RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ametoa risala ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2016 kwa wananchi
na kueleza kuwa kufuatia takwimu za robo mbili za mwanzo wa mwaka 2015, uchumi
wa Zanzibar umeendelea kuimarika.
Katika risala yake
hiyo kwa wananchi, Dk. Shein alisema kuwa
huduma za jamii zikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, huduma za
afya pamoja na elimu nazo
zimeimarika ikiwa ni pamoja na kupiga
hatua kubwa katika kuimarisha
miundombinu.
Dk. Shein alisema kuwa
ujenzi wa barabara muhimu umemalizika na kuzinduliwa Unguja na Pemba pamoja na
kukiimarisha kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume pamoja na
Kiwanja cha ndege cha Pemba ambacho tayari kimeshatiwa taa za kurukia ndege.
Alisema kuwa hatua
iliyofikiwa katika ujenzi wa viwanja hivyo tayari imepelekea kuwepo kwa
ongezeko kubwa la idadi ya ndege za Kimataifa zinazokuja Zanzibar, jambo ambalo
limepelekea kuimariska kwa sekta ya Utalii na shughuli za biashara.
Dk. Shein alisema kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imefanikiwa kutengenezesha meli
mpya yenye mitambo ya kisasa katika Kampuni ya ‘Daewoo International’ ya
Jamhuri ya Korea ambayo ina utaalamu na uzoefu mkubwa wa kutengeneza meli.
“Nasaha zangu kwenu
nyote wananchi ni kuwa tuithamini na kuienzi meli yetu hiyo... tukumbuke msemo
wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume kuwa
‘kithamini chako mpaka usahau cha mwenzako”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
katika risala hiyo alieleza kuwa katika mwaka 2015 Serikali imefanya juhudi
kubwa katika kuhakikisha dhamira ya kujenga bandari ya Mpiga Duri inaanza
kutekelezwa ambapo ujenzi huo unatarajiwa kuanza wakati wowote katika mwaka
2016.
Dk. Shein alieleza
juhudi zilizochukuliwa katika kusambaza umeme vijijini Unguja na Pemba ikiwa ni
pamoja na kuufikisha umeme huko Kisiwa Panza na Kisiwa cha Makoongwe kwa upande
wa Pemba kwa kuwatumia wataalamu wazalendo.
Kwa upande wa huduma
za afya Dk. Shein alisema kuwa katika mwka 2015 huduma hizo zimeimarishwa kwa
kuongeza kasi ya kusomesha wataalamu, upatikanaji dawa na huduma mbali mbali
pamoja na kuziimarisha hospitali kwa kutekeleza miradi ya ujenzi.
Akieleza kuhusu
kuimariaka kwa sekta ya elimu mnamo mwaka 2015, Dk. Shein alisema kuwa
mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na kuanza na kumalizika kwa
miradi ya ujenzi wa skuli, kuongeza fani za mafunzo katika vyuo vikuu na
taasisi za elimu ya juu sambamba na kutekeleza lengo al kuondoa gharama za
kuchangia elimu maskulini.
“Lengo letu ni
kuifanya elimu ya msingi kuwa bure huku tukiandaa utaratibu ili elimu ya
sekondari nayo iwe bure kama ilivyodhamiriwa na Muasisi wa Mapinduzi yetu ya
mwaka 1964”,alisema Dk. Shein.
Alieleza kuimarika kwa
miradi ya ujenzi wa miji na majengo ya kisasa katika sehemu mbali mbali ili
kuweza kuijenga taswira mpya ya Zanzibar katika kipindi kifupi kijacho. Aidha,
alieleza kukamilika kwa viwanja vya kufurahishia watoto hapa nchini.
Aidha, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi wote kuwa walinzi wa miundombinu
iliyopo na wasichelee kuwafichua wale wote wanayoiharibu na kueleza
kusikitishwa kwake katika mwaka uliomalizika baadhi ya watu waliiharibu
miundombinu hiyo kwa kuweka mbele maslahi yao binafsi na kusahau maslahi ya
wote.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alieleza kuwa Serikali inaendelea kutoa ruzuku kwa huduma za matrekta na
pembejeo za kilimo kwa wakulima ambao kwa msimu wa mwaka 2015/2016 tani 750 za
mbolea na lita 15,000 za dawa ya kuulia magugu zimekwishanunuliwa.
Kwa upande wa zao la
Karafuu Dk. Shein alisema kuwa wakulima wameitikia vyema wito wa Serikali wa
kuuza karafuu zao katika vituo vya ZSTC
ambapo katika msimu wa ununuzi wa karafuu wa mwaka 2015/2016, hadi kufikia
mwezi Novemba, 2015 jumla ya tani 962.7 za karafuu zenye thamani ya Tshs.
Bilioni 13.471 zimenunuliwa katika vituo vya ununuzi wa karafuu vya SSTC Unguja
na Pemba.
Akieleza kuhusu
uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25, Oktoba mwaka 2015 ambapo wananchi wa
Zanzibar walishiriki katika kuwachagua viongozi wao ambapo kwa upande wa
uchaguzi wa viongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliosimamiwa na Tume ya
Taifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umemaliza na CCM kupata ushindi, Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Dk. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa
kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa
kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais.
Aidha, Dk. Shein
alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar Tume ya uchaguzi uliufuta uchaguzi huo
tarehe 28 Oktoba, 2015 baada ya kubainika kutokea kwa kasoro kadhaa kama
zilizvyoelezwa na Tume hiyo.
Dk. Shein alisema kuwa
katika suala zima la hali ya kisiasa ya Zanzibar, iliyojitokeza baada ya kufutwa
kwa uchaguzi Mkuu, viongozi walishauriana kukutana ili kufanya mazungumzo ya
kutafuta suluhu kwa njia ya amani, ili nchi iendelee kuwa na amani, umoja na
mshikamano na hatimae wakakubaliana kuanza mazunguzmo hayo.
Kwa mujibu wa maelezo
ya Dk. Shein katika risala hiyo, mazungumzo hayo yanayowahusisha viongozi sita
yamefikia hatua kubwa na bado yanaendelea na kueleza kuwa taarifa kamili ya
mazungumzo hayo itatolewa mara yatakapokamilika.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuwa tarehe 12 Jamuari 2016
Zanzibar itaadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ambapo kama kawaida, sherehe hizo
zitatanguliwa na matukio mbali mbali ya shughuli za uzinduzi wa miradi ya
maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika matukio
mbali mbali yaliopangwa katika maadhimisho hayo ambapo pia, kushiriki kwao
kwenye sherehe ya maadhimisho hayo ni hatua ya kuyaendeleza malengo ya
Mapinduzi kwa shabaha ile ile waliokuwa nayo waasisi wa Zanzibar.
Dk. Shein pia, alitoa
wito kwa wananchi kuzingatia kanuni za afya kwa kuimarisha usafi na kuzitaka
Baraza la Manispaa na Mabaraza ya Miji kwa Pemba na Halmashauri zote za Wilaya
kuchukua hatua za uzoahji wa taka na kuwataka wananchi wote kushiriki katika
kiisafisha miji na maeneo wanayoishi hapo siku ya Januari 3 mwaka 2016.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliwakumbusha wananchi kuwa kesho tarehe 1 Januari ni siku ya kujitokeza
kufanya mazoezi hivyo wajitokeze kwa
wingi kufanya mazoezi.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
No comments:
Post a Comment