tangazo

tangazo

Sunday, January 3, 2016

Makatibu wakuu wapya wakatende kama walivyoapa

Rais Magufuli, wiki iliyopita alifanya uteuzi wa Makatibu Wakuu wa Wizara za serikali ya awamu ya tano na akawaapisha na pia kuwasainisha Hati ya Maadili na Utumishi wa Umma, nao wakaahidi kwenda katika wizara walizopangiwa na kufanya kazi kulingana na kasi ya Serikali mpya.

Hafla ya kuapishwa makatibu wakuu 26 iliyofanyika mwishoni mwa wiki ikulu jijini Dar es Salaam, ilikuwa ya aina yake kutokana na kuapa mara mbili, huku Rais Magufuli akiwaeleza kuwa asiyeweza kazi aseme waziwazi ili asiape, akae kando.

Walikula kiapo cha kwanza mbele ya Rais Magufuli na kiapo cha pili cha maadili ya viongozi wa umma kiliwahusisha makatibu wakuu pamoja na naibu makatibu wakuu 24, na kufanya idadi ya walioteuliwa na Rais Desemba 30 mwaka jana kuwa 50.

Kiapo cha pili walisaini hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma, inayotolewa na ofisi ya Rais, Sekretariet ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Kiapo hicho ni cha kuahidi kutofanya mambo mbalimbali kama kutotumia cheo kwa maslahi binafsi, kulinda rasilimali za nchi, kutotoa wala kupokea rushwa, kutotoa siri za serikali na kuwa wazalendo.

Makatibu Wakuu ndio watendaji wakuu wa wizara, wamepewa madaraka makubwa ya kuhakikisha kuwa sera za wizara husika zinatekelezwa kwa ufanisi chini ya usimamizi wao, na ndio maana wakati wanaapa kiapo cha pili, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliwataka viongozi watendaji wakuu hao wafanye kazi zao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu kwa maslahi ya nchi.

Tunaamini kuwa Makatibu Wakuu hao, wanajua namna kasi ya utendaji wa Serikali ya awamu ya tano ilivyo, wanafahamu pia Serikali ina mifumo ya karibu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango iliyotolewa, ni dhahiri kuwa wao watakuwa chachu ya kusukuma uwajibikaji kwa wote walio chini ya mamlaka yao.

Kero kubwa za wananchi zimekuwa kukithiri kwa rushwa hasa katika sekta za umma, ambako sehemu kubwa ya huduma ilikuwa ikinunuliwa, watendaji wengi waliamini kuwa bila rushwa kutolewa, huduma ilikuwa ngumu kupatikana, na hasa katika sekta za mahakama, polisi, afya nk.

Baada ya kuapishwa kwa Makatibu Wakuu, WAziri Mkuu aliwaasa na kusema "Serikali imeamua kudhibiti utendaji katika sekta mbalimbali, utendaji unaotakiwa ni ule wa wazi, uadilifu, uaminifu ambao utatoa matokeo tarajiwa kwa wananchi".

Ni kweli kuwa wananchi wengi wameonyesha kuwa na imani na Serikali hii ya Rais Magufuli, na dhamira ya Rais  ni kuweka uongozi unaowajibika, uwe karibu zaidi kwa wananchi, ili huduma muhimu ambao zimekuwa tatizo kwao kwa muda mrefu zipatikane bila urasimu.

Baadhi ya Makatibu Wakuu waliovuta hisia za wanataaluma, walikuwa Meja Jenerali Gaudence Milanzi aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, yeye aliahidi kupambana kwa nguvu zote na tatizo la ujangiri wa wanyama pori nchini, pia Jaji Meja Jenerali Rwegasira wa Wizara ya Mambo ya Ndani aliahidi kupambana na mtandao wa dawa za kulevya nchini ambao alisema kwa muda mrefu umekuwa tishio.

Tunaamini Makatibu Wakuu wote watatekeleza majukumu yao kama walivyoapa, ni wazi kwamba Rais amewateua kwa kuzingatia viwango vya uwajibikaji wao, na kwa hakika atakuwa amejiridhisha kwa ufanisi unaotarajiwa kutoka kwao.

Ni wakati muafaka sasa kwa Serikali kutekeleza yale ambayo yanahusu nafasi za Makatibu Wakuu, kwani hao ndio kiungo kikubwa kwa wananchi, tunaamini sehemu kubwa ya kero ambazo zimewakwaza wananchi kwa kipindi kirefu sasa zitapata ufumbuzi unaostahiki.
chanzo nipashe

No comments:

Post a Comment