Kufuatia tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar kufuta matokeo yote ya Uchaguzi wa Rais, Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani, kumejitokeza kauli za uchochezi zenye kuashiria uvunjifu wa amani sambamba na matishio ya miripuko inayoendelea kujitokeza.
MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI ZANZIBAR KUHUSU KUWATAHADHARISHA WANANCHI KUTOJIHUSISHA NA VITENDO VYA VURUGU NA UVUNJIFU WA AMANI
Mnamo siku ya tarehe 25 Oktoba 2015 Wananchi wa Zanzibar walishiriki katika zoezi la kupiga kura kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar Wabunge Wawakilishi na Madiwani.
Kufuatia tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar kufuta matokeo yote ya Uchaguzi wa Rais, Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani, kumejitokeza kauli za uchochezi zenye kuashiria uvunjifu wa amani sambamba na matishio ya miripuko inayoendelea kujitokeza.
Halikadhalika kauli ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamadi ya kuisindikiza Tume ya Uchaguzi Zanzibar imtangaze kuwa mshind pamoja na kauli za wafuasi wa chama hicho za kuhamasika ni nyimbo mbaya isiyohitaji kuchuchiwa mtoto, kwa lugha nyepesi si vyema jambo hilo kufumbiwa macho na vyombo vya ulinzi na usalama likiwemo Jeshi la Polisi kwa lengo la kudumisha amani tuliyo nayo.
Aidha Jeshi la Polisi linapenda kuwatahadharisha wananchi kutojihusisha kufanya fujo kwa madai yoyote yanayotolewa na baaadhi ya wanasiasa kwamba kuanzia tarehe 02 Novemba 2015 kutakuwa hakuna Serikali, na pengine watu watakuwa huru kufanya watakavyo.
Kifungu cha 28(1) Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 :Kimeeleza kwamba ‘Kufuatana na Katiba hii mtu ataendelea kuwa Rais mpaka :
(a) Rais anayefuata ale kiapo cha kuwa Rais, au
(b)Afariki wakati akiwa Rais, au
(c) hapo atakapojiuzulu ; au
(d) iwapo amechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ; au
(e) kwa sababu yoyote nyengine ameacha kuwa Kiongozi kwa mujibu wa vifungu vyengine vya katiba hii.
Ikumbukwe kuwa kutokuwepo Rais wa Nchi kama inavyodaiwa haimaanishi sheria hazipo na watu wafanye watakavyo. Kuna makosa ukiyafanya moja kwa moja sheria itachukua mkondo wake ikiwemo
Kufanya kitendo cha uvunjifu wa amani
Kufanya maandamano ama mikusanyiko ya watu isiyo halali
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Zanzibar
Kifungu 55(1)Kinaeleza kwamba ‘Pindi watu watatu au zaidi wakikusanyika kwa lengo la kufanya kosa na kusababisha kutia hofu watu wengine na kupelekea uvunjifu wa amani utahesabika mkusanyiko huo sio halali’
Kifungu 74(1) ‘b’Kinaeleza kwamba « katika mkusanyiko wa watu ukatumia vitisho au matusi au ukatumia maneno ya kushawishi watu kufanya uvunjifu wa amani utakuwa umefanya
kosa la uchochezi »
Tunawaomba wananchi kuacha ushabiki na jazba ili kuwaondoshea gharama za matatizo wao wenyewe na familia zao. Waswahili wanasema ‘Vyako ni vyako likikupata ni la kwako’ na ‘Kila Mchumia janga hula na mwanawe’’.Ni vyema kipindi hiki kuhubiri amani pamoja na kuwa na subira kuiachia Tume ya Uchaguzi Zanzibar ambayo ndiyo yenye dhamana na mamlaka ya kutangaza tarehe ya kurejewa kwa Uchaguzi huo na si mtu mwengineyo kama inavyodaiwa.
CHANZO ZANZIBAR YETU
No comments:
Post a Comment