Baadhi ya Miwa iliyoteketea kwa moto kutokana na hujuma iliyofanywa na Watu wasiojuilikana huko kwenye mashamba ya Miwa ya Kiwanda cha Sukari Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Meja
Mstaafu Juma Kassim Tindwa.
Meneja wa Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda Bwana Tushar Mehta akimueleza Balozi Seif hasara iliyopatikana kutokana na hujuma ya moto kwenye mashamba ya Miwa Mahonda.
Balozi Seif akielezea masikitiko yake kutokana na baadhi ya
watu kufanya hujuma za makusudi kujaribu kuvuruga juhudi za Uongozi wa Kiwanda
cha Sukari Mahonda za kuimarisha Sekta ya Viwanda.
Tishio la ajira za Wafanyakazi 350 wa Kiwanda cha Sukari
Mahonda zinaendelea kuwa hatarini kufuatia hujuma zinazofanywa kwa makusudi na
baadhi ya watu kuendelea kutia moto mashamba ya miwa huko Mahonda Mkoa wa
Kaskazini Unguja.
Kitendo hicho cha hujuma kinaweza kuusababisha Uongozi wa
Kiwanda cha Sukari Mahonda kuwa na mawazo ya kufikiria kuzuia ajira mpya
450 za Wafanyakazi wa Kiwanda hicho katika malengo yake baada ya kukamilika kwa
matengenezo makubwa na kuanza tena uzalishaji wa sukari.
Meneja wa Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda Bwana
Tushar Mehta alisema hayo wakati akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi aliyefika kuangalia hasara iliyosababishwa na moto
uliotiwa kwa mara nyengine tena na Watu wasiojuilikana ndani ya shamba la
Miwa katika kipindi cha siku Tano baada ya tukio kama hilo la Tarehe 30 mwezi
uliopita.
Bwana Tushar alisema moto huo umetiwa kati kati ya shamba la
Miwa jana jioni na wahalifu wenye dhamira ya makusudi ya kutoa
usumbufu na kizuizi kwa wananchi na vikosi vya Ulinzi katika harakati za
kukabiliana na moto huo. .
Alisema Eka zipatazo 50 za Miwa iliyopevuka imeteketea kwa
moto hali ambayo imeisababishia Kiwanda hicho hasara ya Tani 200 za Sukari na
Lita 2,300 za Spititi zilizokuwa zizalishwe kutokana na miwa hiyo ikiwa na
hasara ya jumla ya dola za Kimarekani Laki 228,758.56 sawa na zaidi ya
shilingi Milioni 494 za Kitanzania.
Meneja huyo wa Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda
alifahamisha kwamba hadi sasa Eka zipatazo 200 zimeteketea kwa moto
kwenye matukio yote mawili katika kipindi cha
siku Tano zilizopita na kusababisha hasara ya jumla ya Dola za Kimarekani
Milioni 1,176,234.28 sawa na shilingi za Kitanzania Bilioni
2,326,818,500/-.
Akiupa pole Uongozi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda kutokana
na hasara ya Mashamba iliyosababishwa na moto huo Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hujuma hiyo ya makusudi
haiitakii neema Zanzibar katika harakati zake za kustawisha uchumi wake.
Balozi Seif aliwanasihi watu wenye tabia hiyo kuachana nayo
kwani mbali ya kujibebesha dhambi lakini pia inawavunja moyo wawekezaji
walioamua kuja kuwekeza miradi yao ya kiuchumi Nchini kwa lengo la
kuisaidia Serikali pamoja na Wananachi hapa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba
juhudi za makusudi za Serikali kuu katika kukifufua tena Kiwanda cha
Sukari na Manukato Mahonda baada ya kusita kwa miaka kadhaa zililenga
kuimarisha Uchumi kupitia sekta ya viwanda sambamba na kupanua soko
la ajira kwa Vijana.
Alisema tabia ya baadhi ya watu kufikiria kwamba hujuma hiyo
itatoa fursa kwao kutumia maeneo ya mashamba ya Miwa kuendeleza Kilimo na
Mifugo inafaa kuachwa mara moja kwa vile mashamba hayo yataendelea kuwa katika
mipango ya Serikali ya kuhudumia Sekta ya Viwanda.
“ Haya ni Mashamba ya Serikali yaliyotengwa maalum kwa
shughuli za harakati za Viwanda. Hivyo ndoto za baadhi ya Watu kufikiria
kwamba hujuma zao zitazaa matunda kwa kufanya wanavyotaka zinapaswa
ziachwe mara moja ”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliufahaisha Uongozi wa
Kiwanda cha Sukari Mahonda kwamba Serikali Kuu inaangalia mpango utakaowezesha
Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kusaidia ulinzi kwenye Mashamba
hayo ili kulinda hujuma zinazoonekana kushamiri siku hadi siku.
Hilo ni tukio la sita la hujuma za moto kwenye mashamba ya
Miwa ya Kiwanda cha Sukari Mahonda tokea kianze tena uzalishaji wa sukari
na Spiriti mapema mwaka uliopita wa 2015.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment