tangazo
Thursday, January 7, 2016
TUHESHIMU NYAKATI LUQMAN MALOTO
TUHESHIMU NYAKATI
Mbwana Samatta ameitoa kimasomaso Tanzania. Watanzania waliomba na kutarajia na hakika imekuwa kweli. Hongera sana Mbwana kwa kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika kwa wachezaji wa ndani ya Bara la Afrika.
Tuzo ya Mbwana ina maana gani? Neno moja tu linatosha kujibu swali “Nyakati.”
Naam! Mbwana yupo kwenye wakati wake, ilikuwa lazima ashinde kwa sababu huu ni wakati wake, asingeshinda mwaka jana kwa sababu haukuwa wakati wake. Anaweza kushinda tuzo nyingine mwakani na kuendelea kama ni wakati wake.
Mwanamuziki Diamond Platnumz au Nasibu Abdul Juma, anatikisa Afrika kwa sasa akitokea Tanzania, ni kwa sababu huu ni wakati wake. Kila akigusa chupa, inakuwa almasi. Ni wakati wake.
Lazima kuheshimu nyakati. Na mafanikio ya Mbwana na Diamond, yawe fundisho kwa kila mmoja kutambua wakati wake na kuutumia vizuri kufika mbali na kupata mafanikio stahiki.
Wapo wengi hawakutumia vizuri nyakati zao. Alikuwepo fundi Haruna Moshi ‘Boban’, akasajiliwa Gefle IF ya Sweden mwaka 2010. Akatarajiwa kufika mbali. Haikuwa hivyo, alirejea nchini kwa kususa na alipofika Bongo, hakuwa Boban yule tena!
Ni nyakati za Floyd Mayweather! Anapigwaje sasa na wakati yupo kwenye wakati wake? Anatangaza kustaafu kisha anarejea ulingoni na hapigiki. Siku nyakati zake zikitoweka, atapigwa akiwa amelegea kama matembele.
Zilikuwepo zama za Mike Iron Tyson! Ilikuwa kabla hujaingia ulingoni, hakikisha umepima ubongo wako, maana ngumi yake ni kama bomu. Ikiwa ubongo wako haupo imara, akikupiga ngumi ya kichwa unakuwa mwendawazimu. Msome Frank Bruno yaliyomkuta.
Tyson alikuwa anamaliza pambano na kuingiza mpaka dola milioni 50 ndani ya sekunde 27. Aliyejifanya sugu na kusogea naye mpaka raundi 12, alikiona cha mtema kuni. Ila zilifika nyakati Tyson akawa akifika raundi ya sita anapigwa kirahisi kama mlenda. Yupo wapi Muhammad Ali? Zama zake zilishapita!
Unawakumbuka magolikipa tishio ulimwenguni kama Peter Schmeichel na Oliver Kahn? Walikuwa habari nyingine kila mtu katika wakati wake. Ni jambo zuri kuwa kila mmoja aliutendea haki wakati wake.
Ni kama Lionel Messi leo anavyoutendea haki wakati wake, kama ilivyo kwa Cristiano Ronaldo.
Zimepita zama za Ronaldinho Gaucho na Ricardo Kaka. Pamoja na kutikisa dunia lakini ukweli usiopingika ni kuwa hawakuzitendea haki nyakati zao, maana walidumu kwa kitambo kifupi mno kuliko viwango walivyokuwa navyo.
Wapi Zinedine Zidane ‘Zizzou’ na Ronaldo de Lima? Uliza kuhusu Luis Figo, Rivaldo, David Beckham na Thierry Henry? Je, maveterani Pele, Garrincha, Maradona, Romario, Lothar Matthäus, Marco Van Basten, Roberto Baggio na wengine?
Zilipowadia zama za George Weah, alichomoza kutoka Liberia, taifa lililokuwa na machafuko ya kivita, lisilo na rekodi ya soka, lakini alifika mpaka kileleni, akawa Mchezaji Bora wa Dunia, Mchezaji Bora wa Ulaya na Mchezaji Bora wa Afrika. Tuzo tatu kwa mkupuo mwaka 1995. Usichezee na nyakati!
Golini kabla ya Juma Kaseja, walimtangulia akina Mohamed Mwameja, Idd Pazi ‘Father’, Peter Manyika, Juma Pondamali, Athuman Mambosasa, Omar Mahadhi na wengineo. Ni nyakati!
Zama za Edibily Lunyamila, ungesema nini kwenye soka la Tanzania? Kama ilivyokuwa kwa Zamoyoni Mogella. Zilishakuwepo zama za mashuti ya Said Sued ‘Scud’ na Dua Said. Alitisha James Tungaraza mpaka akaitwa Boli Zozo.
Joseph Kaniki yupo jela Ethiopita, akitumia adhabu ya kunaswa na madawa ya kulevya. Ila nyakati zake alikuwa anafunga magoli popote kutokana na uwezo mkubwa wa kupiga mashuti. Watanzania walimwita Golota.
Na hii ndiyo sababu walishakuwepo akina Sunday Manara ‘Computer’, walipoondoka wakafuata akina Malota Soma, Edward Chumila, Hussein Marsha, na wengine, walipopisha walifuata akina Muso, Mgosi, Tegete, Ngassa na wengine! Ni kupishana kwa nyakati!
Walikuwepo Tupac Shakur na Notorious BIG, wakaimbwa ulimwengu mzima. Hip Hop iliwatazama wao tu! Walifuata akina Nas, Mase, DMX, Ja Rule, Eminem, 50 Cent na wengine! Jay Z anaendelea kucheza na nyakati, watu sasa hawaambiwi kitu kuhusu Kanye West, Lil Wayne, Wiz Khalifa, Kendrick Lamar, Drake na wengine!
Unawezaje kusahau zama za Bow Wow na Lil Romeo, walivyochuana kutengeneza fedha wakiwa watoto? Huwezi bila shaka kusahau vipindi vitamu vya wakubwa, Dre, Snoop Dog, hayati Big Punisher, Fat Joe, Coolio, LL Cool J, Ice Cube, Scarface na wengine.
Huu ni muda wa Justin Bieber, Chris Brown, The Weekend na wengine. Usher Raymond na Timbelake wanarudirudi. Hutasahau kuwa walikuwepo akina Baby Face, Joe Thomas, Lionel Richie na wengine! Yupo wapi Mfalme Michael Jackson?
Kipindi hiki Rihanna akionekana ndiye malkia, unadhani anafikia robo ya makeke ya Jennifer Lopez alipokuwa kwenye kiwango chake? Anafua dafu kwa Britney Spears na Christina Aguilera? Walikuwepo malkia wengine kama Janet Jackson, Whitney Houston, Mariah Carey na wengineo.
Wakati zikijadiliwa stori za nani anaweza sana ‘kuchana’ kati ya Nick Minaj na Iggy Azalea, kabla yao walikuwepo wakali kama Left Eye, Missy Eliot, Da Brat, Lil Kim na wengine.
Adolph Hitler kwa wakati wake alitawala dunia. Saddam Hussein alipokuwa kwenye wakati wake, alishambuliwa na mataifa zaidi ya 10, yakiongozwa na Marekani mwaka 1991 katika Vita ya Ghuba ya Uajemi, lakini hawakumuweza. Mwaka 2003, Marekani na Uingereza peke yake walimng’oa na ikawa sababu ya kukamatwa kisha kunyongwa. Ni kwamba mwaka 2003 hazikuwa zama za Saddam ndiyo maana alipigwa kirahisi.
Zilikuwepo zama za Michael Jordan na Magic Johnson kwenye kikapu, kabla yao walikuwepo akina Larry Bird, Moses Malone na wengine. Baadaye walifuata akina Shaquille O'Neal, Allen Iverson, Tim Duncan, Steve Nash, Kobe Bryant, LeBron James na sasa Stephen Curry ameshavuta kiti na ameketi.
Siasa za nchi kwa sasa zinamtazama Rais John Magufuli lakini kabla yake alikuwepo Jakaya Kikwete, kama alivyotanguliwa na Benjamin Mkapa, Ali Hassan Mwinyi na Baba wa Taifa, Julius Nyerere.
Upinzani leo wanatazamwa Edward Lowassa, Zitto Kabwe, Freeman Mbowe, Tundu Lissu na wengine, kabla yao walitikisa akina Augustino Mrema, Willibroad Slaa, marehemu Christopher Mtikila, Ibrahim Lipumba na wengineo. Ni nyakati!
CHUKUA SOMO
Juhudi huvuta bahati na bahati ndiyo itakufanya ufike kwenye kipindi chako cha mafanikio.
Muongozo ni wewe kujituma na utakapofika kwenye wakati wako, hakikisha unautumia vizuri ili utakapopita, watu waseme “alikuwepo fulani bwana!”
Pambana kwenye eneo lako ili utengeneze wakati wako mzuri. Utakuwa mwenye kupendwa na kuheshimika sana kama utafikia wakati wako na kufanya kile kinachohitajika.
Huu ni wakati wa Mbwana Samatta, kama ilivyo Diamond Platnumz na Ali Kiba. Hongera nyingi kwao.
Ijumaa Kareem.
Ndimi Luqman Maloto
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment