HAIJAPATA kutokea hata mara moja Zanzibar, nchi ya visiwa vikuu viwili na vidogo viwili vitatu, iliyoko pembeni kwa ukanda wa Bahari ya Hindi, konani mwa Afrika Mashariki, kuongozwa kijeshi. Siku zote ni wananchi wenyewe na walio raia, ndio wamekuwa wakishika hatamu ya kuiongoza Zanzibar.
Sasa angalia tofauti yake na Myanmar. Imekuwa ikifanya uchaguzi tangu 1995 chini ya dhana ya demokrasia ya mfumo wa vyama vingi unaoruhusu siasa za ushindani, kupitia vyama vya siasa vinavyoteua wagombea na kushindania viti katika chombo cha kutunga sheria cha Zanzibar ambacho ni Baraza la Wawakilishi.
Hata hivyo, haijafaidi matunda hasa ya demokrasia. Katika uchaguzi wake, vyama huteua wagombea wakagombania kiti cha urais, mtumishi wa wananchi anayekaa majengo yanayoitwa Ikulu yaliopo Mnazimmoja, mjini Zanzibar. Lakini, kumbe, umeshapatikana uthibitisho usio shaka kuwa mfumo huu ni geresha bwege, au ishtizai au dhihaka.
Zanzibar wakati wa uchaguzi inadhibitiwa na mfumo wa kijeshi. Wiki kabla ya siku ya uchaguzi, siku ambayo wananchi wa Unguja na Pemba walitarajiwa kufika vituo vya uchaguzi na kupigakura, walionekana askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Zanzibar (JWTZ), wameshika vituo muhimu vya serikali.
Wameshika mageti ya Idhaa ya Redio na Televisheni zinazoendeshwa na serikali kwa kodi ya wananchi wote. Walishika Bandari Kuu ya Malindi, walishika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume uliopo Kisauni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Wakati wanajeshi wamedhibiti ulinzi kwenye maeneo hayo, mitaa ya mji imejaa askari wanaotembea kwenye gari zao wakiwa wamebeba silaha huku makundi makubwa yakikutwa yakizunguka mitaa kwa kutembea. Bali mbali na askari wa vikosi viwili vinavyogharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), kuna utitiri wa askari wasio nidhamu wa vikosi vinavyogharamiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Hivi vikosi siku hizi vinaitwa Idara Maalum, baada ya jina la Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kufutwa.
Inawezekana wanasiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaodhibiti hatamu za uongozi wa serikali waliona jina la vikosi linatisha watu. Hawakujua, hizo idara maalum hazijsaidia kuwavua askari wao na lawama, shutuma na masimango kutoka kwa wananchi. Mienendo yao ya utendaji kazi haujabadilika, labda kuongezeka uhuni.
Unaposikia kuna Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), tena ukaambiwa ni tume huru inayoundwa na makamishna wa vyama vya siasa viwili, kila kimoja kikitoea makamishna wawili, na mwingine akitoka vyama vingine vyenye ufuasi wa vidoleni, usidhani hiyo tume ni huru kweli. Asilani.
Wakati wa uchaguzi unakuta watu wasiokuwa makamishna wala watendaji halali wa Tume hii, wanashika majukumu wakiwa wamevikwa vikoti vyenye sura ileile kama vikoti vya watendaji wa Tume yenyewe. Wote hawa ni watumishi wanaotumwa kutekeleza mipango ya kukisaidia chama kinachoongoza kibakie na utawala.
Usidanganyika kwamba ah, lakini si Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaundwa na CCM na Chama cha Wananchi (CUF). Muundo huu nao ni geresha bwege nyingine. Umebaki hapohapo kwenye Baraza la Mapinduzi (BLM), Dk. Ali Mohamed Shein aliyeshika usukani wa urais 2010, baada ya mfumo huo wa uendeshaji serikali kuundwa kikatiba, ameshindwa kuukomaza mfumo huo chini ya hapo.
Anazijua vizuri zaidi sababu za kushindwa kwake. Mimi ninachokiona ni kwamba hakutaka kubadilisha aliyoyakuta, ambayo kwa hakika kabisa, yamejengwa na matakwa ya CCM kujichimbia kwenye hatamu za utawala wa Zanzibar.
Sasa wale wanaovaa vikoti vya Tume wakati si watumishi wa tume hasa, husaidiwa mipango yao na askari wale wasio nidhamu. Wakati mwingine Polisi hupewa jukumu la kuwalinda wafanye walichotumwa.
Hujifanyia watakavyo kwa sababu machoni wanaonekana ni watumishi wa Tume ya Uchaguzi. Matendo yao ndiyo huzindua wananchi kuwa wameingia kutumikia maslahi ya CCM. Hawa wataingia kama wanavyoingia vituoni wale askari wasio nidhamu na watapiga kura watakavyo.
Haikuwa kazi rahisi katika uchaguzi uliokwamishwa. Walibanwa sana wasitekeleze walichotumwa. Ni majimbo machache ya kuhesabu walipenya, la Mahonda, Tumbatu na Kiembesamaki, miongoni mwao.
Uchaguzi wa safari hii ulipata bahati ya mtende. Mawakala walipata heshima yao stahiki. Fomu za kurekodia matokeo zilitolewa vizuri kuliko miaka yote ya uchaguzi. Hata za kura za urais zilitolewa vizuri haijapata kutokea.
Wakati Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha anatangaza matokeo ya kura za urais za majimboni, kila chama kilishajua kimepata kura ngapi na wapi. Fomu zilizobandikwa kwenye vituo zilikohesabiwa, ziliwajulisha hesabu ya kura hizi.
Hili ni eneo ambalo CCM wanajuta kulikubali. Wanaulizana ilikuaje wakaruhusu itokee. Hawataki kuamini kuwa wakati ulilazimisha, na hasa kwa kuwa maandalizi ya uchaguzi yalihusisha ufadhili wa Umoja wa Mataifa kupitia Shirika la Maendeleo (UNDP). Uwazi ulikuwa lazima, ingawa ndio huohuo haukushuhudiwa kwa ukamilifu wake.
Sasa Myanmar baada ya miaka 25 ya utawala wa kijeshi, huku watawala wakimkandamiza kwa kila namna Aung San Suu Kyi, mwanamke shupavu katika harakati za kusaka demokrasia ya watu wa Myanmar, walikubali kufanyike uchaguzi wa kidemokrasia. Bali jeshi wenyewe nao wakaanzisha chama chao Union Solidarity and Development.
USD kikashindana na National League for Democracy (NLD), jina lilelile la chama cha aliyekuwa mwanasiasa makini, Dk. Emmanuel Makaidi ambaye licha ya kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa matumaini ya kupata kiti cha bunge kwa mara kwanza tangu uchaguzi wa 1995, hakufanikiwa. Mwenyewe aliishia kifo cha machungu wiki mbili kabla ya kura kupigwa. Aligombea kiti cha Masasi, mkoani Mtwara.
Zanzibar haijapata demokrasia inayoitaka, lakini Myanmar wameipata ndani ya utawala wa kijeshi. Suu Kyi amefanikiwa kuwaondoa wanajeshi Ikulu. Ameshinda asilimia 82 ya viti vya Bunge la viti 664, likiwemo bunge dogo na kubwa.
Huku mama huyu akiwa ameshinda kiti cha ubunge, upande mwingine ndiye anasubiriwa kuteua mtu wa kuwa rais wa Myanmar. Hata hivyo bado jeshi litapata viti mahsusi kikatiba, litadhibiti usalama wa taifa.
Ni afadhali demokrasia ya Myanmar kuliko Zanzibar, ambako wananchi wanaambiwa wanajitawala lakini wanapofanya uamuzi wa kuchagua kiongozi, wanazuiwa kwa hujuma inayosaidiwa na majeshi. Kuna funzo kubwa hapa.
Chanzo: Mwanahalisi
No comments:
Post a Comment