Zanzibar 1.1.2016
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya siku ya mazoezi
Kitaifa yalioanza katika viwanja vya Tumbaku hadi uwanja wa Amaan na kusisitiza
kuwa mazoezi ni tiba mbadala ya maradhi mbali mbali yanayojulikana na
yasiyojulikana ambayo yanaisumbua jamii katika maisha yao ya kila siku.
Katika hotuba yake
aliyoitoa mara baada ya kupokea maandamano ya
vilabu mbali mbali vya mazoezi vya hapa Unguja, Pemba pamoja na vilabu
kutoka Tanzania Bara, huko katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar, Dk. Shein
alieleza kuwa mazoezi ni kinga na yanapunguza uwezekano wa kupata maradhi mbali
mbali.
Akiyataja baadhi ya
maradhi ambayo yanaweza kuondoshwa kwa kufanya mazoezi Dk. Shein alisema ni pamoja na maradhi ya saratani, kisukari,
ugonjwa wa moyo na shindikizo la damu sambamba na kusaidia kupunguza uzito na
unene uliokithiri.
Dk. Shein aliwataka
wananchi na wanamichezo wasingojee mpaka wapate maradhi ndipo waanze kufanya
mazoezi na badala yake wajipangie muda
wa mazoezi angalau dakika 30 kwa siku kwani kuna faida kubwa katika kukabiliana
na maradhi yanayoathiri afya.
“Iwapo hakuna tatizo
tujipe mazoea ya kutembea kwa miguu kwa safari zetu za karibu na hata kuepuka
kuanda ‘lifti’ kama unapokwenda pana uwezekano wa kufika kwa ngazi ya kawaida
kwani yote haya yana faida katika kuimarisha afya zetu”, alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alieleza kufurahishwa sana na utaratibu wa kufanya mazoezi kupitia vilabu kwani
njia hiyo ina faida nyingi zaidi badala ya kufanya mazoezi kwa mtu mmoja mmoja
ambapo pia hatua hiyo, inaimarisha umoja na mshikamano.
Dk. Shein, alitumia
fursa hiyo kuwapongeza akina mama ambao zamani hawakuwa wakionekana kuwa wengi
katika shughuli za michezo na hasa wanapofikia umri wa watu wazima lakini siku
hizi kwa sababu ya kupata mwamko na kufahamu umuhimu wa mazoezi wamekuwa wengi
kama walivyojitokeza katika maadhimisho hayo.
Kwa upande wa
wastaafu, Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake kwa kuwaona baadhi ya wastaafu
walioshiriki mazoezi hayo na kueleza kuwa anaamini mazoezi yana mchango mkubwa
kwa wastaafu kwa kuimarisha afya na furaha katika maisha yao.
Dk. Shein alisema kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini umuhimu wa kuiendeleza sekta ya
michezo kwa kuzingatia historia ya Zanzibar ya kuwa na vipaji vya michezo mbali
mbali na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya michezo kwa
kukamilisha kazi ya uwekaji wa mpira wa kukimbilia katika uwanja wa Gombani na
ujenzi wa uwanja wa Mao-tse-tung kwa kushirikiana na Serikali ya China.
Dk. Shein alieleza
kuridhishwa kwake na Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na
Michezo katika kutekeleza lengo la kurudisha vuguvugu la michezo katika maskuli
kwa lengo la kuibua vipaji.
Alisema kuwa katika
mradi huo ambao matayarisho yake yameanza tangu mwezi Mei mwaka jana na unatarajiwa
kuanza mwezi Februari mwaka huu na unatarajiwa kumaliza mwaka 2017, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar itachangia Shilingi milioni 480 na fedha zote zilizobaki
zitatolewa na Serikali ya Watu wa China.
Katika mradi wa ujenzi
wa mji wa kisasa katika maeneo ya Fumba ambao matayarisho yake yamekwishaanza,
pia, utajumuisha ujenzi wa kiwanja cha michezo wenye uwezo wa kuchukua watu
45,000.
Pia, Dk. Shein alisema
kuwa katika eneo la Kijini Matemwe
katika Mkoa wa Kaskazini Unguja Kampuni ya ‘Penny Royal’ inayojenga mji wa
kisasa katika eneo hilo, vile vile itajenga kiwanja cha Kimataifa cha mchezo wa
gofu chenye juma la vishimo 18.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kueleza umuhimu wa kuzingatia nidhamu katika michezo ili kuepuka
migogoro hasa katika vilabu vya michezo hapa Zanzibar kwani migogoro hupunguza
nidhamu michezoni na huviza maendeleo ya michezo.
Dk. Shein alisema kuwa
yeye akiwa ni mwaka michezo anahuzunishwa na kusikitishwa sana na migogoro na
mivutano michezoni kwani sio jambo linalotoa taswira nzuri ya maendeleo ya
michezo hapa Zanzibar.
“Nawasihi wanamichezo
wenzangu tufanye kila linalowezekana kuepuka mizozo isiyo ya lazima michezoni
ili kwa pamoja tuweze kufikia azma yetu ya kurudisha hadhi ya Zanzibar katika
tasnia ya michezo”,alisema Dk. Shein.
Dk. Shein aliwaeleza
wanamichezo hao wa mazoezi ya viungo Zanzibar kuwa ataendelea kushirikiana nao
na hata wanapotaka vifaa vya michezo ataendelea kuwatafutia pamoja na misaada
mengine kwa kutambua kuwa wanakila sababu ya kudeka kwa Rais wao.
Aidha, Dk. Shein
alimuagiza Waziri wa Kilimo na Maliasili Dk. Sira Ubwa Mamboya, kukutana na
uongozi wa Chama cha Mchezo wa Mazoezi ya Viungo Zanzibar (ZABESA) kwa lengo la
kuwakabidhi eneo la kilimo waliloliomba na kuwataka wachague ni kilimo cha aina
gani wanakusudia kulima.
Dk. Shein alitoa
pongezi kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa kushirikiana na
(ZABESA) pamoja na Baraza la Michezo pamoja na wanavilabu wote kwa kufanikisha
bonaza hilo linalofanyika kila ifikapo Januari 1 ya kila mwaka.
Dk. Shein pia, alitoa
wito kwa wanamichezo wote nchini pamoja na wananchi kujitokeza kwa wingi
kuangalia michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo ni maalumu kwa kuadhimisha
Mapinduzi matukufu ya Januari 12, mwaka 1964 huku akisisitiza kuwa timu za
Zanzibar zihakikishe kombe la Mapinduzi linabaki nyumbani.
Nae Mwenyekiti wa
Baraza la Michezo Zanzibar (BMZ) Sharifa Khamis, aliwaeleza wanamichezo hao pamoja na wananchi
walioshiriki maadhimisho ya siku ya mazoezi kitaifa kuwa Dk. Shein ndie aliyedhamini maadhimisho hayo
na kumpongeza kwa juhudi zake hizo huku akisisitiza kuwa wanamichezo
wataendelea kudeka kwa Rais wao huyo kwani anawajali.
Nao wanavilabu
haokutoka vikundi zaidi ya 40 kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara katika
risala yao walitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kushirikiana nao katika bonaza
hilo sambamba na kuendelea kuwaunga mkono huku wakiwasisitiza wananchi kufanya
mazoezi na kuiomba Serikali kuweka siku maalum kwa watendaji wote Serikalini
kufanya mazoezi.
Katika bonanza hilo
Dk. Shein alikabidhi vyeti kwa vilabu mbali mbali vya Unguja, Pemba na Tanzania
Bara, Shirika la Bandari, Kocha wa kike ambaye ni muasisi wa bonaza hilo Bi
Nasra Juma Ramadhan.
Viongozi mbali mbali
walishiriki katika bonanza hilo la maadhimisho ya siku ya mazoezi na kuungana
na Rais kwa matembezi tokea viwanja vya Tumbaku hadi uwanja wa Aman mjini
Unguja, akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
No comments:
Post a Comment