Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linatarajiwa kufunguliwa rasmi huko Dodoma kesho huku mchakato wa wagombea mbali mbali kutoka vyama vya siasa, wa nafasi ya Spika iliyoachwa wazi na Anne Makinda baada ya kumaliza muda wake ukisubiriwa kwa hamu kuwasilishwa ndani ya Bunge hilo.
Kwa kipindi hiki, baadhi ya wanasiasa wakongwe pamoja na wasomi wa taaluma mbalimbali, na waliowahi kushika nafasi ya Spika, wamekuwa wakitoa maoni ya sifa za Spika anayefaa kukabiliana na Bunge la sasa, ambalo wanasema linaonekana kubeba changamoto nyingi kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wabunge vijana.
Changamoto nyingine za Bunge la 11 zitatokana na sababu ya kuwepo kwa idadi kubwa ya wabunge wa upinzani, hali ambayo itasababisha nguvu ya upinzani ndani ya Bunge kuwa kubwa na mijadala kuchukua sura tofauti na mabunge yaliyopita.
Wadau hao wanasema wanataka Spika ambaye atakuwa na busara pamoja na uwezo mkubwa wa kutafsiri kanuni zinazo liongoza Bunge, na pia awe na ufahamu mzuri wa sheria pamoja na uzoefu wa kutosha katika masuala ya uongozi.
Anne Makinda ambaye ameamua kustaafu baada ya kuwa mtumishi kwa nafasi mbalimbali ndani ya chama na serikalini kwa miaka 40, amesema Spika anayetakiwa ni lazima akubali kujifunza tabia za wabunge wake na awe na uwezo wakukabiliana na hali halisi ya bungeni.
Makinda alisema Spika lazima awe mvumilivu na anayeweza kuzuia hasira, na badala yake atumie muda mwingi kujifunza kanuni za Bunge na kuwa mwepesi kupokea hoja za wabunge bila kubagua ili aweze kuzifanyia kazi.
Tunaamini kuwa Spika wa Bunge lenye wabunge wa vyama mbalimbali anatakiwa asionyeshe dalili za kuliburuza bunge kwa kung'ang'ania msimamo wa upande mmoja tu, pia Spika asifuate itikadi za vyama wakati wa kuendesha mijadala.
Spika ambaye ni mwadilifu atatenda haki, atafuata kanuni zinazoongoza Bunge na pia atakuwa na subira ya kusikiliza hoja za wabunge bila kuonyesha ubaguzi wa aina yoyote, atapata heshima kutoka kwa wabunge wote na hatimaye itakuwa rahisi kwake kuliongoza Bunge kwa ufanisi zaidi.
Pius Msekwa, aliyewahi kuwa Spika kwa miaka 10 mfululizo, anasema hakuna haja ya kuangalia kama ni idadi gani ya wabunge vijana au wazee ili Spika apange mfumo wa kuendesha vikao vyake, alisisitiza kuwa suala kubwa kwa Spika ni kufuata kanuni na sheria za Bunge.
Kama alivyosema Mzee Msekwa, Bunge ni taasisi ya utungaji wa sheria za nchi, wabunge nao, bila kujali jinsia zao wala umri walionao, wanawajibika kufuata kanuni na sheria zinazotawala Bunge, mbunge anapokiuka kanuni na taratibu zilizopo, anawajibika kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Tunaamini wabunge kama ilivyo kwa binadamu wengine, wanatofautiana katika maono na mitazamo ya mambo mbalimbali, na wanatofautiana katika kujadili, kufanya maamuzi na hata katika utekelezaji.
Wabunge wengine wanamitizamo hasi kwa kila kinachojitokeza, katika hali kama hii, Spika anatakiwa awe mpole, mvumilivu na mshawishi kwa wabunge wa aina hiyo.
Tunakumbuka changamoto alizozipata Spika mstaafu Anne Makunda, aliweza kupambana na baadhi ya wabunge walioonekana machachari wakati wa mijadala, kwa kutumia busara, uzoefu na uadilifu wa kufuata kanuni, aliweza kudhibiti vituko mbalimbali na Bunge liliendelea.
Inawezekana kukawa na sifa za ziada za Spika anayeweza kuhimili changamoto mbalimbali za Bunge la 11, kimsingi sifa hizo, kama zipo lazima zisaidie kuhuisha ufanisi wa kanuni, sheria na mwenendo wa Bunge utakaozingatia maadili.
Tunaamini muda mwingi wa Bunge la 10 lililopita, ulitumika katika mijadala mingi ambayo haikulenga miradi na mipango ya maendeleo ya majimbo ya wabunge.
Bunge lilitumia muda mwingi kujadili ufisadi, rushwa na kashfa nyingine zilizogusa miundombinu mbalimbali, Bunge hili lizingatie zaidi maendeleo ya majimbo ya wabunge wanayoyawakilisha, wananchi wanahitaji mabadiliko ya maendeleo.
Wabunge wamsaidie Spika mpya katika kutekeleza kanuni na sheria za Bunge ili kasi ya maamuzi ya busara yafanyike kwa kuzingatia wananchi wanatarajia mabadiliko ya kweli ya maendeleo yao.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment