ZANZIBAR.
Rais
wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza umuhimu wa taasisi za serikali
kufanyakazi kwa pamoja katika kupanga na kugawana rasilimali fedha ili
kufanikisha utekelezaji wa malengo yaliyowekwa.
Dk. Shein ameeleza hayo alipokuwa akizungumza na
uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo katika kikao cha
kutathmini utekelezaji wa mpango kazi na bajeti ya Wizara hiyo katika kipindi
cha miezi tisa kuanzia Julai 2013 hadi 2014.
Amesema
kuwa utaratibu wa kupanga na kutekeleza kwa pamoja kazi za Wizara na kuweko na
uwazi katika ugawaji na utumiaji wa rasilimali fedha ndio njia pekee
zitakazosaidia kufikia malengo yaliyopangwa na Wizara kwa ufanisi.
aidha
kiongozi huyo Amebainisha kuwa watendaji wa serikali wanajukumu kubwa la
kuhakikisha kuwa fedha za umma zinazopatikana baada ya kukusanywa kutokana na
kodi na malipo mengine mbali mbali zinatumiwa ipasavyo ili kuhakikisha kuwa
tija inayotokana na matumizi ya fedha hizo inaonekana na inawanufaisha wananchi
wote.
Amezitaka
taasisi za serikali kuwa na muongozo utakaoweka bayana vipaumbele vyake, na
mgawanyo wa fedha kufanywa kwa mujibu wa vipaumbele vitakavyobainishwa katika muongozo husika.
Akizungumzia
suala la kuimarisha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Rais wa Zanzibar
ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuchukua hatua za
dharura kukabiliana na changamoto zinazolikabili Shirika hilo ili liweze
kuendesha shughuli zake kwa mafanikio sambamba na kukabiliana ushindani mkubwa
wa kibiashara.
Amesema
serikali tayari imeshatoa fedha nyingi katika Shirika hilo na kusisitiza kuwa
hakuna sababu ya kushindwa kujiendesha kibiashara.
Aidha,
Rais wa Zanzibar ameiagiza Wizara hiyo kufikiria namna itakavyoweza kuimarisha
Tume ya Utangazaji Zanzibar ili iweze kufanya kazi zake ipasavyo.
No comments:
Post a Comment