Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema (Bawacha), Zanzibar limesema halijaridhishwa na mwenendo mzima wa uteuzi wa ubunge wa viti maalum kwa upande wa Zanzibar.
Makamu mwenyekiti wa baraza hilo, Hamida Abdallah, alisema licha ya tamko la Kaimu katibu mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, kwamba wabunge hao wamepangwa kwa mikoa, ikiwemo mkoa wa Unguja na Pemba, lakini Baraza hilo limepinga kauli hiyo kwa kueleza kuwa Zanzibar ni nchi sio mkoa.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho, mjini Unguja.
“Sisi Zanzibar sio mkoa ni nchi inayotambulika kisheria, sasa inakuaje wanatoa nafasi mbili moja Unguja na moja Pemba?” Alihoji.
Alisema Katiba ya Chadema inatambua kuwepo kwa kamati maalum ya chama Zanzibar ambayo inatakiwa kushauri kamati kuu kabla ya uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama kwa mujibu wa ibara ya 7.7.19 na ibara ya 7.7.21.
Alisema katiba na kanuni za chama hicho zimekiukwa kwenye uteuzi wa nafasi hizo licha ya wanawake wa Zanzibar kupitia chama hicho kwa kushirikiana na wanawake wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha mgombea wao wa urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, anapata kura nyingi Zanzibar na kumshinda mgombea wa CCM.
Baraza hilo lilitishia kuwa endapo suala hilo halijapatiwa ufumbuzi, watashusha bendera zote za Chadema Zanzibar na wapo tayari wanawake wote Zanzibar wa chama hicho kuitaka Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini kukiangalia upya Chadema kama kinatekeleza kazi zake kwa mujibu wa Katiba hasa masuala ya Zanzibar.
“Hatuna imani na viongozi wote, jitihada zote tulizozichukua za kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais mpaka wanawake wengine wa Chadema wamehasimiana na waume zao kutokana na kuiunga mkono Ukawa leo hii wametubagua na kutufanya Zanziar ni mkoa,”alisema Hamada.
Alisema kuwa Bawacha Zanzibar haioni uteuzi wa wabunge wa Viti Maalum, ambao wamepewa zawadi hiyo bila ya kufuata Katiba na uteuzi huo umefanyika kibinafsi.
Aidha, alisema walitarajia kwa kuwa Zanzibar ina mikoa mitano wangepata viti vitano vya ubunge wa Viti Maalum.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment