Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alisema kwamba Maadhimisho ya Sherehe za kutimia Miaka 52 ya Mapinduzi ya
Zanzibar ya mwaka 1964 yatafanyika kama kawaida na kupangwa kuanza rasmi jumapili ya Tarehe 3 Januri 2016.
Alisema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba
katika muda wote wa maandamisho hayo kunakuwa na hali ya utulivu na usalama
mkubwa katika maeneo yote ya Visiwa vya vya Unguja na Pemba.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri
ya Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar alisema hayo wakati akitoa Taarifa rasmi ya
ratiba ya maadhimisho ya sherehe za Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar mbele ya
Wana Habari hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema suala la upande wa Upinzani kuzisusia sherehe za
Mapinduzi kwa kisingizio cha Rais aliyepo madarakani si halali ni
muendelezo wa kuwapotosha Wananchi walio wengi nchini.
Balozi Seif alifafanua kuwa Rais wa sasa Dr. Ali Mohammed
Shein ataendelea kuwa rais hadi yule atakayechaguliwa rasmi na kihalali na
Wananchi ale kiapo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kama
ilivyokwishatolewa ufafanuzi na wanasheria walio wengi.
Alisema tukio hili la maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya
Zanzibar kutimia miaka 52 ni jambo la kujivunia kwa kila Mwananchi wa
Visiwa vya Unguja na Pemba mpenda maendeleo na anayeifahamu vyema Historia ya
Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi.
Alieleza kwamba ipo miradi mingi na tofauti ya Wananchi
ambayo Viongozi na hata baadhi ya wanachama wa upande wa upinzani
walishiriki kuibuni sasa inakuaje miradi hiyo waiachie wakati tayari
imeshalengwa kuinufaisha jamii iliyowazunguuka.
“ Tuna kila sababu na ni haki yetu kusherehekea siku hii
adhimu katika Maisha yetu. Hivyo tuambizane, tushajiishane na tushiriki katika
matukio mbali mbali ya maadhimisho ya sherehe hizi kuanzia mwanzo hadi mwisho
“. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba
Miradi yote ya Maendeleo ipatayo 24 ambapo 16 ikiwa imekamilika na Minane
inatarajiwa kuwekwa mawe ya msingi imehusishwa katika maadhimisho hayo
itakayoanza Jumatatu ijayo.
Alisema madhimisho hayo yataanza rasmi kesho Jumapili
ikiwa ni siku maalum kwa kazi za usafishaji wa masingira katika maeneo
mbali mbali Unguja na Pemba ukilenga zaidi katika sehemu za kutolea huduma za
kijamii kama Hospitali, Vituo vya Afya pamoja na masoko.
Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Maadhimisho ya Kitaifa
Zanzibar alifahamisha kwamba ingawa zoezi hilo hufanyika kila zinaponza sherehe
za Mapinduzi lakini mwaka huu juhudi malum zinapaswa kuchukuliwa ili
kuhakikisha maeneo yote yanakuwa katika hali ya usafi muda wote.
Alikumbusha kuwa hivi sasa Taifa linakabiliwa na tatizo la
kuwepo kwa maradhi ya Kipindupindu, hivyo jamii ina wajibu wa kutumia
fursa hizi za maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi kwa kuchukuwa hatua za
kujikinga na kupambana na maradhi hayo ambayo kwa kiasi kikubwa husababishwa na
mazingira machafu ya sehemu zinazotumika na jamii katika shughuli za kila siku.
Alisema kwa vile suala la usafi wa mazingira ni la lazima
Viongozi Wakuu wa Kitaifa watahakikisha wanaungana na Wananchi katika
zoezi hilo kwenye maeneo watakayopangiwa.
Alieleza kwamba utaratibu maalum umeshaandaliwa kwa kila
mamlaka za Mikoa, Wilaya, Baraza la Manispaa, Mabaraza ya Miji na Halmashauri
za Wilaya katika kuratibu mfumo mzima wa kufanikisha zoezi hilo la usafi wa
mazingira.
Akigusia suala la hatma ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar
ambalo limekuwa agenda kubwa kwa baadhi ya watu wakiwemo hata wanasiasa nchini
wakiendelea kupotosha Wananchi Balozi Seif alisema Taarifa rasmi ya vikao
vinavyowakutanisha Viongozi wa juu kulijadili suala hilo itatolewa rasmi mara
baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo.
Hata hivyo Balozi Seif alitanabahisha kwamba Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar {
ZEC } kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ndio yenye mamlaka
ya kuendesha na kusimamia uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Alisema kwa vile tume hiyo kupitia Mwenyekiti wake
haikuridhika na mazingira yaliyojichomoza wakati wa zoezi la kupiga kura na
kulazimika kufuta Uchaguzi pamoja na matokeo yake yote Taasisi hiyo hiyo ndio
yenye uwezo wa kuitisha uchaguzi mwengine kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar.
Akijibu baadhi ya maswali ya Waandishi wa Habari Balozi Seif
alisema katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 iko wazi na kutoa mamlaka kwa tume ya
uchaguzi ya Zanzibar kupanga uchaguzi mwengine kufuatia kufutwa kwa ule wa
mwezi oktoba mwaka 2015.
“ Kinachosubiriwa kwa sasa ni Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
kutangaza Tarehe ya uchaguzi mwengine ambapo kujumu la kugharamia uchaguzi huo
limo ndani ya mamlaka ya Serikali Kuu yenyewe “. Alisema Balozi Seif.
Kuhusu Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao baadhi ya watu
wamekuwa wakitoa tafsiri potofu, Balozi Seif aliwajibu wanahabari hao
kwamba Baraza la Wawakilishi lilivunjwa lakini Rais wa Zanzibar bado
anayo Mamlaka ya kuliitisha iwapo kuna suala muhimu la Kitaifa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment