tangazo

tangazo

Monday, January 4, 2016

wana ccm watakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi wa marejeo

Ally Ndota, Zanzibar.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai amewataka wanachama wa Chama hicho kujiandaa na hatimaye kujitokeza kwa wingi katika Uchaguzi  wa marudio, ili kukiletea ushindi wa kishindo chama hicho.
Aidha, amesisitiza haja kwa wanachama wote popote walipo kujitokeza kwa wingi katika kufanikisha maadhimisho ya sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yanayotarajiwa kufanyika Januari 12, mwaka huu, Mjini Unguja.
Ndugu Vuai ameyasema hayo leo hapo Afisi Kuu ya CCM alipokuwa akizungumza katika kikao maalum na Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC Zanzibar kilichojumuisha pia na Makatibu wa CCM wa Mikoa ya Unguja.
Amesema Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kinawataka viongozi, wanachama wa CCM na Jumuiya zake kujipanga kikamilifu na kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marudio na kuwachagua kuanzania Rais, Wajumbe wa baraza la Wawakilishi na Madiwani wakati utakapowadia.
Ametoa wito kwa wana CCM na wananchi wapenda amani na utulivu kuachana na propaganda potofu zinazoenezwa mitaani siku hadi siku na wapinzani zenye lengo la kuwagombanisha viongozi na wafuasi wa CCM na badala yake hawana budi kujishughulisha na mambo ya msingi kwa maslahi ya Chama na Taifa kwa ujumla.
Ameyataja mambo hayo ya msingi kuwa kwanza ni kujiandaa na hatimaye kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi wa marudio mara baada ya kupangwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na pili kushiriki katika maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964.
Chama Cha Mapinduzi ni Chama imara, chenye heshima na kinachotambulika na kuheshimika ndani na nje ya Tanzania, hivyo wanachama wake katu hawatakubali kupokea propaganda potofu zinazopandikizwa na wapinzania kwa ajili ya kutaka kudhoofisha nguvu ya Chama hicho.

Akizungumzia kuhusu suala la CUF kutoshiriki katika sherehe za mwaka Mapinduzi  za mwaka huu kama ilivyodaiwa na Chama hicho hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar alisema kitendo hicho si jambo la ajabu miongoni mwa Jamii  ya Wazanzibari, kwani kwa vipindi tofauti  kadhaa huko nyuma  wamekuwa wakisusia sherehe hizo.

“Miaka  mingi huko nyuma kabla ya kuundwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa (SUK) Viongozi na wafuasi wa Chama hicho (CUF) walikuwa na kawaida sio tu ya kutoshiriki katika sherehe hizo, bali pia waliweza kususia hata vikao halali vya Baraza la Wawakilishi”. Alidai Naibu Katibu Mkuu huyo.

Amesema CUF kwa muda wote tangu kuasisiwa kwake, kimekuwa na kigugumizi kikubwa katika kuyatambua na kuyathamini Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoleta ukombozi wa kweli kwa wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba hali inayowafanya kuishi wakiwa watu huru ndani ya Taifa lao huru na kufaidika na matunda yatokanayo na Mapinduzi hayo.

Mara kadhaa wana CUF hasa viongozi waliomo ndani ya Serikali walidiriki kuwasilisha mawazo yao ya kutaka neno SMZ liondoshwe na lisitumike kabisa katika Serikali ya Zanzibar  mawazo ambayo yaligonga mwamba, hali inayodhihirisha kuwa CUF haitambui sembese kuthamini sherehe hizo na kinachofanyika sasa ni visingizio tu.

Jambo la msingi kwa jamii ya Wazanzibari ni vyema wakaelewa kwamba ndani ya mioyo ya Wana CUF hawayatambui kabisa Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 na mara kadhaa Viongozi wake wamekuwa wakisisika hadharani kupitia majukwaa ya kisiasa wakitaka Zanzibar iwe na Kumbukumbu za Uhuru bandia wa mwaka 1963.

Kwa mantiki hiyo basi, CCM kinawaomba wana CCM na wale wote ambao ni waumini wa kweli wa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 popote walipo nchini, wajitokeze kwa wingi na kushiriki kikamilifu katika sherehe za maadhimisho ya kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar huku wakiwaambia  wana CUF kwamba “wasitafute visingizio kwani hawana chembe ya Imani na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya 1964 na kwamba kushiriki ama kutoshiriki kwao hakuathiri chochote sherehe hizo”.

No comments:

Post a Comment