Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii ,Vijana, Wanawake na Watoto Nd. ALI KHAMIS JUMA amesema Serikali imejipanga kikamilifu ili kuhakikisha wananchi wa vijijini wanaekewa miundombinu ya kuhakikisha masoko , uongezaji thamani za bidhaa na huduma za kifedha vijijini zinaimarika nchini.
Kauli hiyo ameitoa huko katika ukumbi wa mikutano wa Eacrotanal , Kikwajuni mjini hapa wakati akifungua warsha ya siku mbili (2) ya wadau mbali mbali kutoka Unguja na Pemba wakiwemo maafisa Ushirika wa wilaya na mikoa , chama kikuu cha akiba na mikopo juu ya mradi wa kuongeza huduma za kifedha kwa wananchi wa vijijini (MIVARF).
Naibu Katibu Mkuu huyo amesema Ushiriki wa kila mwananchi wa vijijini utamuharakishia mlengwa kupata huduma za kifedha kupitia taasisi husika na kupata fursa za kukopa ili kuona malengo ya taifa ya kuondoa umasikini yanafikiwa.
Amesema Wizara yake imekamilisha sera ya uwepo wa vyama vya akiba na mikopo SACCOSS na vikoba ambapo kutatoa fusa za watu kuona umuhimu wa mitaji pamoja na kuona fursa ya kwenda kukopa kwa ajili ya kuimarisha uzalishaji mali.
Aidha amefahamisha kuwa kuwepo kwa mradi huo pia kutahakikisha na kuona kuwa fedha zinazokopeshwa zinarudishwa na kwamba kila mtu anasimamia majukumu yake katika utendaji ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Nae mkufunzi katika warsha hiyo ambae ni afisa uangulizi na tathmini wa mradi huo wa MIVARF unaosimamiwa na Wizara ya Kilimo na Maliasili kwa hapa Zanzibar Bw. KHATIB MOH’D KHATIB amesema mradi huo wa miaka saba (7) ambao unatekelezwa Tanzania nzima utagharimu jumla ya dola za Kimarekani miliono mia moja na sabiini (170) utaweza kuimarisha huduma za kifedha pia kupunguka kwa hofu ya kupata hasara kwa taasisi za kifedha pamoja na kuongezeka kwa idadi yake .
Nao washiriki wa warsha hiyo wakichangia mada wamesema wamefarajika sana kupata taarifa ya MIVARF na kueleza kuwa mradi huo utaleta ukombozi mkubwa kwa wananchi wengi kiuchumi na kufikia lengo la kuondoa umasikini nchini.
Warsha hiyo imeandaliwa na Idara ya vyama vya Ushirika kwa mashirikiano na Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar na kufadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB).
No comments:
Post a Comment