tangazo

tangazo

Wednesday, December 25, 2013

WANANCHI HAWANA BUDI KUJIVUNIA MAENDELEO MAKUBWA YALIYOPATIKANA KATIKA SEKTA YA ELIMU ZANZIBAR.


ZANZIBAR

RAIS WA ZANZIBAR AMBAYE PIA NI  MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI DK. ALI MOHAMED SHEIN AMESEMA, WAKATI HUU ZANZIBAR IKIADHIMISHA MIAKA 50 YA MAPINDUZI, WANANCHI HAWANA BUDI KUJIVUNIA MAENDELEO MAKUBWA YALIYOPATIKANA KATIKA SEKTA YA ELIMU NCHINI.

AMESEMA MIAKA 50 YA MAPINDUZI IMESHUHUDIA MABADILIKO MAKUBWA KATIKA SEKTA YA ELIMU NCHINI IKIWA NI UTEKELEZAJI WA MOJA YA LENGO LA MAPINDUZI HAYO YA KUTOA ELIMU KWA KILA MWANANCHI BILA MALIPO WALA UBAGUZI.

DK. SHEIN AMESEMA HAYO JANA KATIKA SHEREHE ZA UFUNGUZI WA SKULI YA SEKONDARI CHASASA NA SKULI YA SEKONDARI YA WANAWAKE YA UTAANI HUKO WILAYA YA WETE MKOA WA KASKAZINI PEMBA IKIWA NI SEHEMU YA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA MAPINDUZI YA MWAKA 1964.

ALISEMA VIKWAZO VYA ELIMU KABLA YA MAPINDUZI HAIKUWA ADA YA SKULI PEKEE LAKINI HATA FURSA ZENYEWE HAZIKUWEPO KWA WATOTO WA FAMILIA MASIKINI KWANI MTU ANGEWEZA KUPATA ADA LAKINI AKASHINDWA KUPATA NAFASI KWA KUWA TU NI KUTOKA FAMILIA YA KINYONGE.

MADHILA YA AINA HIYO YALIYOKUWA WAKIFANYIWA WANANCHI MASIKINI WA ZANZIBAR ALIELEZA DK. SHEIN NDIO YALIYOKIFANYA CHAMA CHA AFRO SHIRAZI KUSIMAMA KIDETE KUTETEA HAKI ZA WANYONGE NA TARATIBU ZA KIDEMOKRASIA ZILIPOSHINDIKANA NDIO CHAMA HICHO CHINI YA UONGOZI THABITI WA MZEE ABEID AMANI KARUME KILIFANYA MAPINDUZI TAREHE 12 JANUARI, 1964.

ALIWAELEZA WALIMU, WANAFUNZI NA WANANCHI WALIOHUDHURIA SHEREHE HIZO KUWA AZMA YA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR TANGU WAKATI HUO NI KUWAPATIA ELIMU WATOTO WOTE HADI KIKOMO CHA UWEZO WAO NA NDIO MAANA KILA WAKATI IMEKUWA IKIONGEZA FURSA ZA ELIMU NCHINI.

DK. SHEIN ALIWAELEZA WANANCHI HAO KUWA ANAJIVUNIA MRADI HUO MKUBWA WA ELIMU ULIOJUMUISHA SKULI 19 IKIWA NI SEHEMU YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI WA CCM KUKAMILIKA KABLA YA MUDA ULIOPANGWA WA MIAKA MITANO.

“NILIPOKUWA NIKINADI ILANI YA CHAMA CHANGU NA KUAHIDI KUJENGA SKULI 19 ZA SEKONDARI WAPO WALIOGUNA WAKIDHANI HATUTAWEZA, WENGINE WAKASEMA TUSUBIRI TUONE NA WAKO WALIOSEMA HATUWEZI KABISA LAKINI WANACCM WALIAMINI” DK. SHEIN ALIWAKUMBUSHA WANANCHI HAO NA KUWATAKA WAJIVUNIE MAENDELEO HAYO.

KATIKA MNASABA HUO ALISISITIZA KUWA NDIO MAANA SERIKALI IMEKUWA IKIIMARISHA MAZINGIRA YA UTOAJI ELIMU NCHINI IKIWEMO UIMARISHAJI WA MASLAHI YA WALIMU KAMA ILIVYO KWA WATUMISHI WENGINE WA SERIKALI.

“WITO WANGU FANYENI KAZI KWA BIDII SERIKALI INAELEWA MATATIZO YETU, TUTAWAFANYIA KAMA TULIVYOWAFANYIA WATUMISHI WENGINE. MUUNDO WENU YA UTUMISHI UMEKAMILIKA NA SISI TUNAUFANYIA KAZI” DK. SHEIN ALIAHIDI NA KUSISITIZA KUWA MILANGO IWAZI KWA WALIMU KAMA WATAKUWA NA MASUALA YA KUZUNGUMZA NA SERIKALI.

KUHUSU CHANGAMOTO ZINAZOZIKABILI SKULI HIZO DK. SHEIN ALISEMA UZIO WA SKULI UTAJENGWA NA WIZARA YA ELIMU KAMA ALIVYOAGIZA KUJENGWA KWA UZIO WA SKULI YA LUMUMBA UNGUJA AMBAYO NAYO INAKABILIWA NA MATATIZO KAMA HAYO.

KUHUSU HUDUMA KATIKA DHAKHALIA DK. SHEIN ALIELEZA KUWA TAYARI AMEIAGIZA WIZARA YA ELIMU KUIMARISHA UTOAJI WA HUDUMA KATIKA DAKHALIA ZA SKULI ZOTE NCHINI NA KUSISITIZA KUWA SERIKALI “INATAKA DHAKHALIA ZENYE TIJA HAITAKI DAKHALIA ZENYE MATATIZO”.

AKISALIMIA WANAJUMUIYA YA SKULI HIZO MKE WA RAIS WA ZANZIBAR MAMA MWANAMWEMA SHEIN ALIWATAKA WASICHANA KUONYESHA UWEZO WAO KATIKA MASOMO KUENZI UAMUZI WA SERIKALI WA KUIREJESHA TENA SKULI HIYO KUWA YA WANAWAKE PEKEE.

MAMA SHEIN AMBAYE ALISOMA KATIKA SKULI HIYO WAKATI HUO IKIWA YA WASICHANA PEKEE ALISEMA WASICHANA WANA UWEZO MKUBWA KATIKA MASOMO HIVYO HAWANA BUDI KUITUMIA FURSA HIYO KWA KUFANYA VIZURI KATIKA MASOMO YAO ILI SKULI HIYO IWEZE KUTOA WATAALAMU WAZURI WA SAYANSI NA PIA VIONGOZI WA BAADAE.

WAKATI HUO HUO WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI ALI JUMA SHAMHUNA AMEWAPA CHANGAMOTO WALIMU NA WANAFUNZI WA SKULI ZA UTAANI NA CHASASA KUONGEZA BIDIII ILI KUONGEZA KIWANGO CHA UFAULU ZA SKULI HIZO.

ALIWAAMBIA WALIMU NA WANAFUNZI WALIOHUDHURIA HAFLA HIYO KUWA NI LAZIMA LENGO LIWE NI KUPATA MADARAJA YA JUU KUANZIA LA KWANZA HADI LA TATU KWA KUWA HIVI SASA MAZINGIRA YA SKULI ZAO YAMEIMARISHWA ZAIDI.

KUHUSU KUIREJESHA SKULI YA UTAANI KUWA YA WANAWAKE PEKEE WAZIRI SHAMUHUNA ALIELEZA KUWA UAMUZI HUO ULIFANYWA MWAKA 2006 AMBAO ILIAMULIWA SKULI ZA UTAANI NA BENBELLA UNGUJA ZIREJESHWE KUWA ZA WASICHANA PEKEE.

AWALI AKITOA MAELEZO KUHUSU UJENZI SKULI YA CHASASA NA UKARABATI WA SKULI UTAANI NAIBU KATIBU MKUU WA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI ABDULLA MZEE ALISEMA SKULI HIZO NI SEHEMU YA UTEKELEZAJI WA MRADI WA KUIMARISHA ELIMU YA LAZIMA (ZANZIBAR BASIC EDUCATION IMPROVEMENT PROJECT) ULIOANZA JULAI 2007 NA KUMALIZIKA MWEZI NOVEMBA MWAKA HUU.

MRADI HUO ALISEMA UNAJUMUISHA UJENZI WA SKULI MPYA 21 IKIWEMO UKARABATI MKUBWA WA SKULI 6 ZA SEKONDARI, KUJENGA KAMPASI MPYA YA CHUO CHA UALIMU CHA BENJAMIN MKAPA, KUZIPATIA VIFAA SKULI HIZO IKIWEMO MAABARA NA VITABU NA KUWAPATIA MAFUNZO WALIMU WA MASOMO YA SAYANSI NA HISABATI.

ALIFAFANUA KUWA MRADI HUO UMEGHARIMU JUMLA YA DOLA ZA KIMAREKANI MILIONI 48 AMBAPO KATI YA HIZO DOLA MILIONI 42 ZIKIWA NI MKOPO KUTOKA BENKI YA DUNIA NA DOLA MILIONI 6 ZIKIWA FEDHA KUTOKA SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR.

MRADI HUO AMBAO ALISEMA NDIO MKUBWA KABISA WA ELIMU KUTEKELEZWA NCHINI UMEFANYIKA KWA MAFANIKIO MAKUBWA KINYUME NA WASIWASI WALIOKUWA NAO BENKI YA DUNIA.

MAPEMA ILIELEZWA KUWA SKULI HIZO ZINAKABILIWA NA CHANGAMOTO KADHAA ZIKIWEMO UHABA WA WALIMU WA MASOMO YA SAYANSI NA UHARIBIFU WA MAJENGO NA MAZINGIRA YA SKULI KUTOKANA NA SKULI KUKOSA UZIO.

“KUKOSEKANA KWA UZIO KUNAFANYA MAGARI YAKIWEMO YA MIZIGO KUPITA, MIFUGO KUZURURA KATIKA MAENEO YA SKULI PAMOJA NA WATU KUKITUMIA KIWANJA CHA MICHEZO KUCHEZA MPIRA NA KUHARIBU MAJENGO YA SKULI” ILIELEZA SEHEMU YA RISALA YA SKULI HIZO ILIYOSOMWA NA MWALIMU MKUU MSAIDIZI WA SKULI YA UTANI A BI. ZAINA OMAR OTHMAN.

No comments:

Post a Comment