tangazo

tangazo

Saturday, December 12, 2015

UZINDUZI WA MV MAPINDUZI II NI KIELELEZO YA DHAMIRA YETU YA KUIMARISHA USAFIRI WA MAJINI

 Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohd Shein akikata Utepe ikiwa ni ishara ya Uzinduzi Rasmi wa Meli Mpya ya Mv Mapinduzi II Bandarini Zanzibar.
 Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein akitoa hotuba ya Uzinduzi wa Meli Mpya ya Mv Mapinduzi II Bandarini Zanzibar.kulia kwake ni Naibu Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano Zanzibar Issa Haji (Gavu) na kushoto ni Waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Moh'd Shein akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Bandari kuhusiana na sehemu ya kupumzikia abiria watakao safiri kwa Meli ya Mv MAPINDUZI II katika uzinduzi wa meli hiyo uliofanyika Bandari ya Malindi Zanzibar.
 Baadhi ya Wafanyakazi wa huduma mbalimbali watakao kuwemo katika Meli ya Mv Mapinduzi II iliozinduliwa  na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohd Shein Bandarini Zanzibar.
 Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein katikati akiwa katika picha ya pamoja na waheshimiwa mbalimbali katika uzinduzi wa Meli ya Mv Mapinduzi II Bandarini Zanzibar.
 Captan Abubakar Mzee akiwa pamoja na makaptain wenzake watakaokuwemo katika Meli ya Mv Mapinduzi II iliozinduliwa  na Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein Bandarini Zanzibar.
 Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein akijibu maswali mbalimbali yalioulizwa na waandishi baada ya Uzinduzi wa Meli ya Mv Mapinduzi II Bandarini Zanzibar.
 Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein akipata maelezo ya kitaalamu kutoka kwa Captan Abubakar Mzee kuhusiana na Mitambo ya uendeshaji wa Meli itakavyofanya kazi ikiwa baharini katika Uzinduzi wa Meli hio Bandarini Malindi Zanzibar.


Baadhi ya wananchi mbalimbali waliohudhuria katika Uzinduzi wa Meli Mpya ya Mv Mapinduzi II Bandarini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Ali Mohamed Shein leo amezindua meli mpya ya kisasa MV Mapinduzi II na kueleza kuwa uzinduzi wa meli hiyo ni hatua muhimu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kuimarisha usafiri wa baharini nchini.

Dk. Shein alibanisha pia kuwa ujenzi wa meli ni sehemu za hatua za serikali za “kulifanyia mageuzi makubwa Shirika la Meli na Uwakala Zanzibar ili liweze kujiendesha kibiashara kama mashirika mengine ya serikali yaliyofanyiwa mageuzi.

Alifafanua kuwa mageuzi yaliyofanyika na yanayoendelea kuyafanyika katika mashirika ya  serikali kama Shirika la Biashara (ZSTC), Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) na Shirika la Bima kumeleta mafanikio makubwa kwa kuwa sasa mashirika hayo yamekuwa yakifanya shughuli zake kibiashara hivyo uongozi wa shirika la Meli “sasa una kazi ya kuhakikisha kuwa shirika hili linajiendesha wenyewe”.  

Katika hotuba yake kwa wananchi na wageni waliohudhuria hafla hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na usafiri wa baharini wa uhakika, Serikali imedhamiria kununua meli nyingine mbili.

“wakati leo tukizindua meli hii, nataka wananchi watambue kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba ina mpango wa kununua meli mpya ndogo inayolingana na MV Maendeleo na meli mpya ya mafuta” Dk. Shein  alieleza na kushangiliwa na umati wa wananchi wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi .

Alibainisha kuwa meli ya serikali ya MV Maendeleo iliyopo sasa itauzwa kwa kuwa ni ya zamani na kusisitiza kuwa kwa sasa serikali haitaruhusu tena meli iliyozidi umri wa miaka 15 kusajiliwa Zanzibar.

Dk. Shein aliwataka wananchi kuyapuuza maneno ya baadhi ya watu kuwa meli hiyo si mpya na kusisitiza kuwa meli hiyo ni mpya kabisa iliyotengenezwa na kusimamiwa na makampuni yanayotambulika kimataifa na kwamba imezingatia matakwa ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

“Meli hii imetengenezwa na Kampuni inayotambuka ulimwenguni na kamwe haiwezi kufanya udanganyifu huo na zaidi tumekuwa na timu makini iliyokuwa ikifuatulia ujenzi wa meli hiyo hatua kwa hatua hadi kukamilika kwake” Dk. Shein alifafanua.

Aliwataka wananchi kuhakikisha wanaitunza vyema meli hiyo kwa kuwa imegharimu fedha nyingi ambazo zimetokana na nguvu zao wenyewe hivyo ni wajibu wao kuzithamini nguvu zao kwa kuitumia meli hiyo na kuacha uharibifu wa aina ye yote ile.

“Ni meli ya kisasa kabisa yenye huduma zote muhimu na imewekewa vifaa maalum vya kuzuia kuyumba majini dhidi ya mawimbi makali na mitambo ya usalama kuangalia mienendo ya abiria wakiwa melini” Dk. Shein alisema.

Awali katika maelezo yake Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mwasiliano Dk. Juma Akil alieleza kuwa gharama za meli hiyo ni Dola za Kimarekani milioni 30.6 chini ya mkataba uliotiwa saini kati ya serikali na kampuni ya Daewoo International na wabia wake Kampuni ya Posco Plantec Co. Ltd zote za Korea Kusini.

Alitoa maelezo ya kiufundi Dk. Akil alisema meli hiyo ina urefu wa mita 90 na upana mita 17 na ina uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani 200 za mizigo ikiwemo magari 80 madogo au magari 50 makubwa.

Alibainisha kuwa meli hiyo ina uwezo wa kufanya safari za kutoka Zanzibar hadi Pemba kwa saa 4 wakati safari ya Zanzibar hadi Dar es salaam inachukua 3.

Meli hiyo alieleza ina madaraja 4; daraja la tatu linalochukua abiria 800, daraja la kwanza abiria 350 na watu maalum (VIP) abiria 50.

Dk. Akil aliongeza kuwa meli hiyo inatumia tekinolojia rafiki wa mazingira ambapo ina mitambo ya kusafisha mafuta mazito ya kulainisha injini yaliyochafuka na kuyatumia tena.  

Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa meli hiyo ni mfano mzuri wa utendaji kazi kwa ushirikiano (team work) kwa kuwa kazi ya usimamizi wake ilishirikisha wizara na taasisi mbalimbali za serikali nchini.

Katika maelezo yake mafupi kumkaribisha Mgeni rasmi, waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee ambae pia ndie aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ujenzi wa Meli hiyo aliwashukuru wajumbe wote wa kamati walioshiriki hadi kufikia hatua ya kukabidhiwa meli hiyo.

“Kamati tulishirikiana wote kwa pamoja wakiwemo Mawaziri wa Mindombinu na Mawasiliano pamoja na Ofisi ya Mwanasheria chini ya Mwanasheria Mkuu wa zamani na wa sasa” alieleza na kubainisha kuwa wajumbe wa kamati hiyo hakuwahi kulipwa posho.

Waziri huyo alibainisha kuwa baadae mchana kutakuwa na hafla ya kusaini mkataba wa makabidhiano ya meli hiyo ambapo kampuni ya Daewoo itaikabidhi rasmi meli hiyo Serikali ya Mpinduzi ya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti  wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed Shein ameipongeza kamati ya usimamizi  iliyoshuhulikia utengenezaji wa Meli Mpya Mapinduzi II kwa kuweza kukamilika kwake.

Pongezi hizo alizitoa leo huko Bandarini wakati wa uzinduzi wa Meli hiyo ya kisasa ya ambayo imetengenezwa na Kampuni ya Daewoo International  kutoka  Korea ya Kusini.

Alisema kuwa Meli hiyo ni mpya na yenye mitambo ya kisasa yenye uwezo mkubwa  ambayo haiyumbishwi, kwani inavyombo maalumu vya kurekebisha mwenendo wa mawimbi mkondoni.

“Wananchi Msisikilize maneno ya mitaani kuwa Meli imeshatumika suala hilo halina ukweli, nawataka muje kuitembelea meli hiyo ili  kuweza kujionea wenyewe”. Amesema Dkt Shein.

Aidha alisema kuwa utaratibu wote wa utengenezaji tokea hatua ya awali hadi kumalizika kwake umeonyesha na Kampuni ya Daewoo ya Korea haiwezi kudanganya na kuihadaa Dunia na imeweza kugharimu Dola million 30.4 za kimarekani na ujenzi ulianza mnamo July 2013 hadi Disemba 2015 kuwasili Zanzibar.

Rais wa Zanzibar alisema kuwa kazi iliokuwepo  hivi sasa ni wananchi kuweza kuitunza  na kuihifadhi  meli hiyo ibakie kuwa na haiba na uzuri wake.

Aidha alisema kuwa Meli ya Mapinduzi II ni mpya na yakisasa  yenye uwezo mkubwa wa kusafirisha abiria 1200  na mizigo tani 200.

Alifahamisha kuwa kukamilika kwa meli hii mabadiliko makubwa yameweza kufanyika katika shirika la meli na uwakala tiketi zinauzwa kwa njia za kutumia komputa abiria hawezi kuuziwa tiket mpaka awe na kitambulisho cha Mzanzibar ,Mtanzania au kwa mgeni awe shahada ya kusafiria.

Pia alieleza kuwa Serikali inategemea kuweka Bandari kubwa ya mizigo eneo la Maruhubi mpiga duri na tayari imeshaanza makubaliani na Serikali ya China kuanzia mwezi wa Januari au Febuari wanatarajiwa kuanza  kazi ya ujenzi.


Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Utengenezaji wa Meli ambae pia ni Waziri wa Fedha Omar Yusuf Mzee amesema ameridhika na umalizaji wa meli hiyo na kutoa shukrani kwa wale wote waliokuwa sambamba katika kukamilisha kazi hiyo.

No comments:

Post a Comment