Ni wazi kwamba Rais Dk. John Magufuli ameanza majukumu yake kwa kasi kwa lengo la kuongeza uwajibikaji na kuongeza tija kwa taifa kwa kutembelea Wizara Fedha na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambako kote alishuhudia madudu.
Itakumbukwa kwamba Dk.Magufuli alitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa mshindi wa nafasi hiyo kati ya wagombea nane wa nafasi ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na baada ya kutangazwa aliapishwa katika tukio la halaiki Novemba 5 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo baadhi ya watu, viongozi wa vyama, wanachama na mashabiki wameibuka na kukosoa waziwazi uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu na kumuweka madarakani Dk.Magufuli, wabunge na madiwani kwa maelezo kuwa baadhi ya maeneo uchaguzi huo ulikuwa na dosari mbalimbali, huku wakitaka tume huru ya uchaguzi.
Mkoani Kagera baadhi ya wananchi wanataja kasoro hizo kuwa ni baadhi ya vitabu kunyofolewa kwa karatasi za kupigia kura, kutokuwapo majina ya wapiga kura halali kwenye orodha ya wapiga kura, baadhi ya vituo kutofunguliwa kwa wakati, vifaa kutofika kwa wakati na wasimamizi kuchelewa kutangaza matokeo.
Sued Juma mkazi wa Hamgembe, manispaa ya Bukoba anasema kuwa kutokana na kasoro hizo wananchi wengi hawakupiga kura baada ya kukata tamaa. Kuhusu matokeo kuchelewa kutangazwa anadai kuwa chanzo ni udhaifu wa NEC, wasimamizi na wasimamizi wasaidizi katika Halmashauri za Wilaya na Manispaa.
“Katika baadhi ya maeneo ilionekana waziwazi kwamba washindi walishajulikana kabla hata ya kupiga kura, hii inakatisha sana tamaa. Inakuwaje wananchi tulipoteza muda kujiandikisha BVR, tukahakiki majina yetu lakini siku ya kupiga kura jina lako halionekani hasa waliobainika kuwa ni wanachama wa chama fulani cha siasa,”alisema.
Kwamba mfumo wa upatikanaji wa viongozi wa tume husika siyo huru, unalinda upande mwingine kisiasa na kwa hiyo siyo rahisi haki kwa upande mwingine kutendeka hasa wakati wa kutangaza matokeo, anasema Juma.
Anasema vyama vya siasa vya upinzani, wanaharakati na baadhi ya wananchi wasiokuwa na vyama wamekuwa wakitaka mabadiliko ya mfumo wa upatikanaji wa viongozi wa tume ya taifa ya uchaguzi wakipinga mfumo wa uteuzi wa viongozi hao na kutaka ubatilishwe lakini suala hilo halitiliwi maanani kwasababu ni mkakati wa kutetea upande mmoja.
“Hoja za kutaka mabadiliko hayo zipo kwenye msingi kwamba Mwenyekiti wa Tume huteuliwa na rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa chama tawala (Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kutokana na mazingira hayo anasema siyo rahisi kuwapo kwa uwazi wakati wa kutangaza matokeo ambapo kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi hutangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ambaye huteuliwa na Mwenyekiti wa chama tawala (rais).
Hivyo inapojitokeza chama tawala kushindwa, wasiwasi hujitokeza kwa upande wa vyama vingine (mfano upinzani) kuwa Mwenyekiti wa tume huweza kupindisha matokeo ili kumridhisha au kulinda heshima ya Mwenyekiti wa chama tawala aliyemteua kwa nafasi hiyo.
Kimsingi madai ya tume huru ya uchaguzi ni jambo mtambuka, haki ambayo imekuwa ikidaiwa katika nchi nyingine pia hasa za maziwa makuu, anasema.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 12 (1) inasema binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa, ingawa wanawake wengi mkoani humo hawakuweza kupiga kura kutokana na kutozijua haki zao za kikatiba.
Nasra Jamada mkazi wa Kibeta katika manispaa hiyo, anasema kundi la wanawake wengi hawakuweza kupiga kura kutokana na hofu ya vitisho na tofauti za kiitikadi na wenzi wao.
Anasema pamoja na kuhakikishiwa ulinzi, wanawake wengi hawakuweza kupiga kura kwa kuwa maeneo mengi hayakuwa na ulinzi wa kutosha licha ya hatarishi kwa kundi hilo wanapokwenda kupiga kura, mfumo dume kutokana na baadhi ya wanaume kuficha kadi za kupigia kura za wanawake zao kwa kutofautiana kiitikadi.
“Mimi sikupiga kura, mume wangu alificha kadi yangu, hata nilipomdai hakunipatia licha ya kunijibu kwa jeuri,”alisema.
Justus Rutabingwa ni mfanyabiashara katika manispaa ya Bukoba ambaye aligombea nafasi ya udiwani katika kata Rwamishenye kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anasema kuwa uchaguzi huo ulijaa hujuma, wizi na rushwa, na kutoa mfano wa maeneo ya kupigia kura kuwa kwenye mazingira yaliyojificha zaidi na kusababisha mpiga kura kutoonekana.
Rutabingwa anasema pia baadhi ya vitabu vya karatasi za kupigia kura vilivyofolewa karatasi huku na kupunguza idadi ya karatasi halali kwenye kitabu husika na kudai kuwa baadhi ya wasimamizi wa vituo waliwapendelea wapiga kura walioawatambua hasa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Karatasi za kupigia kura ziliisha mara mbili katika baadhi ya vituo na kusababisha kuagizwa nyingine ambazo zililetwa muda ukiwa umeenda mno, jambo lililochangia baadhi ya wapiga kura kukata tamaa na kurudi nyumbani bila kupiga kura,”alisisitiza.
Rutambingwa ambaye alishindwa kwenye uchaguzi huo anaitaka NEC kukomesha vitendo vya hujuma ikiwamo tabia ya baadhi ya wasimamizi kupendelea wagombea wengine huku wakijua kuwa si chaguo la wananchi na kufananisha kitendo hicho na wizi.
Naye mgombea kiti cha ubunge katika jimbo la Nkenge kupitia Chadema ambaye pia alishindwa, Valelian Rugalabamu, anasema kuwa uchaguzi katika jimbo hilo haukuwa wa haki kwa maelezo kuwa ulitawaliwa na vitisho na kusababisha baadhi ya wapiga kura kutojitokeza kupiga kura kwa kuhofia usalama wao.
Anasema kuwa pia suala la wagombea wengi wa nafasi za udiwani hasa wa vyama vya upinzani kuwekewa pingamizi na tume kushindwa kuzipatia ufumbuzi, lilivuruga uchaguzi katika jimbo hilo.
Baadhi ya mawakala wa vyama vya upinzani hawakuruhusiwa kukagua masanduku ya kupigia kura huku wasimamizi wa uchaguzi wa vituo waliwakatalia mawakala kusaini fomu namba 14 na16 za malalamiko.
Akijibu baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika jimbo lake, msimamizi wa uchaguzi katika jimbo la Bukoba mjini Aron Kagurumjuli, anasema baadhi ya kasoro zilitokana mvua na kusababisha baadhi ya magari yaliyokuwa yamebeba vifaa hivyo kukwama.
Anakiri kupokea malalamiko ya baadhi ya vitabu kunyofolewa karatasi za kupigia kura na kusema uchunguzi unaendelea kubaini maeneo ambayo dosari hizo zilijitokeza na chanzo cha mapungufu hayo.
“Kila msimamizi alikabidhiwa vifaa vilivyokamilika, kama kuna mapungufu hayo siwezi kutoa majibu hadi uchunguzi ufanyike," alisema.
Kuhusu kura zilizotelekezwa zikiwa tayari zimepigwa katika kituo cha shule ya sekondari Kahororo, msimamizi huyo anasema kuwa pia hawezi kulitolea majibu haraka, kwa madai kuwa ni suala linalohitaji kufanyiwa uchunguzi, ili kubaini kura hizo zilifikaje kwa wahusika.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa sababu zilizosababisha matokeo kuchelewa kutangazwa na kusababisha baadhi ya wananchi waliokuwa wamekusanyika karibu na ofisi za msimamizi wa uchaguzi kuanza kuharibu mali wakishinikiza matokeo yatangazwe, anasema hakuna sheria inayawaruhusu kuharibu mali kwa madai ya kucheleweshwa kwa matokeo.
“Kilichotokea ni wananchi kukosa subira, mbona maeneo mengine walichelewa zaidi yetu kutangaza matokeo lakini hawakufanya fujo,” anahoji Kagurumjuli.
Baadhi ya mali zilizoharibiwa ni jengo la CCM mkoa wa Kagera na jengo la kituo cha redio inayomilikiwa na aliyekuwa mgombea ubunge katika jimbo la Bukoba mjini kupitia CCM, balozi Khamis Kagasheki ambayo vioo vya madirisha yake vilipasuliwa kwa mawe.
Katibu wa CCM mkoa wa Kagera, Idd Ame alidai kuwa uharibifu huo umefanywa na wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa kwa madai ya matokeo kuchelewa kutangazwa.
Kwa upande wake Balozi Khamis Kagasheki ambaye alishindwa kutetea jimbo hilo katika uchaguzi huo uliompatia ushindi Wilfred Rwatakare wa Chadema, analaani kitendo cha mali zake kuharibiwa kwa kisingizio cha matokeo kucheleweshwa kwa kuwa yeye siyo chanzo cha ucheleweshwaji huo.
“Ushindi usisabishe watu kufanya vurugu, nimewaomba viongozi wa Chadema kuzungumza na wafuasi wao maana baada ya uchaguzi wafahamu kuwa kuna maisha yanaendelea, ambayo inabidi tuishi kwa kushirikiana,” anasema.
Mwenyekiti wa Chadema wilayani Bukoba, Victor Sherejey alipinga Chadema kuwa chanzo cha vurugu na uharibifu huo na kudai kuwa pia wanachama wa CCM, wananchi wengine walikuwamo wakati fujo hizo zikitokea.
“Hawakuwa wanachama wa Chadema au vyama vingine vinavyounda Ukawa, bali walikuwamo wana CCM, na wananchi wengi wa Bukoba mjini waliofika ili kutangaziwa kiongozi wao waliyemchagua, mimi nilikuwa ndani ya ofisi za Halmashauri, labda kama uharibifu huo umetokea ndani ya ofisi hizo, basi tushtakiwe, ” anasema Sherejey.
Katika mkoa wa Kagera watu walioandikishwa kupiga kura walikuwa 1,039,268. Kufuatia uchaguzi mkuu huo, CCM ilinyakua majimbo manane kati ya tisa, huku Chadema wakipata jimbo moja tu la Bukoba mjini.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment