Na Ali Issa Maelezo –Zanzibar
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma Haruon Ali Suleiman ameshauri walimu watakaosomesha Skuli ya Zingwezingwe wawe walimu wanaoishi karibu na kijiji hicho.
Hayo ameyasema leo huko Zingwezingwe Mkoa wa Kaskazini, Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, wakati alipokuwa akifungua skuli mpya ya msingi ya kijiji hicho ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar .
Ametaka ushauri huo ufanyiwe kazi na iwapo watahitajika walimu wapya kuajiriwa kwa ajili ya kufundisha katika skuli hiyo Wizara yake ambayo ndiyo inayohusika na masuala ya ajira watakuwa tayari kufanya hivyo.
“Ni vyema kuajiri walimu wakaazi na wenyeji wa kijiji cha Zingwezingwe wenye kuyaelewa mazingira ya kijiji hicho na mimi kama Waziri wa Ajira niko tayari kusaidia hilo,” alisema Waziri Haroun.
Aidha aliwashauri wanafunzi wanaosoma katika skuli hiyo kuitumia frusa waliyoipata kusoma kwa juhudi kwani hiyo ni skuli ya kwanza kujengwa katika kijiji hicho.
Hata hivyo aliwataka wazazi na walezi kwa upande wao kutimiza wajibu wao wa kufuatilia kikamilifu maendeleo ya Watoto wao na kutoa ushirikiano kwa walimu ili kufanikisha maendeleo ya watoto wao.
Waziri Haroun aliwataka walimu kusomesha kwa juhudi kwani serikali tayari imeshatoa maelekezo ya kuwaongezea maslahi yao mara itakaporudi madarakani baada ya uchaguzi wa marejeo.
Katika kuongeza ujenzi wa madarasa mengine ya kusomea katika Skuli hiyo, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Kazi na Utawala wa Umma alichangia matofali 1000 ambapo ujenzi wake utaaza hivi karibuni.
Nae Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Balozi akitoa salamu za Baloz Seif Ali Idd alisema suala la umeme katika skuli hiyo litafanywa na Makamu huyo wa Rais.
Ujenzi wa skuli hiyo yenye madarasa manne na Ofisi ya Mwalimu Mkuu umegharimu shilingi milioni 66 ambazo zimetolewa na Shirika la Maendeleo la Sweden SIDA, Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini B, Mbunge na Mwakilishi na Wazee wa kijii cha Zingwezingwe.
No comments:
Post a Comment