tangazo

tangazo

Sunday, November 15, 2015

UTATA WA MAWAZIRI WA DK SHEIN HUU HAPA

Wakati hali ya kisiasa visiwani Zanzibar ikiendelea kuwa tete kutokana na kufutwa kwa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, utata kuhusiana na uhalali wa mawaziri wanaounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) chini ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein umeibuka na kuendelea kuibua mijadala.

Akizungumza mjini Zanzibar jana, Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Awadh Said, alisema kutokuwapo kwa Baraza la Wawakilishi katika kipindi hiki kilichozidi siku tisini tangu kuvunjwa kwa Baraza hilo kunaondoa uhalali wa kuwapo kwa mawaziri ambao kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, sifa yao kuu ni lazima watokane na Baraza la Wawakilishi.

Awadh alisema kinachofanyika sasa ni kuendeshwa serikali bila ya kuwapo kwa muhimili mmoja wa dola ambao ni huo wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, na kufanya hivyo ni kukiuka kifungu cha 5A (1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Alisema katiba ya Zanzibar imeweka mgawanyo wa madaraka kati ya mamlaka tatu, ambazo ni mamlaka ya utendaji, mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma na mamlaka ya utekelezaji wa utoaji haki.

“Mamlaka ya utendaji ni Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za Umma ni Baraza la Wawakilishi na mamlaka ya utekelezaji wa utoaji wa haki ni Mahakama,” alisema Awadh, akigusia kifungu cha 5A(2) cha katiba ya Zanzibar.

“Ukifuta uchaguzi unakuwa umevuruga na kuporomosha mihimili na (bahati mbaya) mifumo ya katiba yetu haikutoa mwanya wa kuwapo hali hiyo,” alisema Awadh ambaye pia ni wakili katika Mahakama Kuu ya Zanzibar na Kamishina wa iliyokuwa Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kwamba kimsingi, suala la utawala limeondoka kutokana na mhimili mmoja unaotajwa na katiba kuwa haupo wakati mfumo wa serikali za mabunge, mawaziri hutoka ndani ya Baraza la Wawakilishi chini ya Kifungu cha 43(2) cha Katiba ya Zanzibar kinachosomeka kuwa: ‘Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi watateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi’.

“Kama Baraza halipo utasemaje Serikali ipo kihalali? Huwezi kuwa waziri bila ya kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi. Ukisema Waziri ana sifa basi na Mwakilishi ana sifa na aendelee kulipwa mshahara wakati Baraza limevunjwa Agosti 13 mwaka huu,”alisema Awadh.

Akieleza zaidi, Awadh alisema Rais wa Zanzibar anaendesha Serikali ya Awamu ya Saba bila ya kuwa na ushiriki wa wananchi kupitia Baraza la Wawakilishi (BLW), kitendo ambacho ni kinyume cha kifungu cha 21 (1) cha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.

Alisema kifungu hicho kimesisitiza kuwa: “Kila Mzanzibari anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi , ama moja kwa moja au kwa kupitia Wawakilishi waliochaguliwa kwa hiari,”alisema akinukuu kifungu cha 21(1) cha katiba ya Zanzibar.

Alisema kwa mujibu wa Katiba, Zanzibar haina chombo cha kusimamia serikali wala kumdhibiti Rais kutokana na kukwama kuundwa kwa Baraza la Wawakilishi kufuatia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.

Mawaziri wanaotoka Chama cha Wananchi (CUF) walitangaza hivi akribuni kuwa wameshaachia ngazi na kukabidhi ofisi na magari kwa maelezo kuwa wanaheshimu katiba kwani serikali iliyopo imepoteza sifa, madai yaliyopingwa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, aliyesema kinachofahamika mawaziri bado wanashikilia nafasi zao kwani katiba inampa mamlaka rais kuendelea kuongoza hadi rais mteule atakapokula kiapo.

SPIKA BARAZA LA WAWAKILISHI ANENA
Akizungumzia hali iliyopo sasa, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, alisema ataendelea kuwa Spika asiyekuwa na wajumbe baada ya ZEC, kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu na kusababisha Baraza la Wawakilishi lishindwe kupatikana kwa wakati kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.

Akizungumza mjini Zanzibar jana, Spika Kificho alisema kifungu cha 90(1) cha Katiba ya Zanzibar kinaeleza wazi kuwa: “Wakati Baraza litakapovunjwa, uchaguzi mkuu wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi utafanywa na mkutano mwanzo wa Baraza jipya utafanywa si zaidi ya siku tisini (90) tokea kuvunjwa kwa baraza hilo.

Kificho alikiri kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya katiba, mkutano wa kwanza ulitakiwa kufanyika Novemba 12, 2015, ikiwa ni kwa kuzingatia kipindi hicho kilichoainishwa tangu kuvunjwa kwa Baraza la Wawakilishi.

Hata hivyo, jambo hilo limeshindikana kutokana na chombo hicho kutokuwa na Wawakilishi wapya baada ya ZEC kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

Alisema katika mazingira kama hayo, yeye na naibu wake, Ali Abdalla Ali,  wataendelea kubakia katika nyadhifa zao hadi Uchaguzi Mkuu wa marudio utakapofanyika baada ya ZEC kutangaza tarehe ya kufanyika uchaguzi huo.

“Wenyeviti wa Kamati muda wao umemalizika kama Wawakilishi baada ya Baraza kuvunjwa Agosti 13 mwaka huu,” alisema Kificho.

Hata hivyo, alisema ataendelea kushika wadhifa wake na Naibu wake Ali Abdalla Ali mpaka Spika mpya atakapopatikana baada ya kufanyika uchaguzi mkuu katika siku za baadaye.

Alisema serikali itaendelea kuwapo na Rais ataendelea kubaki madarakani pia, kwa mujibu wa katiba Katiba ya Zanzibar Kifungu cha 28(1), kinachosema rais ataendelea kuwa rais mpaka pale rais anayefuata atakapokula kiapo cha kuwa Rais wa Zanzibar.

Aidha, alisema katiba inampa rais uwezo wa kuitisha Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) ambalo limemaliza muda wake na kuvunjwa kama kutatokea mazingira ya hali ya hatari yakiwamo ya vita katika eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 “Kilichojitokeza ni kitu kipya na hakuna sehemu ilipozingatiwa kuwa inapotokea mazingira kama hayo nini kifanyike… ni mambo ya kuangaliwa katika siku za baadaye pindi hali kama hiyo inapotokea,” alisema Kificho.

Aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hamid Mbwezereni, alisema kama kuna wanasheria wanalalamika kuwa katiba imevunjwa, ni vyema wakaenda mahakamani kwani hicho ndiyo chombo pekee chenye uwezo wa Kikatiba wa kutafasiri Katiba na siyo wanasiasa au wanaharakati, kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar.

Alisema kila mwanasheria anafahamu njia ya kutafuta haki lakini bahati mbaya ni kwamba, wanasheria wa Zanzibar wanaishia kulalamika nje ya utaratibu wa utafutaji haki kisheria.

Alisema kwa mtazamo wake, anaamini Jecha alikuwa sahihi kwani amefuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu kutokana na mamlaka aliyonayo, kwa mujibu wa kifungu cha 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 na Sheria ya uchaguzi namba 11 ya Mwaka 1984.

“Kama kuna watu wanatia shaka kwa maamuzi ya mwenyekiti wa tume, mahakama pekee ndiyo mwamuzi,” alisema Mbwezeren.

Kwa mujibu wa katiba, mkutano wa kwanza wa Baraza la Wawakilishi ulitakiwa kuitishwa ndani ya siku tisini tangu kuvunjwa Baraza Agosti 13, yaani walau Novemba 12, lakini imeshindikana kutokana na kukosekana Wajumbe wateule wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Tayari ZEC imetoa tangazo rasmi katika gazeti la Serikali juu ya kufutwa kwa uchaguzi huo na kuitishwa uchaguzi wa marudio unaosubiri tarehe ya kufanyika kwake itakayotangazwa na ZEC.

MGOGORO WENYEWE
Zanzibar imeingia katika mgogoro wa kisiasa baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha,  kutangaza kufutwa kwa uchaguzi kutokana na kile alichoeleza kuwa ‘haukuwa huru na wa haki’, ingawa ndiwo uliotumika kupata kura zilizompa ushindi Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Uamuzi huo wa Jecha unapingwa na CUF ambayo mgombea wake, Maalim Seif Sharif Hamad, aliitisha mkutano na waandishi wa habari hapo kabla na kuwaonyesha alichodai kuwa ni karatasi halisi za matokeo ya kura kutoka katika vituo vyote visiwani humo zikionyesha kuwa ameshinda kwa asilimia 52.87.

Kadhalika, waangalizi mbalimbali wa ndani na wa kimataifa wamepinga hatua ya kufutwa kwa uchaguzi huo, baadhi wakiwa ni Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Afrika Mashariki na pia balozi za mataifa ya Marekani, Uingereza na Ireland ya Kaskazini.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment