Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, na Mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, jana walikutana jijini Dar es Salaam na kuteta kwa zaidi ya saa moja.
“Ndugu waandishi wa habari tumekuwa na kikao kifupi na mazungumzo kuhusiana na suala la Zanzibar, Jumapili (kesho) tutazungumza na waandishi wa habari kwa undani juu ya suala hilo,” alisema Lowassa.
Maalim Seif aliwasili ofisini kwa Lowassa, Mikocheni eneo la viwanda vidogo, majira ya saa 10:45 jioni na kupokewa na mwenyeji wake na baadaye kwenda kwenye chumba cha siri kwa mazungumzo yaliyohusisha pia baadhi ya viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Lowassa katika Uchaguzi Mkuu uliopita, alilalamika kutokubali matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kwa madai kuwa kura zake zilichakachuliwa.
Kufuatia malalamiko hayo, viongozi wa Ukawa, walisusia hafla ya kukabidhiwa cheti cha mshindi wa urais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli, iliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
Aidha, viongozi hao pia walisusia sherehe za kuapishwa kwa rais huyo wa Awamu ya Tano, zilizofanyika katika Viwanja vya Uhuru.
Baadhi ya viongozi waliokuwapo kwenye mkutano wa jana kati ya Lowassa na Maalim Seif ni Wenyeviti wenza wa Ukawa, James Mbatia na Twaha Taslima wa Chama cha Wananchi (Cuf),walioambatana na mmoja wa wanasheria wa Chadema, Prof. Abdalah Safari na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Prof. Mwesiga Baregu.
Mbatia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi na Taslima ni Mwenyekiti wa Cuf, baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba, kujiuzulu wadhifa huo.
Ukawa inaundwa na vyama vya Cuf, Chadema, NCCR- Mageuzi na National League for Democracy (NLD), ambavyo vilimuunga mkono mgombea wa Chadema, Lowassa.
Mara baada ya mazungumzo hayo, walipiga picha ya pamoja na Lowassa kuzungumza kwa ufupi na waandishi wa habari. Waandishi wa habari walimuuliza Maalim Seif kuhusu mazungumzo yaliyofanyika baina yake na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Hata hivyo, alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa.
Kuhusu msimamo wa Cuf kuhusu uchaguzi mkuu, alisema haujabadilika ni ule ule wa kutotambua kufutwa kwa matokeo ya urais, wanachotaka ni kura zihesabiwe na mshindi wa nafasi hiyo kutangazwa.
“Msimamo wa CUF uko wazi tangazo la kufutwa kwa uchaguzi lilitolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, ni lake ndiyo maama linasema mimi Jecha na siyo vinginevyo,” alisema na kuongeza;
“Hatuwezi kushiriki uchaguzi mwingine utakaotishwa kwa kuwa tumeshiriki huu na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiyo kimeyakataa matokeo, wakileta uchaguzi mwingine hatutakubali.’
Maalim Seif alisema tangazo la kufuta uchaguzi ni la Jecha hivyo siyo msimamo wa Zec, na Cuf inasubiri kura zihesabiwe na mshindi kutangazwa.
Uchaguzi wa Zanzibar ulifutwa Oktoba 28, mwaka huu, na Mwenyekiti wa Zec, Jecha, ambaye alieleza sababu tisa za kufutwa kuwa ni pamoja na wajumbe wa Tume kutofautiana na kuonyesha itikadi za vyama, kasoro kama za kuongezeka kwa kura hasa Pemba zaidi ya wapigakura halisi.
Nyingine ni namba za fomu kufutwa, vyama kuingilia majukumu ya Tume na baadhi ya vijana wa vyama vya siasa kuvamia vituo vya kupigia kura.
Tangu kufutwa kwa uchaguzi huo kumekuwa na matamko mbalimbali ya kimataifa na kitaifa, yakitaka kutangazwa kwa matokeo hayo kwa kuwa waangalizi wa ndani na nje waliridhika na mchakato wa uchaguzi na kushangaa sababu zilizotolewa na Jecha za kufuta uchaguzi.
Rais wa Zanzibar na Dk. Shein na Maalim Seif, wameshakutana kwenye mazungumzo kuhusu uchaguzi huo, mapema wiki hii.
Maalim Seif pia alipeleka barua kwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, ambaye alisema suala hilo ameliacha kwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli.
Serikali ya Zanzibar imeshatoa ufafanuzi wa kikatiba na sheria kuwa Dk. Shein ataendelea kuwa rais hadi rais mwingine atakapopatikana.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment