Jumla ya kampuni 160, alama za biashara 430, majina ya biashara 280, jumuiya za kiraia 67 na nyaraka 583 zimesajiliwa katika kipindi cha robo tatu ya mwaka wa fedha 2013/2014.
Akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji Mpangokazi wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014 jana Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Assaa Ahmad Rashid alieleza pia kuwa katika kipindi hicho Wizara imesajili vizazi 27,445 kote nchini.
Alibainisha kuwa kati ya vizazi hivyo 13,742 ni wanaume na 13,703 ni wanawake huku vifo vilivyosajiliwa vikiwa ni 1,648 kati yake wanawake ni 760 na wanaume 888.
Katika kikao hicho Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa katika kuimarisha utoaji huduma za Zakka na Wakfu Wizara katika kipindi hicho imeendelea na jitihada za kuelimisha waumini kuhusu masuala hayo ambapo mikutano 24 iliyokusanya wadau mbalimbali ilifanyika na miongozo ya zakka, mirathi na Wakfu iligawiwa Unguja na Pemba pamoja na kutoa vipindi vya elimu kwa njia ya redio na televisheni.
Katika hatua nyingine taarifa hiyo ilieleza kuwa Wizara imo mbioni kukiimarisha Kituo cha Utafiti na Mafunzo ya Sheria Zanzibar ambapo hivi karibuni kinatarajiwa kupata hati ya utambulisho(accreditation) ili kuanza kutoa mafunzo ya sheria katika ngazi ya cheti na Stashahada kuanzia mwezi Julai mwaka huu.
Kwa upande wa hakimiliki taarifa hiyo ilieleza kuwa Wizara kwa mara ya kwanza imeweza kugawa mirahaba kwa wasanii na wabunifu 726 ambapo jumla ya shilingi milioni 36 ziligawiwa. Katika kipindi hicho Wizara imeweza pia kusimamia mapito ya Sheria ya Hakimiliki.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato katika Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa hadi mwisho wa robo tatu ya mwaka wa fedha Wizara imekusanya shilingi milioni 345.1 ikiwa ni sawa na asilimia 79 ya lengo la kukusanya shilingi milioni 435.
Katika kikao hicho kilichofanyika Ikulu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK. Ali Mohamed Shein amezitaka Wizara na Taasisi za Serikali zilizo na jukumu la kukusanya mapato kuongeza juhudi ili Serikali iweze kupata mapato zaidi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Alibainisha kuwa mwenendo wa ukusanyanji mapato kwa upande wa Bodi ya Mapato Zanzibar- ZRB na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA unakwenda vizuri kwa makusanyo kuongezeka mwaka hadi mwaka lakini alisisitiza kuwa wizara na Taasisi nyingine zinapaswa kuiga mfano wa taasisi hizo.
Mhe Rais alizikumbusha Wizara kuzingatia utaratibu wa Bangokitita kwa kuwa ni utaratibu endelevu unaokwenda sambamba na mfumo wa ukusanyaji mapato na matumizi ya Serikali pamoja na utekelezaji wa kazi za Serikali ambao unategemea bajeti iliyopangwa.
Katika kikao hicho alihimiza uwekaji wa kumbukumbu za Serikali kwa kuanzisha na kuimarisha maktaba katika wizara na taasisi za serikali ili kutoa fursa kwa watumishi kuongeza taaluma zao na kujifunza mambo mbali yanayofanyika katika Wizara na taasisi pamoja na duniani kwa jumla.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
No comments:
Post a Comment