tangazo

tangazo

Friday, November 20, 2015

MAJALIWA NA UTEUZI WA KUSHTUKIZWA

Waziri Mkuu Mteule, Majaliwa Kassim Majaliwa, amesema kuwa hakuna na taarifa za uteuzi wake hadi aliposikia na kuona kwenye luninga na kulazimika kwenda bungeni.

Akizungumza wakati wa kuwashukuru wabunge katika ukumbi wa Bunge jana mjini Dodoma, Majaliwa alisema nafasi hiyo hakuitegemea, lakini ameipokea na yupo tayari kufanya kazi.

“Sikuwa na maandalizi yoyote, hata karatasi niliyonayo sijaandika chochote, lakini imeniongoza kutambua uwepo wenu na mchango mkubwa, nawahakikishia kuwa jukumu nililopewa na ambalo nitapewa, kama mwakilishi wa wananchi, nitashirikiana nanyi katika kufanya kazi zetu,” alisema.

Aidha, alimshukuru Mungu na Rais kwa kumteua pamoja na wabunge kumthibitisha kwa kura nyingi kushika nafasi hiyo.

“Mheshimiwa Spika, nilikuona nikiwa naangalia kwa njia ya televisheni ulipokuwa unaendesha zoezi la ufunguzi wa bahasha zote tatu...nawashukuru wabunge wote kwa kuridhia, kupiga kura nyingi jina langu, tuweze kufanya kazi kwa pamoja ya kuwatumikia Watanzania.”

Majaliwa aliahidi ushirikiano wa hali ya juu bila kujali vyama kwa kuwa ni wawakilishi wa wananchi wa Tanzania na watafanya kazi kwa pamoja ya ufuatilia wa shughuli za maendeleo na kuisimamia serikali ikiwa ni pamoja na kusikikiza ushauri wa wabunge katika kufanyakazi za kila siku.

KUANZA KAZI KARIBUNI
Majaliwa alisema baada ya kuapishwa atafanya ziara katika majimbo mbalimbali ili kuona changamoto zilizopo, maendeleo waliyofikiwa na kuwasikia Watanzania wana mawazo gani.


HALI ILIVYOKUWA BUNGENI
Majaliwa aliingia bungeni huku wabunge wa CCM wakipiga makofi hadi alipokaa kwenye kiti cha nyuma kabisa.
Kabla ya kushukuru, baada ya kupigiwa kura za kuthibitishwa, alisalimiana na wabunge wa CCM na Upinzani na kwenda moja kwa moja kuwashukuru.

ATHIBITISHWA KURA 73.5%
Awali akisoma matokeo ya uthibitisho huo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, alisema Majaliwa alipata kura za ndiyo 258 (asilimia 73.5), kura 91 za hapana (asilimia 25.9) na kura mbili ziliharibika. Baada ya kuthibitishwa kwa kura hizo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimkaribisha Majaliwa atoe shukrani kwa wabunge.

Majaliwa katika hotuba yake fupi, alimshukuru Rais John Magufuli kwa imani aliyoionyesha mwake na kuwashukuru wabunge kwa kumthibitisha.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment