Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Ardhi Mh. Ramadhan
Abdulla Shaaban na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Nd. Ali Khalil Mirza na kulia ya
Balozi Seif ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Zanzibar { ZHC } Nd.
Moh’d Hafidh Rajab.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
akizungumza na Kamati ya Kitaifa ya Sherehe za Maulidi ya Kuzaliwa kwa Kiongozi
wa Dini ya Kiislamu Duniani Mtume Muhammad { SAW } aliyokutana nayo Ofisini
kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Sheikh
Sherali Shamsi akifuatiwa na Mjumbe wa Kamati Hiyo Bwana
Moh’d Baloo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi ameagiza kufuta mikataba yote ya makubaliano ya
ukodishwaji wa Nyumba za Serikali zilizojengwa maalum kwa kuwasaidia
Wananchi wa kipato cha Chini unayofanywa kijanja na baadhi ya
watu pamoja na Kampuni binafsi kwa kukodisha watu wengine.
Alisema tabia hiyo iliyojengeka kwa muda mrefu sasa imekuwa
ikitumiwa na wajanja hao wanaokodishwa Nyumba na Serikali na baadaye
kubuni mikataba mipya ya kuwakodisha watu wengine kwa nia ya kupata faida
kubwa zaidi {
Maarufu kilemba }.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa Kauli hiyo wakati alipofanya
ziara fupi ya kufuatilia Mikataba ya Wafanyabiashara waliokodishwa
milango ya Maduka katika Jumba la Maendeleo Nambari Kumi Michenzani Mjini
Zanzibar ambayo baadhi ya waliokodishwa milango hiyo na Serikali tayari
wameshaikodisha kwa watu wengine.
Alisema tabia ya baadhi ya Watu hao kutumia mali za Serikali
walizopewa kwa misingi ya kupata tahfifu ya kupunguza ukali wa maisha na
kuwauzia au kuwakodisha watu wengine waelewe kwamba wanafanya dhulma na dhambi
kubwa.
Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Shirika la Nyumba
Zanzibar { ZHC } kwa uamuzi iliyochukuwa ya kuwafutia mikataba wajeta wake wa
mwanzo iliyowapa milango la Maduka na wakaamua kuikodisha tena kwa watu
wengine.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alionya kwamba
tabia kama hiyo imejengeka pia katika Nyumba zilizowekwa Wakfu na kuishauri
Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar kufanya utafiti na kuwabaini
wapangaji wake wenye tabia kama hiyo.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Zanzibar Nd.
Moh’d Hafidh Rajab alisema Watendaji wa Shirika hilo wameanza
ukaguzi Maalum wa kuzipitia Nyumba zote za Serikali zilizokodishwa kwa watu na
Taasisi tofauti hapa Nchini.
Nd. Hafid alisema ukaguzi huo utatoa fursa kwa Uongozi wa
Shirika hilo kufanya marekebisho ya kodi zilizofungwa katika mikataba ya
zamani ili iende na wakati na soko liliopo hivi sasa.
Alisema Shirika la Nyumba la Zanzibar lililoasisiwa hivi
karibuni baada ya kupata baraka za Baraza la Wawakilishi Zanzibar linahitajika
lijitegemee lenyewe badala ya kusubiri ruzuku inayotolewa na Serikali Kuu.
Akitoa shukrani zake Mmoja wa wamiliki wa Maduka yaliyopo
Michenzani ambae ni Meneja wa Kampuni ya A l – Salam na Seib Ruila Bwana
Yussuf Juma Msanif aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia
Shirika lake la Nyumba kwa uamuzi wake wa kukagua majengo yake mbali mbali.
Bwana Yussuf alisema uamuzi huo wa busara na hekima umewapa
faraja wao binafsi na Kuliomba Shirika la Nyumba kufikiria upya kodi zake
inazotoza kwa lengo la kuwapa tahfifu Wafanyabiashara wachanga ili waweze kuwa
na uwezo mzuri wa kulipa kodi.
Mlango mmoja wa Duka hapo Michenzani ulikuwa ukikodishwa
Mteja kutoka Serikalini kwa Shilingi Thamanini Elfu kwa Mwaka wakati mkodishwa
huyo anaamuwa kukodisha tena kwa Mtu wa Pili wa Dola za Kimarekani mia
450 kwa mwaka sawa na Shilingi Laki Tisa na Thamanini { 980,000 }
za Kitanzania.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi alikutana na Kamati ya Taifa ya Sherehe za Maulidi ya
kuzaliwa Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad { SAW }.
Kamati hiyo aliyokutana nayo Ofisini kwake Vuga Mjini
Zanzibar pamoja na mambo mengine Mwenyekiti wake Sheikh Sherali Shamsi
alimuelezea matayarisho yanayoendelea ya Maulidi hayo yanayofanyika Kitaifa
kila mwaka hapa Nchini.
Sheikh Sheral alisema kikawaida Maulidi hayo
yanayoadhimishwa Usiku wa Mwezi Kumi na Moja Mfunguo Sita hufanyika
katika Viwanja maarufu vya Maisara alakini endapo itanyesha Mvua shughuli hiyo
itahamia katika Ukumbi wa salama Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment