Na Hafidh Hussein,
Zanzibar.
MAISHA ya Mwanadamu yeyote
katika sayari hii ya Dunia yametawaliwa na mambo mengi ambayo kimantiki
uonekana kama furaha ama uzuni, ambayo yote hayo katika falsafa za kiimani
uitwa mitihani inayotokana na majaaliwa ya Mola kwa wanadamu na viumbe vingine.
Kilichonisukuma kuandika
makala haya ni kutokana na kuguswa na maisha halisi aliyepitia kijana mmoja
mwenye historia ya kusisimua anayeitwa Hilmy Faria Shawali tangu anazaliwa mpaka sasa
kwa ufupi naweza kueleza kuwa kimtizamo ni masahibu na mitihani.
Lakini pia naweza
kunasibisha msemo maarufu unaotumiwa na wazee wetu ama watu wazima wakati
wanapokuwa wakitoa usia kwa vijana wao kwamba “Kama hujafa ujaumbika” msemo huu
umekuwa na maana pana sana juu ya maisha ya mwanadamu ya kila siku kwani kila
mmoja Mwenyezi mungu anampa mtihani wake katika hii dunia.
Kijana huyo ambaye ni Hilmy
Faria Shawali ni mtoto wa kwanza katika Familia ya mzee Faria Shawali amezaliwa
Septemba 29, mwaka wa 1996 katika hospitali ya
Chelsie Westminister katikati ya mji wa London nchini Uingereza.
Hilmy katika kipindi cha
miaka 19 aliyonayo amepitia masahibu mengi mpaka kufikia alipo sasa na laiti
kama sio ujasiri wa baba yake mzazi leo nisingeandika Makala hii.
Kama ilivyo kawaida ya
nchi za wenzetu hasa za Magharibi zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo kufuatilia
makuzi ya mtoto toka akiwa tumboni kwa mama yake, kutokana na ukuwaji wa
Teknolojia ya sayansi na vifaa vya kisasa katika Hospitali zao, hivyo wakati wa
ujauzito wa miezi minne tayari Hilmy alishajulikana atakuwa ni mtoto wa namna
gani.
Kutokana na maumbile yake
Jopo la wataalamu wakiwemo wakunga na Matatibu wakashauri familia ya mimba ya
Hilmy itolewe maana mtoto atakayezaliwa atakuwa mwenye ulemavu wa viungo.
Ushauri wa kutolewa mimba
hiyo ni kutokana na Imani na tamaduni za wazungu walioamini kuwa motto huyo
akizaliwa anakuja kuwatesa na kuwasumbua
wazazi wake lakini kutokana na Imani ya dini aliyokuwa nayo Baba yake Hilmy, alikataa ushauri huo na kutaka mtoto huyo azaliwe licha
ya madaktari kumsihi mara kwa mara afuate ushauri wao.
Mzee Faria alianza
kutawaliwa na hofu kutokana na Madaktari kumsumbua mara kwa mara akubali
kutoa mimba ya mkewe, hali iliyopelekea
kwenda mara kwa mara katika hospitali aliyopangiwa mkewe Klinic licha ya kuwa
mbali na sehemu aliyokuwa akiishi, lakini ilimlazimu kutumia usafiri wa (Public
Transport).
Kutokana na Mzee huyo kuwa
ni mgeni katika nchi hiyo ilibidi kuacha kazi kwa ajili ya kufuatilia kwa
ukaribu hali ya mke wake ndipo baba yake akakutana na daktari mmoja kutoka
kenya akamwambia kuwa yeye ni muislamu hawezi kukubali mimba ya mke wake
itolewe.
“ Wewe unajua mimi ni
muislam sitoweka kukubali mimba itolewe kwa misingi ya dini yangu, na isitoshe
eti kutokana na kuwa kiumbe kilichokuwa ndani ya tumbo la mke wangu kina
ulemavu”, alisisitiza Faria na kuendelea kuweka wazi msimamo wake huo kuwa ni
lazima mtoto huyo azaliwe hali iliyopelekea Madaktari kumuunga mkono huku
wakimwambia kuwa mtoto huyo akizaliwa kupona ni bahati.
Wakati wa kujifungua
ulifika na ikabidi Mama yake Hilmy awe china ya uangalizi wa madaktari kwa
lengo na kukabiliana na lolote linaloweza kutokea.
Jopo la Madaktari
walifanya kazi kubwa ya kuokoa maisha ya Mama na mtoto kutoka lipozaliwa usiku
wake alifanyiwa upasuaji (Operesheni) kubwa ambayo hata madaktari hawakutegemea
kupona kwa mtoto huyo.
Upasuaji huo kitaalamu
unaitwa Spinali Bifida na kulazimika
kukaa, Chumba cha wagonjwa Mahututi (ICU) kwa muda wa wiki mbili mara baada ya
upasuaji huo, alilazimika kufanyiwa
upasuaji nyingine mkubwa wa kichwa ambayo ulijulikana kama Unshunt nayo
madaktari walikuwa na nusu kwa nusu kunusuru maisha ya Hilmy, lakini kwa uwezo
wa mola madaktari walipatwa na mshangao maana Hilmi alipona.
Akiendelea na matibabu
yake Hilmy alikuwa akiishi katika maisha ya kufanyiwa matibabu kwa njia ya
upasuaji ambapo mpaka sasa inasadikika tayari ameshafanyiwa upasuaji 50, kati ya hizo 13 zilikuwa za za kawaida,
licha ya huzuni na majonzi kwa upande wa Mama yake Hilmy lakini Baba mzazi wa kijana huyo, alisimama kidete kwa kumliwaza na kumfariji mkewe kwa
kuamini hiyo yote ni mipango ya mwenyezi mungu.
Maisha ya Hilmy
yaliendelea chini ya uangalifu na umakinifu wa wazazi wake na kujitahidi kumkuza mtoto wao
katika hali ya kumfariji ili ajihisi yeye ni sawa na watoto wengine
alipofikisha umri wa kwenda shule naye alipelekwa shule na wazazi wake ili
kujiunga na watoto wenzake.
Hilmy alisoma katika shule
za kawaida shule ya John Chilton walimu wa shule aliyosoma hawakumuacha mkono
Hilmy walimpa uangalizi wa hali ya juu
kutokana na hali yake ya ulemavu aliyonayo na alisoma hapo mpaka alipo maliza
kidato cha sita na mwaka huu wa 2015 Hilmy yupo Chuo Kikuu anasomea uandishi wa
Habari za Michezo (Sport Journalism) .
Katika kusoma kwake Kijana
huyo elimu ya Chuo kikuu anakabiliwa na changamoto kubwa ya umbali wa kutoka
anapoishi mpaka kufika chuo maana anakaa Mji wa London Middlesex kitongoji cha
Han Well anasoma katika university ya Hendon Middlesex.
Kama ilivyo kawaida kwa
raia wa Zanzibar waishio nje ya nchi yao hutenga muda maalum kwa watoto wao
aidha kila mwisho wa mwaka shule zinapofungwa au kila baada ya muda Fulani
kuwaleta watoto wao katika nchi zao za asili walizozaliwa ili kujifunza lugha
zao za asili yaani lugha mama au kuja kuzijulia hali familia zao kwa lengo la
watoto kufahamu familia za wazazi wao.
Baada ya kutembelea
familia zao zilizopo Zanzibar Hilmy aligundua kitu cha ziada ambacho hata madaktari
waliokuwa wakimuhudumia mama yake kipindi cha ujauzito wake walishindwa
kugundua kitu gani kilifichikana katika mimba ile na vipi kitaleta faraja kwa
walemavu wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Mnamo mwaka 2013 akitokea
katika jiji la London kuja Zanzibar
katika safari za kawaida kutembelea nchi ya wazazi wake hapo Hilmy akiwa na
miaka kumi na saba alipofika alipata fursa ya kutembelea maeneo tofauti ya mji
wa Unguja katika pita pita zake zake alikutana na watu tofauti bila ya mtu
yeyote kujua nini Hilmy anafikiria na athari gani anaipata akiwa katika kigari
chake cha kutembelea (Will Chair).
Katika hali isiyokuwa ya
kawaida Hilmy alipokuwa akitembea katika maeneo mbali mbali, alikutana na Watu
wenye maumbile kama yake yaani watu wenye ulemavu wanaohitaji misaada maalum
kutokana na uhalisia wa maumbile yao.
Watu hao walimgusa kwa
kiasi kikubwa kijana Halmy na muda wake mwingi kuzingatia ni kwa kiasi gani
anaweza kuwasaidia ni watu wenye hali kama yake ambao ni walemavu maana
aliguswa na hali zao na jinsi wanavyokosa mahitaji muhimu wengine wanasota hata
nyenzo za kutumia kutoka sehemu moja au nyingine hawana.
Baada ya muda wa likizo
kuisha na kurudi uingereza ndipo alipomwita Baba yake mzazi na kumuelezea dhamira
na lengo lake la kuanzisha Jumuiya ambayo itamuwezesha kuwasadia watu wenye
ulemavu wanaoishi Zanzibar.
Baada ya kijana huyo
kuzungumza yaliyokuwepo moyoni na kueleza kinaga ubaga hali halisi ya watu
wenye ulemavu wanaoishi Zanzibar, Baba yake alipoteza ujasiri na kuenda kukaa
pembeni na kuanza kutokwa na machozi kwa kuona mwanawe amafikiria jambo kubwa
ambalo hata yeye hakuwahi kulifikiria licha ya mara kwa mara alikuwa anakuja
nyumbani kwao Zanzibar.
Baba Mzazi wa kijana huyo
alifikria mengi na hata kuwaza kuwa alipokuwa anakuja Zanzibar alikuwa akikutana
na Watu wenye ulemavu ambapo aliweza kumsaidia mtu mmoja mmoja na kwa vitu
ambavyo haviwezi kukidhi mahitaji yao yote ya msingi lakini hakuwahi kuwaza
kuanzisha jumiya (charity).
Malengo ya Hilmy juu ya Watu
wenye ulemavu wa Zanzibar ni mengi jambo ambalo mwandishi wa Makala hii
alipopata fursa ya kukaa na Hilmy na kuzungumzia masuala mbali mbali alimwambia
mambo mengi anayopanga kuyafanya juu ya maendeleo ya watu wenye ulemavu.
Miongoni mwa mambo ya
msingi aliyoyapa kipaumbele katika mipango yake ni kuwa anatamani siku moja awe
na uwezo wa kuwafikia watu wote wenye ulemavu ili aweze kuwapa mahitaji yao ya
msingi ili waishi kama watu wengine.
“ Natamani siku moja niwe na
uwezo wa kuwafikia watu wenye ulemavu wote wa Zanzibar ili niweze kuwapatia
mahitaji yao yote ya msingi”
Bado nina imani kuwa
Mwenyezi mungu atanijaalia kufikia malengo yangu, kwani nakuwa naumia sana
ninapoona mtu mwenye ulemavu kama mimi anaishi katika hali ya kukata tama
kutokana na kukosa huduma za msingi hata za kumuezesha kutoka sehemu moja
kwenda nyingine kwa usalama”,. alisema Hilmy huku akiwa na hisia za huruma na
kuonyesha nia ya dhati ya kuwajali wao hao.
