Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein leo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe ofisini kwake Ikulu.
Waziri Chikawe ambaye alifuatana na Naibu wake Bwana
Pereira Ame Silima alifika Ikulu kujitambulisha rasmi kufuatia mabadiliko ya
Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.
Jakaya Mrisho Kikwete mwezi Januari mwaka huu.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimpongeza Waziri
Chikawe na Naibu Waziri Silima kwa kukubali uteuzi wa kushika uongozi wa Wizara
hiyo yenye majukumu mazito na muhimu ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
Alimueleza waziri huyo kuwa Taasisi za Wizara yake
Zanzibar zinafanya vizuri na kuzipongeza taasisi hizo kwa ushirikiano wake na
utekelezaji mzuri wa majukumu yao.
Hata hivyo alieleza kuwa pamoja na taasisi hizo, ikiwemo
Jeshi la Polisi kukabiliwa na changamoto kadhaa lakini watendaji wake wamekuwa
wakionesha ujasiri na kuliletea sifa jeshi hilo.
Alitoa pongezi maalum kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa-NIDA kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikiifanya tangu zoezi la uandikishaji
wa vitambulisho hivyo ilipoanza hapa Zanzibar.
Dk. Shein aliukumbusha uongozi wa Wizara hiyo ya Mambo ya
Ndani ya Nchi wakiwemo Waziri na Naibu Waziri kuweka utaratibu maalum wa
kutembelea taasisi zake zilizoko Unguja na Pemba mara kwa mara ili kuangalia
utendaji na mazingira ya utendaji kazi ya taasisi hizo.
Katika mazungumzo hayo ambayo yalihudhuriwa pia na
Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Bwana Dickson Maimu na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA
Zanzibar Bwana Vuai Mussa Suleiman, Dk. Shein aliitaka Wizara hiyo pamoja na mafanikio
iliyoyapata kuongeza juhudi na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu
yake.
Wakati huo huo Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi Mathias Chikawe katika mazungumzo hayo alimwambia Mhe
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwa Wizara yake
imejidhatiti katika kuimarisha utendaji kazi wa wizara na taasisi zake kwa
kubuni mbinu na mikakati ambayo inaendana na mazingira ya sasa.
Aliongeza kuwa wizara na taasisi zake zinatekeleza
majukumu yake na ulinzi wa raia na mali zao na kuwa jitihada zinafanywa
kuzipatia nyenzo taasisi zinazohusika ili kuongeza ufanisi katika kazi.
No comments:
Post a Comment