ZANZIBAR.
WIZARA ya Afya
Zanzibar, imesema kuwa itahakikisha hatua zilizofikiwa katika kupunguza vifo
vya akimama wajawazito na watoto wakati wa kujifungua zinakuwa endelevu ili
kufikia malengo ya millennia.
Mkurugenzi Mipango,
Sera na Utafiti katika wizara hiyo Abdullatif Haji, amesema katika mkutano wa
siku moja kufunga mradi wa miaka mitano uitwao MAISHA uliofanyika katika hoteli
ya Grand Palace Zanzibar, kuwa lazima juhudi za kuimarisha afya ya mama na
mtoto ziendelezwe.
Mkurugenzi huyo
amepongeza hatua iliyofikiwa kwa kupunguza vifo hivyo kutoka 377 mwaka 2012,
hadi kufikia 221 kwa sasa.
Amefahamisha kuwa,
vifo vya akimama wajawazito na watoto vinaweza kupunguzwa na kumalizwa kabisa,
kama kutakuwa na mkakati madhubuti wa utoaji huduma endelevu na uangalizi wa
kutosha kabla na baada ya kujifungua.
Mkurugenzi huyo amewashukuru
watu wa Marekani na serikali yao na USAID, kwa msaada wao mkubwa na muhimu, kwa
kufanya kazi bega kwa bega na Zanzibar katika kuhakikisha vifo vitokanavyo
na uzazi vinapungua kwa kiasi kikubwa Unguja na Pemba.
Alisema lengo la
Wizara ya Afya, ni kuhakikisha kuwa vifo vya mama wajawazito vinavyotokana na
uzazi na vya watoto wanaokufa wakati wa kuzaliwa, vinapungua hadi 150 ifikapo
mwaka 2015.
Mapema, Mkurugenzi
Mkazi wa Jhipiego nchini Tanzania Maryjane Lacoster, ameelezea kuridhishwa
kwake na ushirikiano wanaoupata kutoka
serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi
Zanzibar.
Naye Mwakilishi wa
USAID nchini Tanzania Lisa Patel, ameishukuru Wizara ya Afya Zanzibar, kwa
kuupa ushirikiano mradi huo uliorahisisha wanawake kupata huduma bora kutokana
na vifaa vya kisasa wakati wa ujauzito, kabla na baada ya kujifungua.
Kwa upande wake,
msimaizi mkuu wa mradi wa MAISHA Dk. Dunstan Bishanga, alieleza kuwa, tangu
kuanzishwa kwa mradi huo mwaka 2008, zaidi ya watoa huduma 250 Unguja na
Pemba, wamepatiwa mafunzo kuhusiana na jinsi ya kuwahudumia akina mama
wajawazito na watoto.
No comments:
Post a Comment