Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein leo amemwapisha Bwana Chimbeni Heri Chimbeni kuwa Mshauri wa
Rais Masuala ya Utamaduni kufuatia uteuzi alioufanya hapo jana ambapo aliteua
pia watendaji wengine wa serikali.
Watendaji wengine walioapishwa leo ni Bwana Juma Hassan Juma
Reli kuwa Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango, Bwana Mdungi Makame Mdungi kuwa
Katibu Kamisheni ya Utumishi wa Umma na Bwana Kai Bashir Mbarouk kuwa Naibu
Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria.
Bwana Reli ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali
ikiwemo ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania anachukua nafasi ya Bi Amina
Khamis Shaaban ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na
Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kabla ya uteuzi wa kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma
bwana Mdungi alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba Sheria.
Kwa upande wa Bwana Kai Bashir kabla ya uteuzi huo alikuwa
Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Wizara hiyo.
Hafla hiyo fupi iliyofanyika Ikulu ilihudhuriwa na viongozi
mbalimbali wakiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi,
Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Said
Hassan Said.
Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala
Bora Dk. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa
Umma Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman, Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya
Mzee, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Maalim Abdulla Mwinyi na Makatibu na
Manaibu Katibu wakuu wa wizara mbalimbali.
No comments:
Post a Comment