibu wa kupiga kura.
Tume imetekeleza shuhuli nyingi ambazo ni mujarab kwa kuwafikia na kuhamasisha wapiga kura katika uandikisha wa wapiga kura wapya,uendelezaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na hata kwenye uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika octoba 25 mwaka 2015.09.23
Miongoni mwa mikakati iliyotekezwa katika uandikishaji ambayo pia kwenye uchaguzi mkuu inaendelezwa ni kufanya semina na makongamano kwa makundi mbali mbali ya jamii mfano semina kwa watu wenye ulemavu wa aina zote, semina kwa asasi za kiraia, semina kwa makonda na wamiliki wa vyombo vya usafiri wa barabarani, wagombea, vyombo vya habari, makongamano ya vijana ambayo yalijumisha wasanii, wanafunzi wa elimu ya juu, watu wa masikani za mitaani (vijiwe) na jamii yote kwa jumla.
Katika kuitekeleza ibara hii ya 5(b) ya sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar No.11 ya mwaka 1984 Tume ya Uchaguzi imefanya mabonanza matano ya mpira wa miguu kwa mikoa yote ya Zanzibar kwa ajili ya kuhamasisha watu wajitokeza kujiandikisha.
Aidha tarehe 12/09/2015,Tume imefanya bonanza la mpira wa miguu viwanja vya malindi Unguja ambapo timu na kutoka mikoa mitatu zilishirki na tarehe 19/09/2015 bonanza kama hilo limefanyika uwanja wa Ole kipangani Kisiwani Pemba kwa ajili ya kuhamasisha Uchaguzi wa Amani Zanzibar.
Tume imeandaa miongozo,maelekezo na vitabu mbali mbali vya maadili kwa ajili ya wanasiasa, wapiga kura , vyombo vya habari na waangalizi wa Uchaguzi wa ndani na nje.
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inafanya yote hayo ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki kikamilifu katika kupata haki yake ya kidemokrasia kumchagua kiongozi anaemtaka na kuwa na uwazi katika Uchaguzi wa huru, haki na wenye Amani.
PIGA KURA KWA AMANI UPATE MAENDELEO NCHINI

Monday, September 21, 2015

SHAKA HAMDU SHAKA ASEMA MAALIM HAFAI KUWA RAISI

KAIMU KATIBU MKUU  WA UMOJA WA VIJANA  WA CHAMA CHA MAPINDUZI  (UVCCM) SHAKA HAMDU SHAKA AMEMTAJA MGOMBEA URAIS WA ZANZIBAR KUPITIA CUF MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KUWA HAFAI KUWA RAIS WA ZANZIBAR AMA KUPEWA MADARAKA YA NGAZI ZA JUU KWANI  AMEWAHI  KUSHIRIKI VITENDO VYA UFISADI NA UFUJAJI WA FEDHA ZA UMAA WAKATI AKIWA WAZIRI KIONGOZI WA  SSERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR. 

SHAKA AMETOA MADAI HAYO JUZI KATIKA UZINDUZI MKUTANO WA KAMPENI ZA CCM JIMBO LA MWANAKWEREKWE MJINI UNGUJA ZILIZOFANYIKA KWENYE VIWANJA VYA IJTMAI YA ZAMANI, AMESEMA MGOMBEA HUYO WA URAIS WA ZANZIBAR KUPITIA TIKETI YA CUF  NI  KING'ANG'ANIZI WA MADARAKA ASIYETOSHEKA KWA NAFASI YEYOTE NA KWAMBA KUTAMANI KWAKE URAIS HUENDA ANA AJENDA YA  SIRI DHIDI MAENDELEO YA ZANZIBAR NA MUSTAKABALI WAKE KISIASA , KIUCHUMI NA  KIUSALAMA.

AMESEMA MWANASIASA HUYO AKIWA WAZIRI KIONGOZI AKICHUKUA SHILINGI MILIONI 100 KWA AJILI YA KUJITIBU MARADHI YA MATONSISI NCHINI BRUNEI  HADI SASA HAJAONYESHA VILELELEZO , VIAMBATANSHO AU MCHANGANUO WA MATUMIZI YA FEDHA ZA UMMA, AMBAZO MPAKA SASA HAJAWAHI KUZITOLEA MAJIBU YA KURIDHISHA.

AIDHA SHAKA  AMEMTUHUMU KIONGOZI HUYO KWAMBA FEDHA ZA  SMZ ANAZOTUMIA KWA AJILI YA MATIBABU  YAKE NI SHILINGI MILIONI 80 KWA SAFARI MOJA HUKO INDIA WAKATI ALISEMA NA KUAHIDI AKIWA SERIKALINI ANGETIBIWA NCHINI KATIKA HOSPITALI YA MNAZI MMOJA, KAULI AMBAZO KWA SASA ZINAONYESHA WAZI KUWA NI KIONGOZI ASIYEFAA KUWAONGOZA WANANCHI.

KAIMU KATIBU MKUU HUYO AMESEMA  MWANASIASA HUYO ANAPOSEMA ANA UWEZO WA KULETA MABADILIKO YA KIUCHUMI NA KULETA  MAISHA BORA KWA WANANCHI  WOTE KWA SIKU MIA MOJA ANAJITAFUTIA UMARUFU WA KISIASA NA WALA HANA UBAVU WA KUTEKELEZA HAYO KAMA ANAVYODAI KWENYE MAJUKWAA YA KISIASA. 

SHAKA ALIMEMTUPIA LAWAMA MAALIM SEIF NA KUDAI MWAKA 1995 ALITAMKA KWAMBA AKISHINDA URAIS ATAUTAMBUA UFALME ULIOPINDULIWA ZBAR MWAKA 1964 NA KWAMBA ATAYAZAMISHA MAPINDUZI YA ZBR  KATILA MKONDO WA NUNGWI.

AMEFAFANUA KUWA KUTOKANA NA KAULI PAMOJA NA VITENDO VYA MAALIM SEIF HANA NIA NJEMA YA KUJENGA UMOJA NA KULETA MAELEWANO BALI ANAKUSUDIA KUSHIKA URAIS ILI KUWAGAWA WANANCHI WA ZBR KWA MAPANDE YA UNGUJA NA UPEMBA. 

AMEWATAKA WANANCHI KUAMKA , KUMTAZAMA  NA KUTOMPIGIA KURA ZA NDIYO MGOMBEA HUYO URAIS WA CUF NA KUMHESBU KAMA NI ADUI NAMBA MOJA  WA MISINGI YA UMOJA, UPENDO NA MSHIKAMANO WA KITAIFA ANAYEPIGANIA KUVIZA JUHUDI ZA VYAMA  VYA  ASP NA TANU.

AMEWATAKA WANANCHI WA MWANAKWEREKWE KUMCHAGUA MGOMBEA URAIS WA JAMHURI YA MUUNGAMO DK JOHN MAGUFULI KUPITIA CCM NA DK ALI MOHAMED SHEIN KWA URAIS WA ZANZIBAR , MGOMBEA UWAKILISHI ABDALLA BUNGENI ALI KOMBO NA AHMADA ABDUL WAKIL MGOMBEA UBUNGE NA MADIWANI TOKA CCM .