Katika juhudi za
awali kijana huyo amefanikiwa kuanzisha Taasisi
yake kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye ulemavu Zanzibar inayojulikana kama
“Hilmy Charity” ambayo ni jumuiya isiyokuwa ya kiserikali inayotambuliwa na
serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Jumuiya hiyo imesajiliwa
mwaka ………na kuanza kufanya kazi zake rasmi mwaka…. Ambayo ipo chini ya mwamvuli wa jumuiya zisizo za
kiserikali Zanzibar (Angoza) inayofanywa kazi za kuwasaidia watu wenye ulemavu
nchini.
Hilmy Charity tayari
wametoa msaada wa vigari( Will Chear) vya watu wenye ulemavu 220, ambavyo tayari vimetolewa katika maeneo
mbali mbali ya mikoa ya Zanzibar, kwa upande wa Unguja 150 pamoja na Pemba
vigari 70.
Licha ya ulemavu wa Hilmy
anauthibitishia ulimwengu kuwa ulemavu sio kikwazo cha kufikia malengo ambapo
mpaka sasa anashiriki mashindano ya mbio
za vigari ya mita 200 na 400 ya watu wenye ulemavu na tayari ameshiriki katika
mashindano mbali mbali ikiwemo London youth ,Middlesex, Bedford na mengineyo
mengi na ameshinda katika baadhi ya mashindano na kuchukua medani sita za dhahabu
na mategemeo yake ni ifikapo mwaka 2020 kushiriki mashindano ya Olimpic ya
Tokyo.
Kijana huyo Hilmy Faria Shawal
ni mtoto wa mchezaji wa zamani wa mpira
wa miguu katika timu ya Small Simba Zanzibar ambayeni ni Faria Shawal, pamoja
na ulemavu wake haukumfanya wazazi wake wamfungie ndani na kumuona ni mkosi
kwao bali walimpa fursa za kuishi kama watu wengine.
Kutokana na historia
halisi ya Maisha ya Hlmy unaweza kuwa na maswali mengi ya kujiuliza ikiwemo
kuwa je kama Baba yake angekubali Madaktari watoe mimba yake nyota yake
ingeweza kung’ara kwa watu wengine, na je baada ya kuzaliwa laiti wazazi wake
wangemfungia ndani na kumkosesha fursa ya kupata elimu angeweza kuwa msaada na
mfano wa kuigwa kwa watu wengine, hivyo majawabu ya maswali hayo yapo vichwani
mwa wasomaji wa makala hii huku tukikubaliana kuwa ulemavu kwa binadamu sio
mkosi ama usumbufu kwa watu wengine bali ni majaaliwa ya mola.
Bado kijana huyo mwenye
ulemavu anaishi kwa kujiamini na kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, hivyo
jamii ya Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kuendelea kuunga mkono
juhudi za kijana huyo kwa lengo la kujenga jamii shirikishi ya watu wenye
ulemavu ili waweze kuishi kwa amani na utulivu kama walivyo watu wengine.
Jamii ni vyema kuanzia
sasa kila mmoja akajihesabu kuwa ni Mtu mwenye ulemavu wa kesho hata kama leo
anajihesabu kakamilika kwani sababu za ulemavu kwa asilimia kubwa zinatokana na
asili ya maisha yetu ya kila siku zikiwemo ajali, maradhi ama kuzaliwa na
ulemavu mambo ambayo kwa kiasi kikubwa hayana kinga ya moja kwa moja hivyo kila
mmoja anaweza kuwa katika hali hiyo, hivyo tuungane kwa pamoja kulaani vikali
vitendo vya udhalilishaji kwa watu wenye ulemavu na kuwa mabalozi wema wa
kuunga mkono juhudi za maendeleo za watu hao.
Katika mfululizo wa Makala
za Maisha na Vipaji vya watu wenye ulemavu pia tukae tayari kupokea Makala
nyingine hivi karibuni yenye kuelimisha na kusisimua ya Binti ambaye
anaishi na ulemavu wa viungo vya macho aliyemaliza shahada yake ya sharia na
kuwa msaada mkubwa kwa watu wenye ulemavu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment