Ugomjwa wa kipindupindu mpaka mwanzoni mwa wiki hii, ulikuwa umeua watu 106 kote nchini na maelfu kuugua maradhi hayo.
Hadi kufikia jana, taarifa zilieleza kuwa ugonjwa huo ambao chanzo chake kikuu ni uchafu wa mazingira, ulikuwa umeua watu 53 huku wengine 4,202 wakiugua maradhi hayo kwa Jiji la Dar es Salaam peke yake.
Kati ya wagonjwa hao, kwa mujibu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Mecky Sadiki, 1,981 walitoka Manispaa ya Kinondoni, 1,554 Manispaa ya Ilala na 667 Manispaa ya Temeke.
Sadiki alizitaja kata katika Manispaa za Kinondoni zilizoathirika zaidi kwa ugonjwa huo kuwa ni Manzese, Tandale, Kigogo, Mburahati na Saranga.
Katika Manispaa ya Ilala ni kata ya Buguruni, Vingunguti, Jangwani, Kariakoo, Kiwalani, Mchikichini na Ilala wakati Manispaa ya Temeke ni Tuangoma, Magogoni, Mbagala, Keko, Temeke, Yombo Vituka, Makangarawe na Kibonde Maji.
Aidha, imeelezwa kuwa Serikali imetumia Sh. bilioni 1.8 kukabiliana na ugonjwa huo jijini Dar es Salaam.
Katika kukabiliana na hali hiyo serikali imevifungia visima vya maji 303 vikiwamo vilivyobainika kuchafuliwa na kinyesi cha binadamu chenye vimelea vya kipindupindu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, alisema serikali imetumia kiasi hicho kikubwa katika kukabiliana na ugonjwa huo, fedha ambazo zingeelekezwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo, lakini zimeishia kutibu ugonjwa unaotokana na uzembe.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, kiasi hicho cha fedha kimetumika kununua dawa za kutakasa maji, kutibu wagonjwa, dawa za kutakasa nyumba na mazingira waliyotokea wagonjwa, kuhudumia kambi za kipindupindu, kusambaza maji kwa njia ya boza kwenye kata zilizoathirika na dawa ya water guard.
Hali kadhalika, fedha nyingine zilitumika kwa vipeperushi, mafuta ya magari kwa ajili ya ufuatiliaji na malipo ya watumishi wanaofanya kazi kwenye makambi.
Hata hivyo, alisema fedha hizo zinaweza kuongezeka kwa kuwa hazikujumlishwa pamoja na misaada ya wahisani mbalimbali.
Moja ya sababu kubwa inayochangia ugonjwa huu kuendelea kusambaa kwa kasi, ni uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji kutotunzwa ipasavyo.
Kwa msingi huo, ili kuudhibiti, hapana budi wananchi kufuata kanuni za usafi katika maeneo wanayoishi, fanyia kazi na maeneo ya biashara kama masoko, hoteli, baa, mama ntilie nakadhalika.
Suala la usafi kwa ujumla, ni tabia ambayo kila mwananchi anapaswa kuiheshimu.
Tunawashauri Watanzania wabadilike kwani ugonjwa huu ni wa hatari sana.
Kwa hakika kama hatutakuwa makini, ugonjwa huu utaleta maafa makubwa hasa katika kipindi hiki ambazo mvua zimeanza kunyesha katika maeneo mengi ya nchi.
Ni muhimu kuzingatia kwa dhati kabisa kanuni za usafi ambazo mbali ya usafi wa mazingira, pia kuhakikisha kwamba maji ya kunywa yanachemshwa, kunawa mikono baada ya kutoka msalani, kuosha matunda kabla ya kula na usafi wa vyombo vyote vinavyotumiwa kwa chakula ama kinywaji.
Ni matumaini yetu kwamba Watanzania watazingatia haya pamoja na maelekezo yanayotolewa mara kwa mara na wataalam wa afya ili kuepusha maafa zaidi ya gonjwa hili.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment