tangazo

tangazo

Saturday, December 12, 2015

Gambia ni Jamhuri ya Kiislamu

Rais Yahya Jammeh wa Gambia ameitangaza nchi hiyo ya Kiafrika kuwa Jamhuri ya Kiislamu.
Akitangaza hatua hiyo, Rais Jammeh amesema kuwa, kuanzia sasa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unatawala nchini humo ikiwa ni katika juhudi za kutoa utambulisho kwa thamani za kidini.
Rais Yahya Jammeh amesema kuwa, kwa kuwa raia waliowengi wa nchi hiyo ni Waislamu, Gambia haiwezi kuendelea kuvumilia turathi za kikoloni.
Rais wa Gambia amesisitiza kuwa, wafuasi wa dini nyingine nchini humo hawatabughudhiwa na wanaweza kuishi kulingana na mafundisho ya dini zao.
Rais Jammeh ambaye mwaka 2013 alitangaza kujitoa nchi hiyo katika Jumuiya ya Madola, Commonwealth na kuitaja kuwa ni ukoloni mamboleo, anataraji nchi za Kiarabu zitaisaidia nchi yake ili iweze kuziba pengo la misaada iliyokatwa na itakayokatwa ya madola ya Magharibi. Machi mwaka huu serikali ya Gambia ilibadilisha lugha yake rasmi ya Kiingereza na kuifanya kuwa Kiarabu.
Gambia ina wakazi milioni moja na laki nane huku asilimia 95 wakiwa ni Waislamu. Gambia ilikoloniwa na Uingereza hadi mwaka 1965 ilipopata uhuru.

Nchi hiyo inategemea zaidi kilimo na utalii kama sekta kuu na uti wa mgongo wa uchumi wake.

UZINDUZI WA MV MAPINDUZI II NI KIELELEZO YA DHAMIRA YETU YA KUIMARISHA USAFIRI WA MAJINI

 Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohd Shein akikata Utepe ikiwa ni ishara ya Uzinduzi Rasmi wa Meli Mpya ya Mv Mapinduzi II Bandarini Zanzibar.
 Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein akitoa hotuba ya Uzinduzi wa Meli Mpya ya Mv Mapinduzi II Bandarini Zanzibar.kulia kwake ni Naibu Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano Zanzibar Issa Haji (Gavu) na kushoto ni Waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Moh'd Shein akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Bandari kuhusiana na sehemu ya kupumzikia abiria watakao safiri kwa Meli ya Mv MAPINDUZI II katika uzinduzi wa meli hiyo uliofanyika Bandari ya Malindi Zanzibar.
 Baadhi ya Wafanyakazi wa huduma mbalimbali watakao kuwemo katika Meli ya Mv Mapinduzi II iliozinduliwa  na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohd Shein Bandarini Zanzibar.
 Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein katikati akiwa katika picha ya pamoja na waheshimiwa mbalimbali katika uzinduzi wa Meli ya Mv Mapinduzi II Bandarini Zanzibar.
 Captan Abubakar Mzee akiwa pamoja na makaptain wenzake watakaokuwemo katika Meli ya Mv Mapinduzi II iliozinduliwa  na Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein Bandarini Zanzibar.
 Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein akijibu maswali mbalimbali yalioulizwa na waandishi baada ya Uzinduzi wa Meli ya Mv Mapinduzi II Bandarini Zanzibar.
 Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein akipata maelezo ya kitaalamu kutoka kwa Captan Abubakar Mzee kuhusiana na Mitambo ya uendeshaji wa Meli itakavyofanya kazi ikiwa baharini katika Uzinduzi wa Meli hio Bandarini Malindi Zanzibar.


Baadhi ya wananchi mbalimbali waliohudhuria katika Uzinduzi wa Meli Mpya ya Mv Mapinduzi II Bandarini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Ali Mohamed Shein leo amezindua meli mpya ya kisasa MV Mapinduzi II na kueleza kuwa uzinduzi wa meli hiyo ni hatua muhimu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kuimarisha usafiri wa baharini nchini.

Dk. Shein alibanisha pia kuwa ujenzi wa meli ni sehemu za hatua za serikali za “kulifanyia mageuzi makubwa Shirika la Meli na Uwakala Zanzibar ili liweze kujiendesha kibiashara kama mashirika mengine ya serikali yaliyofanyiwa mageuzi.

Alifafanua kuwa mageuzi yaliyofanyika na yanayoendelea kuyafanyika katika mashirika ya  serikali kama Shirika la Biashara (ZSTC), Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) na Shirika la Bima kumeleta mafanikio makubwa kwa kuwa sasa mashirika hayo yamekuwa yakifanya shughuli zake kibiashara hivyo uongozi wa shirika la Meli “sasa una kazi ya kuhakikisha kuwa shirika hili linajiendesha wenyewe”.  

Katika hotuba yake kwa wananchi na wageni waliohudhuria hafla hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na usafiri wa baharini wa uhakika, Serikali imedhamiria kununua meli nyingine mbili.

“wakati leo tukizindua meli hii, nataka wananchi watambue kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba ina mpango wa kununua meli mpya ndogo inayolingana na MV Maendeleo na meli mpya ya mafuta” Dk. Shein  alieleza na kushangiliwa na umati wa wananchi wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi .

Alibainisha kuwa meli ya serikali ya MV Maendeleo iliyopo sasa itauzwa kwa kuwa ni ya zamani na kusisitiza kuwa kwa sasa serikali haitaruhusu tena meli iliyozidi umri wa miaka 15 kusajiliwa Zanzibar.

Dk. Shein aliwataka wananchi kuyapuuza maneno ya baadhi ya watu kuwa meli hiyo si mpya na kusisitiza kuwa meli hiyo ni mpya kabisa iliyotengenezwa na kusimamiwa na makampuni yanayotambulika kimataifa na kwamba imezingatia matakwa ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

“Meli hii imetengenezwa na Kampuni inayotambuka ulimwenguni na kamwe haiwezi kufanya udanganyifu huo na zaidi tumekuwa na timu makini iliyokuwa ikifuatulia ujenzi wa meli hiyo hatua kwa hatua hadi kukamilika kwake” Dk. Shein alifafanua.

Aliwataka wananchi kuhakikisha wanaitunza vyema meli hiyo kwa kuwa imegharimu fedha nyingi ambazo zimetokana na nguvu zao wenyewe hivyo ni wajibu wao kuzithamini nguvu zao kwa kuitumia meli hiyo na kuacha uharibifu wa aina ye yote ile.

“Ni meli ya kisasa kabisa yenye huduma zote muhimu na imewekewa vifaa maalum vya kuzuia kuyumba majini dhidi ya mawimbi makali na mitambo ya usalama kuangalia mienendo ya abiria wakiwa melini” Dk. Shein alisema.

Awali katika maelezo yake Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mwasiliano Dk. Juma Akil alieleza kuwa gharama za meli hiyo ni Dola za Kimarekani milioni 30.6 chini ya mkataba uliotiwa saini kati ya serikali na kampuni ya Daewoo International na wabia wake Kampuni ya Posco Plantec Co. Ltd zote za Korea Kusini.

Alitoa maelezo ya kiufundi Dk. Akil alisema meli hiyo ina urefu wa mita 90 na upana mita 17 na ina uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani 200 za mizigo ikiwemo magari 80 madogo au magari 50 makubwa.

Alibainisha kuwa meli hiyo ina uwezo wa kufanya safari za kutoka Zanzibar hadi Pemba kwa saa 4 wakati safari ya Zanzibar hadi Dar es salaam inachukua 3.

Meli hiyo alieleza ina madaraja 4; daraja la tatu linalochukua abiria 800, daraja la kwanza abiria 350 na watu maalum (VIP) abiria 50.

Dk. Akil aliongeza kuwa meli hiyo inatumia tekinolojia rafiki wa mazingira ambapo ina mitambo ya kusafisha mafuta mazito ya kulainisha injini yaliyochafuka na kuyatumia tena.  

Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa meli hiyo ni mfano mzuri wa utendaji kazi kwa ushirikiano (team work) kwa kuwa kazi ya usimamizi wake ilishirikisha wizara na taasisi mbalimbali za serikali nchini.

Katika maelezo yake mafupi kumkaribisha Mgeni rasmi, waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee ambae pia ndie aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ujenzi wa Meli hiyo aliwashukuru wajumbe wote wa kamati walioshiriki hadi kufikia hatua ya kukabidhiwa meli hiyo.

“Kamati tulishirikiana wote kwa pamoja wakiwemo Mawaziri wa Mindombinu na Mawasiliano pamoja na Ofisi ya Mwanasheria chini ya Mwanasheria Mkuu wa zamani na wa sasa” alieleza na kubainisha kuwa wajumbe wa kamati hiyo hakuwahi kulipwa posho.

Waziri huyo alibainisha kuwa baadae mchana kutakuwa na hafla ya kusaini mkataba wa makabidhiano ya meli hiyo ambapo kampuni ya Daewoo itaikabidhi rasmi meli hiyo Serikali ya Mpinduzi ya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti  wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed Shein ameipongeza kamati ya usimamizi  iliyoshuhulikia utengenezaji wa Meli Mpya Mapinduzi II kwa kuweza kukamilika kwake.

Pongezi hizo alizitoa leo huko Bandarini wakati wa uzinduzi wa Meli hiyo ya kisasa ya ambayo imetengenezwa na Kampuni ya Daewoo International  kutoka  Korea ya Kusini.

Alisema kuwa Meli hiyo ni mpya na yenye mitambo ya kisasa yenye uwezo mkubwa  ambayo haiyumbishwi, kwani inavyombo maalumu vya kurekebisha mwenendo wa mawimbi mkondoni.

“Wananchi Msisikilize maneno ya mitaani kuwa Meli imeshatumika suala hilo halina ukweli, nawataka muje kuitembelea meli hiyo ili  kuweza kujionea wenyewe”. Amesema Dkt Shein.

Aidha alisema kuwa utaratibu wote wa utengenezaji tokea hatua ya awali hadi kumalizika kwake umeonyesha na Kampuni ya Daewoo ya Korea haiwezi kudanganya na kuihadaa Dunia na imeweza kugharimu Dola million 30.4 za kimarekani na ujenzi ulianza mnamo July 2013 hadi Disemba 2015 kuwasili Zanzibar.

Rais wa Zanzibar alisema kuwa kazi iliokuwepo  hivi sasa ni wananchi kuweza kuitunza  na kuihifadhi  meli hiyo ibakie kuwa na haiba na uzuri wake.

Aidha alisema kuwa Meli ya Mapinduzi II ni mpya na yakisasa  yenye uwezo mkubwa wa kusafirisha abiria 1200  na mizigo tani 200.

Alifahamisha kuwa kukamilika kwa meli hii mabadiliko makubwa yameweza kufanyika katika shirika la meli na uwakala tiketi zinauzwa kwa njia za kutumia komputa abiria hawezi kuuziwa tiket mpaka awe na kitambulisho cha Mzanzibar ,Mtanzania au kwa mgeni awe shahada ya kusafiria.

Pia alieleza kuwa Serikali inategemea kuweka Bandari kubwa ya mizigo eneo la Maruhubi mpiga duri na tayari imeshaanza makubaliani na Serikali ya China kuanzia mwezi wa Januari au Febuari wanatarajiwa kuanza  kazi ya ujenzi.


Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Utengenezaji wa Meli ambae pia ni Waziri wa Fedha Omar Yusuf Mzee amesema ameridhika na umalizaji wa meli hiyo na kutoa shukrani kwa wale wote waliokuwa sambamba katika kukamilisha kazi hiyo.

Friday, December 11, 2015

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR AFUTA MIKATABA YOTE YA UKODISHWAJI WA MAJENGO YA MICHENZANI.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo na Uongozi wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar mara baada ya kufuatilia Mikataba ya Wafanyabiashara waliokodishwa  milango ya Maduka katika Jumba la Maendeleo Nambari Kumi  Michenzani Mjini Zanzibar.

Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Ardhi Mh. Ramadhan Abdulla Shaaban na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Nd. Ali Khalil Mirza na kulia ya Balozi Seif ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Zanzibar { ZHC } Nd. Moh’d Hafidh Rajab.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Kamati ya Kitaifa ya Sherehe za Maulidi ya Kuzaliwa kwa Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Duniani Mtume Muhammad { SAW } aliyokutana nayo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Sheikh Sherali Shamsi akifuatiwa na Mjumbe wa Kamati Hiyo Bwana 
Moh’d  Baloo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  ameagiza  kufuta mikataba yote ya makubaliano ya  ukodishwaji wa Nyumba za Serikali zilizojengwa maalum kwa kuwasaidia Wananchi wa kipato cha Chini  unayofanywa kijanja  na  baadhi ya watu  pamoja na Kampuni binafsi kwa kukodisha watu wengine.
Alisema tabia hiyo iliyojengeka kwa muda mrefu sasa imekuwa ikitumiwa na wajanja hao wanaokodishwa Nyumba  na Serikali na baadaye kubuni mikataba mipya ya kuwakodisha watu wengine kwa nia ya kupata  faida kubwa zaidi            { Maarufu kilemba }.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa Kauli hiyo wakati alipofanya ziara fupi ya kufuatilia Mikataba ya Wafanyabiashara waliokodishwa  milango ya Maduka katika Jumba la Maendeleo Nambari Kumi  Michenzani Mjini Zanzibar ambayo baadhi ya waliokodishwa milango hiyo na Serikali tayari  wameshaikodisha  kwa  watu wengine.
Alisema tabia ya baadhi ya Watu hao kutumia mali za Serikali walizopewa kwa misingi ya kupata tahfifu ya kupunguza ukali wa maisha  na kuwauzia au kuwakodisha watu wengine waelewe kwamba wanafanya dhulma na dhambi kubwa.
Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Shirika la Nyumba Zanzibar { ZHC } kwa uamuzi iliyochukuwa ya kuwafutia mikataba wajeta wake wa mwanzo  iliyowapa milango la Maduka na wakaamua kuikodisha tena kwa watu wengine.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alionya  kwamba tabia kama hiyo imejengeka pia katika Nyumba zilizowekwa Wakfu na kuishauri Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar kufanya utafiti na kuwabaini wapangaji wake wenye tabia kama hiyo.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Zanzibar Nd. Moh’d  Hafidh Rajab alisema  Watendaji wa Shirika hilo wameanza ukaguzi Maalum wa kuzipitia Nyumba zote za Serikali zilizokodishwa kwa watu na Taasisi tofauti hapa Nchini.
Nd. Hafid alisema ukaguzi huo utatoa fursa kwa Uongozi wa Shirika  hilo kufanya marekebisho ya kodi zilizofungwa katika mikataba ya zamani ili iende na wakati na soko liliopo hivi sasa.
Alisema Shirika la Nyumba la Zanzibar lililoasisiwa hivi karibuni baada ya kupata baraka za Baraza la Wawakilishi Zanzibar linahitajika lijitegemee lenyewe badala ya kusubiri ruzuku inayotolewa na Serikali Kuu.
Akitoa shukrani zake Mmoja wa wamiliki wa Maduka yaliyopo  Michenzani ambae ni Meneja wa Kampuni ya A l – Salam na Seib Ruila Bwana Yussuf Juma Msanif  aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Shirika lake la Nyumba kwa uamuzi wake wa kukagua majengo yake mbali mbali.
Bwana Yussuf alisema uamuzi huo wa busara na hekima umewapa faraja wao binafsi na Kuliomba Shirika la Nyumba kufikiria upya kodi zake  inazotoza kwa lengo la kuwapa tahfifu Wafanyabiashara wachanga ili waweze kuwa na uwezo mzuri wa kulipa kodi.
Mlango mmoja wa Duka hapo Michenzani ulikuwa ukikodishwa Mteja kutoka Serikalini kwa Shilingi Thamanini Elfu kwa Mwaka wakati mkodishwa huyo anaamuwa kukodisha tena kwa Mtu wa Pili wa Dola za Kimarekani  mia 450  kwa mwaka sawa na Shilingi Laki Tisa na Thamanini { 980,000 }  za Kitanzania.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Kamati ya  Taifa ya Sherehe za Maulidi ya kuzaliwa Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad  { SAW }.
Kamati hiyo aliyokutana nayo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar pamoja na mambo mengine  Mwenyekiti wake Sheikh Sherali Shamsi alimuelezea matayarisho yanayoendelea ya Maulidi hayo yanayofanyika Kitaifa kila mwaka hapa Nchini.
Sheikh Sheral alisema kikawaida Maulidi hayo yanayoadhimishwa  Usiku wa Mwezi Kumi na Moja Mfunguo Sita hufanyika katika Viwanja maarufu vya Maisara alakini endapo itanyesha Mvua shughuli hiyo itahamia katika Ukumbi wa salama Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.


Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

TAARIFA  KWA VYOMBO VYA  HABARI  JUU YA UTEUZI WA BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI KWA SERIKALI YA JAMUHURI YA MUNGANO WA TANZANIA.


KIDUMU  CHAMA CHA MAPINDUZI.
TAARIFA  KWA VYOMBO VYA  HABARI  JUU YA UTEUZI WA BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI KWA SERIKALI YA JAMUHURI YA MUNGANO WA TANZANIA.
   Awali ya yote shirikisho la  vyuo vya elimu ya juu  CCM –    
   Zanzibar  linapenda kuchukua fursa hii , kumshukuru    
   M/Mungu  kwa kutujaalia nchi yetu  kuwa katika   hali ya  
   amani  na  utulivu.
Pili, tunachukua fursa hii  kuwashukuru nyinyi  vyombo vya  habari  kwa mahudhurio yenu  mazuri kuja  kuchukua taarifa kwa  lengo  la kuwahabarisha umma  juu ya mustakbal wa nchi yetu.
Shirikisho la vyuo vya elimu ya juu CCM  -  Zanzibar  Linampongeza Rais wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na wasaidizi wake Makamu wa Rais na Waziri mkuu kwa kulitangaza Baraza jipya la mawaziri.
Aidha, sisi shirikisho la vyuo vya Elimu ya juu CCM Zanzibar tunampongeza sana Mhe. Rais Magufuli kwa kufanya uteuzi wa baraza jipya la mawaziri kwani watu walioteuliwa wana uwezo wa kutosha katika kuisaidia jamii ya watanzania.
Pamoja na kuunga mkono wa uteuzi wa baraza hilo, pia tunampongeza kwa kasi alioaanza nayo ya kubana matumizi katika kuendesha serikali, kitendo hicho kinaashiria moyo wa dhati aliokuwa nao katika kuleta maendeleo ya Tanzania na watanzania kwa ujumla.
Ndugu waandishi wa habari tunaomba ifahamike kuwa Mhe. Rais anatekeleza ilani ya CCM 2015/2020 ambayo imetoa vipaumbele katika maeneo manne makuu

i.                  Kupunguza umaskini wa watanzania
ii.               Kutatua changamoto ya ajira kwa vijana.
iii.            Kupambana na rushwa na ufisadi na
iv.             Kudumisha amani ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
Ndugu wandishi wa habari, kutokana na baraza la mawaziri na watu walioteuliwa tunaamini ya kwamba ilani yetu ya CCM itatekelezwa kwa asilimia kubwa na itarejesha heshima kwa chama chetu.
Tunawaomba kwa dhati mawaziri walioteuliwa watekeleze majukumu yao kwa nguvu zao zote katika kumsaidia DK. Magufuli kusukuma gurudumu la maendeleo la taifa letu.
Ifahamike kuwa, Mhe. Rais amefanya mambo makubwa wakati hajateuwa baraza la mawaziri, hivyo kupitia taarifa hii tunawaomba wateule hao kuengeza kazi kwa kuchapa kazi ili wamsaidie Mhe. Rais kuyatumbua majipu bila ya woga.
Sambamba na hayo, shirikisho la Vyuo vya Elimu ya juu CCM Zanzibar tunampongeza sana Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Makam wa pili wa Rais wa Serekali ya M apinduzi ya Zanzibar, pia mjumbe wa kamat ya ccmi kwa utendaji wake mzuri kwa kuwataka mamlaka ya maji Zanzibar (ZAWA) kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua watendaji waliotumia dhamana zao vibaya katika kusimamia huduma  za maji.
Lakini pia tunampongeza Mhe. Makamu wa pili kwa kusitisha mara moja Bw. Anuar Abdulla kufanya ujenzi wa nyumba ya ghorofa katika maeneo ya makaazi ya watu hapo mlandege kwani eneo hili linatumika kwa ajili ya shughuli za kijamii.
Mwisho, shirikisho la vyuo vya Elimu ya juu Zanzibar linawaomba viongozi wa juu wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar  pamoja na watendaji wote kuiga mfano wa Mhe. Magufuli katika kufanya kazi kwa maslahi mapana ya umma pamoja na kudhibiti matumizi mabaya ya serekali pia kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato sambamba na kuwatumikia wananchi wa Zanzibar. Kwani hii imejidhihirisha wazi wazi katika ahadi za mwana ccm ambayo inasema ˵Cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwengine kwa faida yanguˮ
Ahsanteni  kwa kunisikiliza.


‘’ Mungu   ibariki  Zanzibar’’
‘’Mungu ibariki Tanzania ‘’
‘’Mungu ibariki Afrika”
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Imetiwa Saini na Katibu,


………………………………………..

UHURU WA TANGANYIKA KUFIKIA MIAKA 54

CHAMA CHA ADA – TADEA
UHURU WA TANGANYIKA KUFIKIA MIAKA 54

Ni fahari ya watanganyika kusherehekea uhuru wao kwa kujua wapi wanapotoka na wapi wanapokwenda kwa mujibu wa sheria.

Kama tunavojua Tanganyika ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni tarehe 9 December 1961 na wakapata kiti cha umoja wa Mataifa tarehe 14 December 1961 namba ya kiti chao (GA Resolution 1667(XVI) na ikawa nchi huru. Lakini ilipofika tarehe 26 April 1964 iliungana na Zanzibar na kua Tanzania ambayo ipo mpaka sasa lakini tukirudi nyuma maendeleo makubwa ya miji na watu sambamba na maendeleo ya miundombinu na mawasiliano ya kitaifa na kimataifa mawasiliano ya jamii na ya mtu kwa mtu. Lakini kama hiyo haitoshi uhuru huu umeleta heshima kwa taifa na jamii na umeondondosha  dharau na kuimarisha upendo kwa kuondoa ubaguzi wa rangi ukabila na udini na kuijengea sifa Tanganyika na watanganyika wenyewe . Lakini uhuru huo wa Tanganyika kuna changamoto nyingi za maendeleo kwa mfano; 1962 Tanganyika ilikua ninchi ya pili duniani inayozalisha mbao. nchi ya kwanza ilikua ni Crprus. Lakini kwa sasa Tanganyika kama Tanzania tunashuhudia watoto wa shule wanakaa chini lakini kama nchi ilokua inatoa mbao nyingi na kama hiyo haitoshi Tanganyika kwa sasa wanahifadhi za kitaifa18 sambamba  na mbuga za wanyama, tukilinganisha na  nchi za jirani Kenya waliopata uhuru wao tarehe 10/December 1963 ilojulikana kama (madaraka day) ambao wanasherehekea kesho lakini Kenya wao wanahifadhi 8 za kitaifa lakini Kenya ni ndogo sasa kwa Tanzania hawana ardhi kubwa hata katika hecta za miraba Tanganyika bado kubwa. Tanganyika wana watu wasiopungua milioni 40,000,000 kenya wao wana watu wasiopungua milioni 18,000,000 lakini wakenya wapo juu kiuchumi unaoendana na elimu sahihi na kwa hilo kwa ushindi mwengine pesa ya Kenya ilikuwa sawa sawa mia kwa mia kubadilishana lakini kwa sasa pesa ya Kenya ipojuu mia Kenya kwa 12 ya Tanzania. Na hii inatokana na kushuka kiuchumi na ukizingatia Tanganyika ina rasilimali nyingi kulikokenya kama vile gasi, uranium, chuma ambayo madini hayo yanatosha kwa kuinua uchumi wa taifa. Lakini siri kubwa ya maendeleo ya wakenya inatokana na kutumia vyema rasilimali zao sambamba na kutumia rasilimali watu kwa kutumia vipaji na elimu ya wakenya kwa kuinua maendeleo na ustawi wa jamii kwa mujibu wa sheria ya Kenya. Na kwa Tanganyika wanatakiwa walione hilo. Na wapunguze uzembe  ubadilifu na rushwa ili kuleta maendeleo ya kweli sambamba kutumia rasilimali zao na rasilimali watu kwa kudumisha umoja na kutooneana muhali kwa wale wanaohujumu mali za serikali. Lakini hata hivyo sera ya kilimo kwanza itawakomboa watanganyika kama tunavyojua asilimia 75 watanzania ni wakulima na wafugaji lakini hata hao wafanyakazi nao ni wakulima na wafugaji ipo haja kwa sasa serikali kuimarisha pembejeo za kilimo na kuwa kilimo cha kisasa ambacho hutumia mbolea. Tatizo la wakulima ni masoko ya kununulia bidhaa sambamba na viwanda vya kilimo kwa sasa kunahitajika viwanda vya matunda kama vile lushoto kunatakiwa kiwanda kikubwa cha kusindika matunda ili kuokoa matunda yasiharibike ovyo lakini kwa kuacha wakulima wa pamba na wa korosho kutowalipa na kuwacheleweshaea kuwalipa  pesa zao. Kunapunguza jitihada za wakulima na kupelekea kudumaza sera ya kilimo kwanza. Lakini kufika miaka 54 ya uhuru wa Tanganyika uhuru huo ni faraja na heri kwa watanganyika ili kuondosha tatizo la afya, elimu na ajira. Na hili ni tatizo kubwa kwa maendeleo ya watanganyika na hata watanzania kwa ujumla ikiwepo Zanzibar. Bado wananchi wanataka afya bora elimu juu na ajira zaidi.
Na kwa upande wa afya kuna haja ya kuboresha vituo vya afya katika kata na vitongoji ili wananchi ziwafilie huduma hizo tena huduma ziwe bora na kuhusu suala la elimu bado watanganyika wanahitaji elimu bora inayoendana na wakti kwa kuwa na mitaala bora, shule za mabweni zenye maabara kwa mfumo huo wa elimu mzuri unaofuata vigezo vya mataifa ili kupata elimu bora itakayokwenda sambamba na katika shule za kata tarafa na vijiji. Kwa sababu taifa lolote linakua bora kwa elimu. Na kwa upande wa ajira kufufua viwanda vilivyokufa na kuongeza vingine ili kuweza kupata ajira kama tunavyojua ajira sahihi ya nguvu kazi kama tunavyojua ajira sahihi ulimwenguni ni ile ya viwanda ambayo hutoa ajira ambao wamesoma na ambao hawajasoma ( ajira ya nguvu kazi).
Kwasasa watanganyika au watanzania ni fahari yao kwa kuwa na kiongozi ambae John Joseph Pombe Magufuli ambae ana sera ya hapa ni kazi tu na ndiomana siku ya Uhuru wa Tanganyika amesema tusherehekee kwa kuokoa fedha na kupeleka katika maendeleo ya jamii kama vile barabara. Hata hivyo sera zake kama vile kuendeleza viwanda, mifugo wakulima,uvuvi na hata kusema atakuwa na sera ya viwanda ambayo itatokana na kilimo, mifugo, uvuvi na kuondosha tatizo la ajira kwa asilimia 40% ifikapo 2020 na kuona tatizo la ajira linaondoka kwa kias. Lakini itapofika 2016 ilimu itakua bure yaani bila malipo, hii yote ni faraja na maendeleo makubwa kwa Tanganyika na Tanzania kwa ujumla lakini uokozi wa fedha za serikali zilizokua zishapotea umakini wa viongozi hawa unaweza kuleta maendeleo kwa sasa Mh Rais Magufuli, Waziri mkuu Majaaliwa Kassim na Mama Jasiri Samia Suluhu ni wachapakazi na wafatilia wasimamizi wa shughuli za jamii kwa kuona kazi zinafanyika kua hapa kazi tu . Watu wataweza kuona tunainuka kiuchumi kwa muda mfupi tu kwa kufikia uchumi wa kati na kupunguza umasikini na kuona jirani zetu Kenya tunawapita kwa maendeleo kwa kutumia rasilimali watu kiuhakika sambamba na rasilimali zetu zilizomo nchini kama mafuta, gesi, urenim, chuma na madini mbalimbali yalozuka nchini na yalokuwemo sambamba na kutumia hifadhi za kimataifa kwa kukuza utalii wa ndani na nje kwa kuzifanyia kazi vizuri nilizozitaja nchini ya awamu mpya ya uongozi wa Mh John Pombe Magufuli tutatimiza malengo makuu ya kiuchumi na ulimwengu utaona hilo

Ahsante

ITAWEZEKANA SANA TUKIONDOSHA UZEMBE, UFISADI, RUSHWA MUHALI NA TUKIFUATA KAULI MBIU YA WAASISI WETU WALIPOSEMA UHURU NA KAZI.

Wako Mwanasiasa Mkongwe (Mwanaharakati)
Katibu mwenezi
 Taifa ADA – TADEA

………………………..
RASHID YUSSUF MCHENGA
0715560243

0773560243

Zanzibar itaendelea kutunza na kulinda Utamaduni wa Zanzibar na kuyafanyia matengenezo  majengo ya Mji  Mkongwe

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni,Utalii na Michezo Issa Mlingoti akifungua Mkutano wa Mfuko wa usimamizi wa Magofu Duniani kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ali Mwinyikai. Mkutano huo ulijadili mambo mbalimbali juu ya uhifadhi wa mambo ya kale pamoja na kutembelea na kuzungumzia namna ya kuyafanyia matengenezo majumba  yaliyo chakaa ili yasitoweke katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
 Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho na mambo ya kale Zanzibar Dkt. Amina Issa akionesha Picha ya Uchakavu wa Jengo wakati alipokuwa akitoa Mada katika Mkutano wa wadau wa kutembelea na kuzungumzia namna ya kuyafanyia matengenezo majumba  mabovu ili yasitoweke katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.
 Stephen Battle kutoka Mfuko wa Kimataifa wa kuyaendeleza majengo  ya  Miji Mikongwe Duniani na kuyatunza {World Monument Fund} akitoa mada katika Mkutano wa Mkutano wa kutembelea na kuzungumzia namna ya kuyafanyia matengenezo majumba  mabovu ili yasitoweke katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.
 Mkutano wa kutembelea na kuzungumzia namna ya kuyafanyia matengenezo majumba  mabovu ili yasitoweke katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Na Ali Issa Maelezo- Zanzibar

Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutunza na kulinda Utamaduni wa Zanzibar na kuyafanyia matengenezo  majengo ya Mji  Mkongwe yaliyochoka kwa ushirikiano wa Mfuko wa Kimataifa wa kuyaendeleza majengo  ya  Miji Mikongwe Duniani na kuyatunza {World Monument Fund}.

Hayo yamesemwa  na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni,Utali na Michezo Issa Mlingoti wakati akifungua mkutano kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo  wa kutembelea na kuzungumzia namna ya kuyafanyia matengenezo majumba  mabovu ili yasitoweke katika Mji huo.

Amese matengenezo hayo  hufanywa kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Serikali, wahisani na Mashirika mbalimbali  ya Kimataifa.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya  Mji Mkongwe Zanzibar  Issa Makarani amesema  hivi sasa kuna majengo yapo hatarini kupotea katika urithi wa Kimataifa  kutokana na kuchakaa na  kufikia hatua ya  kuanguka hivyo kutokea mfuko huo kusaidia ni jambo la faraja.

Aidha alisema  wananchi  kwa upande wao wanalazimika kufuata kanuni na taratibu za  kuuhifadhi na kuulinda Mji Mkongwe wa Zanzibar ikiwamo kuacha kupitisha magari makubwa ambayo hupelekea kupasuka kwa majengo.

“Kuazia mwakani kutakua na sheria maalumu ya kupitisha vyombo vya moto katika maeneo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar ambayo madereva watalazimika kuifuata,” alisema Makarani.

Nae Meneja wa  Mfuko wa Kimataifa wa kuyaendeleza majengo  ya  Miji Mikongwe Duniani na kuyatunza kwa nchi za  Jangwa la Sahara Stephen Battle  amesema taasisi hiyo imekuwa ikifanya matengenezo majengo ya miji yenye urithi wa Kimataifa ikiwemo Kanisa la Mkunazini liliopo Mji mkongwe wa Zanzibar.

Mkutano  mkuu wa mwaka wa Kamisheni ya Wachezaji Tanzania .

 Mwenyekiti wa Kamisheni ya wachezaji Tanzania (KAWATA) Ramadhan Zimbwe akizungumza na Wanamichezo  mbalimbali waliohudhuria katika Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika katika Ukumbi wa kituo cha Utengamano Welezo Mjini Zanzibar.
 Katibu Mkuu wa TOC Filbert Bayi akizungumza na wana Michezo  mbalimbali waliohudhuria katika Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika katika Ukumbi wa kituo cha Utengamano Welezo Mjini Zanzibar.
 Washiriki wa Mkutano Mkuu wa Mwaka waliohudhuria katika Mkutano huo wakisikiliza maelezo  kwa Mgeni Rasmi Katibu Mkuu msaidizi Jamali Nassor Adi hayupo pichani.
 geni Rasmi Jamal Nassor Adi akizungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa kamisheni ya Wachezaji Tanzania (KAWATA) katika Ukumbi wa Kituo cha Utengamano Welezo Mjini Zanzibar.
Wajumbe wakiwa katika picha ya Pamoja.

Na Rahma Khamis /Miza Othman -Maelezo Zanzibar.

Kamati ya Olimpiki Tanzania  (TOC)  wamewataka Viongozi  wa Mashirika ya  Vyama  vya Michezo  Tanzania  kusaidiana na wanamichezo mbalimbali ili kufikia hadhi ya kimataifa .
Hayo yameelezwa na na Katibu mtendaji wa TOC Jamal  Nassor Adi  huko Kituo cha Utengamano Welezo  Zanzibar  wakati alipokua akifungua  Mkutano  mkuu wa mwaka wa Kamisheni ya Wachezaji Tanzania .
Amesema lengo kuu la mkutano huo ni kuhamasisha na kuamsha ari kwa Wachezaji ili kuweza kurejesha hadhi ya Michezo  Tanzania.
 Katibu Jamal amefahamisha kuwa wachezaji  ndio wahusika wakuu  wa michezo hivyo ni lazima kushirikishwa na kupatiwa elimu ili kuweza kufahamu  wajibu wao katika michezo   na kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.
Akizungumzia suala la dawa za kuongeza nguvu kwa wanamichezo,  Katibu Jamal amesema  ni vyema wachezaji kuzifahamu na kujiepusha nazo kwani kitendo hicho kinaweza kupelekea nchi kupigwa marufuku kushiriki michezo ya Kimataifa.
Nae Katibu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania Filbert Bayi  amesema kuwa michezo ni chanzo cha kujipatia  ajira  kwa vijana  hivyo ni vyema michezo  iendelezwe ili kuleta maendeleo kwa wachezaji wenyewe  na Taifa kwa ujumla.
Aidha  amesema katika kuimarisha michezo Nchini   suala la   kuteuliwa wawakilishi  wenye uwezo   ni jambo muhimu  na amewashauri washiriki wa mkutano  huo kusaidia ili kupunguza malalamiko.
Mwenyekiti wa  Kamsheni ya  Wachezaji Tanzania (KAWATA)   Ramadhani Zimbwe ameahidi kupambana na rushwa kwa viongozi na watendaji  wa michezo nchini kwani  vitendo hivyo vinarudisha nyuma  ufanisi wa michezo.
Amesema rushwa ni adui wa haki na mara nyingi hupelekea mtu mwenye uwezo wa kifedha kupata haki asiyostahiki na kumuacha mwenye haki hiyo kuikosa kutokana na kukosa fedha.