Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alisema wakati umefika sasa katika kuona Wananchi wanalazimika ipasavyo kutoa
mashirikiano ili kufanikisha ile azma ya Serikali Kuu ya kupambana na biashara
na matumizi ya dawa za kulevya Nchini.
Amesema kukosekana ushirikiano katika kutoa ushahidi
Mahakamani dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na dawa za kulevya ambako
kunawahusu zaidi Wananchi wanaokuwa karibu na wahusika hao inapelekea kufutwa
kwa kesi na hivyo kudumaza juhudi za Serikali katika vita dhidi ya matumizi ya
dawa hizo.
Balozi Seif Ali Iddi almesema hayo baada ya kuweka jiwe la
msingi la ujenzi wa Kituo cha Tiba na marekebisho ya Tabia kwa Vijana wanaoacha
Dawa za kulevya hapo Kidimni Wilaya ya Kati ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho
ya sherehe za kutimia Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 1964.
Alisema suala la Dawa za kulevya hivi sasa limekuwa janga la
Dunia kwa vile ni la muda mrefu na kuathiri watu wengi hasa Vijana. Hivyo
udhibiti wa matumizi yake unahitaji maamuzi magumu ya Serikali pamoja na
ushirikiano wa Kitaifa Kikanda na Dunia kwa ujumla.
Balozi Seif alisema licha ya changamoto zilizopo za
utekelezaji wa sheria na kanuni za udhibiti wa dawa za kulevya katika
kukabiliana na wimbi la uingizaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya
Nchini, lakini Serikali kupitia vyombo vyake vya dola imefanikiwa kuwakamata
wahusika wa biashara hiyo katika kipindi cha mwaka 2015.
Balozi Seif alifahamisha kwamba suala la rushwa limekuwa
likipewa nafasi kubwa kuwa ni miongoni mwa vikwazo vya kupata mafanikio dhidi
ya vita vya dawa za kulevya licha ya juhudi kubwa inayochukuliwa na Serikali
katika kupambana dhambi hiyo ya rushwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwanasihi walioanzisha
nyumba hizo pamoja na Vijana wanaoishi kwenye nyumba hizo kujitahidi
kutoshawishika kurudi nyuma kwa kujiingiza tena katika janga la matumizi ya
dawa za kulevya.
Mapema akitoa Taarifa ya ujenzi wa Kituo hicho Katibu
Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Dr.Omar Dadi Shajak alisema
ujenzi wa kituo hicho unagharimiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
zaidi ya Shilingi Bilioni Nne na Milioni Mia Mbili { 4,200,000,000/- }
hadi kukamilika kwake.
Dr. Shajak alisema Kituo hicho cha aina yake ndani ya ukanda
wa Mwambao wa Afrika Mashariki kitakuwa na uwezo wa kuhudumia Vijana wapato 200
wake kwa waume kwa wakati mmoja ambapo pamoja na mambo mengine kutakuwa na
mafunzo ya kazi za amali, michezo na huduma nyengine za kurekebisha tabia.
Dr. Omar Dadi Shajak alifahamisha kwamba Ofisi ya Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika kukabiliana na wimbi la uingizaji, uuzaji
na matumizi ya dawa za kulevya tayari imeshaandaa zawadi kwa Mtu au Kikundi
kitakachojitolea kutoa Taarifa ya kukamatwa kwa wahusika wa dawa za kulevya.
Ujenzi wa Kituo cha Tiba na marekebisho ya Tabia kwa Vijana
wanaoacha Dawa za kulevya hapo Kidimni Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja
chenye eneo la ukubwa wa Eka Tatu kinajengwa na Kampuni ya Kizalendo ya
Al – Hilal General Trading Cooperation Limited chini ya Mkandarasi Mbwana
Bakari Juma kutoka Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment