HATUA aliyoitekeleza Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufuta uchaguzi huku yeye mwenyewe akiwa ameshatangaza zaidi ya asilimia 70 ya matokeo, ilitarajiwa.
Ilitarajiwa katibu mkuu mstaafu serikalini huyu, na mwenye kima kifupi kimaumbile, atatafuta kisingizio, ikibidi hata cha kutengeneza mwenyewe, mpaka amridhishe bwana-mteuzi.
Jecha aliteuliwa na Dk. Ali Mohamed Shein, rais ambaye leo anakamilisha muda wa uongozi wake, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Toleo la 2010, na ambaye ameingia tena kutafuta ridhaa ya miaka mitano mingine.
Huyu Jecha alijitafutia la kufanya sio tu kwa ajili ya kufurahisha aliyemteua na chama chao. Alitafuta njia ya kutokea ili atimize dhamira yake ya kufurahisha moyo wake, utashi wake na ushabiki wake uliopitiliza wa CCM.
Ipo kwenye kumbukumbu kwamba aliomba nafasi ya kuwania ubunge jimbo la Amani, mjini Zanzibar lakini aliangushwa katika kura za maoni, na hakuteuliwa majina yalipopelekwa Kamati Maalum ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC-CCM).
Lakini kule kuonesha nia tu ya kutaka uongozi wa kuwakilisha wananchi kupitia CCM, kulimpatia tuzo – akateuliwa na Dk. Shein mwaka 2013 kushika wadhifa mzito wa Mwenyekiti wa ZEC. Ina maana anakuwa kiongozi mkuu wa Tume ya Uchaguzi, muongoza vikao vya makamishna na mtangazaji wa matokeo ya urais.
Hivi mtu kama huyu, mwenye historia mwanana ya kuwa kada wa CCM, utamtarajiaje awe muadilifu kwa kutenda haki panapokuja ushindani unaomhusisha mwanasiasa anayeongoza kundi lisiloamini kamwe siasa, sera, imani na malengo ya CCM?
Mimi mwenyewe sikuamini niliposikia ameteuliwa ili kushika wadhifa huo mkubwa kabisa wa Tume ya Uchaguzi ambayo haijafanikiwa kujenga imani kwa wananchi kuwa inaweza kutegemewa kuendesha uchaguzi wa viwango na ikatenda haki kwa mstahiki.
Sikuamini wakati ule, na hata sasa ningali naamini tu kuteuliwa kwake hakukuwa na nia ya kusaidia ujenzi au uimarishaji wa demokrasia Zanzibar, hatua mojawapo ikiwa hii ya kuendesha uchaguzi ulio huru, wa haki na katika taratibu zilizo wazi.
Huyu Jecha ni mtu mchangamfu sana. Ukimuona waweza kumpa heshima na kumuamini. Alivyo kwa nje, unamuona mwenye busara na anayeweza kuona ukweli akaushuhudisha.
Tatizo kubwa ni yeye kuwa kada wa CCM. Kwa asili ya siasa za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilivyo, makada wa CCM hasa walio katika umri wa kuelekea kustaafu utumishi wa umma, na yeye akiwa ameshastaafu, huwa wagumu wa kuamini zao zimepita hazirudi tena.
Wengi wao hulialia waongezwe muda wa kutumikia nchi. Utadhani ni kweli wanashauku na dhamira hasa ya kutumikia umma – kwa hakika asilimia kubwa yao wamejaa mahaba ya kutumikia matumbo yao. Maslahi yao. Siku hizi Zanzibar utasikia mtu akisema, ah fulani ni BT (Bora Tumbo) kama anavyoitwa rafiki yangu mwa fulani.
Hapana shaka, kwa kufuta uchaguzi ambao makundi mengi kama si yote ya waangalizi walishausema umekidhi vigezo vya kuitwa uchaguzi ulio huru na wa haki, kwa kuwa wameona marekebisho mengi wakilinganisha na uchaguzi wa 2010, Jecha amethibitisha ni “BT.”
Ninapokutana naye huwa na mawili matatu kuzungumza. Wiki chache baada ya kuteuliwa kushika uenyekiti wa ZEC, tulikutana Rahaleo, mjini Zanzibar, nilipokuwa nasubiri picha za binti yangu aliyekuwa anahangaikia hati ya kusafiria ili kwenda masomoni nchini India. Hii ilikuwa ni Juni 2013.
Kwa kuwa alinikuta nimekaa, naye amenizidi umri, nilisimama nikampa heshima. Tukasalimiana kwa kupeana mikono bukheri khamsa ishirini kama ilivyo desturi ya Wazanzibari. Ninatabasamu naye anatabasamu.
Nikamwambia neno la kumpongeza. “Nikupongeze kwa kuteuliwa.” Maneno yangu ya ziada kwake yalikuwa hivi, “nimekupongeza kwa sababu ni kawaida anayeteuliwa kuchukua dhamana ya kutumikia umma kwa nafasi kubwa na nzito kama hii anastahili kupongezwa.”
Lakini, nikamwambia upande mwingine. “Ila kwa dhamana uliyopewa, nakupa pole maana najua itakushinda ila, nakutakia kila la kheri na Mungu akujaalie.”
Alishtuka na haraka nikamuwahi, “Najua ninachokisema, nakujua kiasi.” Kwa unyonge alijipa imani ataiweza dhamana. Nikaongeza neno la kumtakia kila kheri kwa mara ya pili.
Huyu ndiye Jecha ambaye baada ya kukimbia dhamana yake kwa siku mbili Oktoba 26 na 27, aliamua kulikoroga. Kutangaza uchaguzi umeharibika siku ya nne ya kutangaza matokeo ni kulikoroga kabisa.
Aliahirisha haraka kikao cha Jumanne usiku mchana mara tu umeme ulipokatika kwenye ofisi maalum za Tume ndani ya Hoteli ya Bwawani. Hakukuwashwa jenereta ambalo mchana liliwashwa umeme ulipokatika.
Akaahidi kikao cha kuhakiki matokeo kuwa “tuendeleeni kesho saa 4 asubuhi.” Waandishi nao wakaambiwa (nilikuwa sijaingia ndani) matokeo yataendelea kutangazwa kesho yake.
Wakati hayo yakitokea, watu wazima wale wa Tume wanaoongozwa na Jecha walikuwa wametangaza matokeo ya majimbo manne tu kati ya majimbo 54 ya Zanzibar. Yeye ndiye mtangazaji mkuu, si mwingineo.
Jumatano hakufika mapema ofisini. Baadaye ikajulikana kuwa hakufika mpaka subira ya kusubiriwa afike aongoze kikao ilipokatika. Makamishna wakaridhiana kuwa kikao kiendeshwe na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji Abdulhakim Ameir Issa.
Tafadhali huyu ni jaji mwerevu aliye kazini, sema tu aliondolewa Idara ya Mahakama isivyotarajiwa baada ya kutoa ripoti nzuri ya uchunguzi wa ajali ya meli ya Spice Islander iliyoua mamia ya watu mwaka 2012. Labda hakuwafurahisha waliompa kazi ile.
Jaji Abdulhakim akaongoza kikao. Kilikuwa ni kikao cha kukamilisha kazi ya uhakiki wa matokeo ya majimbo 22 ya mwisho, manne yakiwa ya Unguja, na yaliyobakia 18 ya kisiwani Pemba, kule ambako CCM imekuwa ikihenyeshwa kwa kuzuiwa isifikishe asilimia 10 ya kura za urais.
Kumbe wakati Jecha amejichimbia anakokujua na waliopanga naye ushetani, wakagundua “si kule kazi inaendelea, wakimaliza je na kutangaza, itakuaje?” nasikia yalikuwa maoni ya mmoja ufichoni.
Jibu lililotoka ni mpango wa kumtoa kikaoni Jaji. Masikini akafuatwa kwa askari makomandoo, akiwemo mtoto wa waziri mmoja katika serikali inayotoka. Ni kutoka CCM sio CUF. Walivyomchukua kila aliyeona anaendelea kusema, “walimteka makamu mwenyekiti.”
Mimi nasema hivi, “Maaskari wajuzi wa watawala walimteka Jaji Abdulhakim.” Wakampeleka anakokujua na yeye. Nimejitahidi kumuuliza hajanieleza alikopelekwa. Najua si rahisi kusema haraka hivyo. Ila “ataja sema tu iko siku.”
Kumteka jaji kulikuwa na maana moja tu – kuua kikao cha kukamilisha kazi muhimu ya wananchi. Ikafa kweli.
Makamishna walipopata taarifa wakasambaratika baada ya kusikitika. Hakuna kazi tena. Na waandishi wakatoweka, na wananchi waliobahatika kupenya ulinzi mkali wa maaskari kazi, nao wakaondoka Bwawani.
Muondoko wao ulisukumwa na kuondoka kwa makamishna ambao waliondoka kwa kuwa hawana kazi, iliyokufa kwa sababu mwenyekiti Jecha alishatangaza eti “uchaguzi umeharibika na naufuta, utarejewa.” Jecha alitoa sababu tisa. Zote hazina mashiko mbele ya Sheria na Katiba ya Zanzibar.
Kila uthibitisho umeshatolewa wa hilo. Sababu nyepesi na za ovyo. Masikini Jecha Salim Jecha, leo anatakiwa ahojiwe na timu ya majaji kwa tuhuma za kutenda kosa baya la kuzusha machafuko Zanzibar. amenithibitisha.
CHANZO ZANZIBAR YETU
No comments:
Post a Comment