tangazo

tangazo

Tuesday, November 24, 2015

WARAKA WA ZATU JUU YA HOJA YA KUANZISHWA KWA KODI YA ELIMU “EDUCATION LEVY” KISHERIA ZANZIBAR


1.0              UTANGULIZI
Moja kati ya mambo makubwa na adhimu ya kujivunia Wazanzibari, ni uwamuzi uliochukuliwa na  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tarehe 23 Septemba 1964, wa kutoa elimu kwa wananchi wake wote bila ya malipo, SERA YA ELIMU BURE KWA WOTE. Sera hii ilikuwa ni mfano kwa wengine hapa Afrika, ambapo baadhi ya mataifa yaliiga. Mfano wa mataifa hayo ni Mauritius. Pamoja na kuyumba kwa uchumi wa taifa letu, lakini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wakati wote imekuwa ikiisisitiza na kuin’gan’gania sera ya elimu bure kwa wote. Bila shaka imekuwa ikifanya hivi kwa kuamini kuwa, elimu sio tu ni haki ya msingi kwa kila raia, bali pia ndio msingi mkuu wa maendeleo ya jamii yetu. Chama cha Walimu Zanzibar kwa dhati, kinaipongeza sana serikali yetu kwa hatua hii ya kimaendeleo na kimapinduzi. 
Lakini pamoja na nia njema na nzuri ya serikali  yetu, mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, yamepelekea nia njema hii, kuwa na changamoto kubwa na nyingi, kiasi cha kuathiri matokeo ya jumla ya nia yenyewe. Sio siri hata chembe, kuwa ubora wa elimu yetu umeshuka, tena umeshuka sana. Hali hii ya kushuka kwa ubora wa elimu, imetokea wakati taifa likiwa linapiga hatua kubwa, ya mafanikio ya kusambaza huduma ya elimu katika nchi yetu. Kwa sasa hakuna mwanafunzi anaepaswa kutembea, masafa marefu ya zaidi ya kilomita tatu kufuata skuli. Kwa maneno mengine inawezekana kusema kuwa taifa limefanikiwa kuongeza idadi ya skuli, na wanafunzi wanaosoma, lakini ongezeko hilo haliendani sambamba na ongezeko la ubora wa elimu yenyewe.
Inakubalika kuwa katika elimu kinachohitajika, sio wingi wa idadi bali ni ubora, hivyo haitoshi kabisa kuridhika na wingi pasina kuangalia ubora wa elimu itolewayo.
Sababu kubwa ya kushuka kwa kiwango cha elimu nchini, ni gharama kubwa za elimu ambazo zimekuwa zikipanda siku hadi siku, hivyo ni wakati sasa wa kubuni njia na mbinu mpya za namna ya kuigharamia elimu yetu.
Waraka huu unakusudia kuwasilisha hoja ya Chama cha Walimu Zanzibar ZATU juu ya kuanzishwa rasmi kwa kodi ya elimu “Education levy” ili jaza pengo la gharama zinazohitajika za elimu nchini mwetu.
2.0              USULI WA TATIZO
Elimu katika nchi yoyote ni mali ya umma, hivyo ni wajibu wa umma kuigharamia. Taifa kwa ujumla wake, ni lazima libebe dhima ya kuhakikisha kuwa, gharama za elimu nchini hazikwamishi upatikanaji wake. Elimu lazima ipatikane kwa wote, na kwa ubora wa hali ya juu. Kigezo sahihi cha ubora wa elimu katika nchi, kiwe ni ubora wa elimu katika skuli za umma, ambazo kila mmoja ana uwezo wa kusoma. Hata pale zinapokuwepo skuli binafsi, jambo ambalo kwa sasa haliwezi kuepukika, kusijengeke mazingira ya kuwa, mwananchi akitaka elimu bora kwa mtoto wake, iwe ni lazima ampeleke katika skuli ya binafsi. Skuli binafsi ziwe ni kwa utashi wa mambo ya ziada tu na sio ubora wa elimu.
Katika makubaliano ya Dakkar ya Mkutano wa Dunia juu ya elimu, ilikubalika kuwa nchi maskini zisaidiwe kuona kuwa kila taifa linafikia lengo la elimu kwa wote kwa mataifa yenye uwezo kuwatoa fedha za kutosha kwa shughuli za elimu. Pia ilielekezwa kuwa, nchi zenyewe maskini zitenge asilimia 4-6 ya pato lote la taifa au asilimia 15 – 20 za bajeti zake kwa ajili ya masuala ya elimu, kulingana na ipi kati ya hiyo ni bora zaidi.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita imekuwa ikiweka elimu kuwa moja ya vipaumbele na kuwa bajeti ya elimu imekuwa ni wastani wa asilimia 20 ya bajeti yote ya serikali inayopangwa, japokuwa kiwango kitolewacho na hazina huwa pungufu ya hiyo asilimia 20.     
3.0              UCHANGANUZI WA TATIZO
Kama ilivyoelezwa hapo juu kuwa pamoja na nia ya serikali yakuwapa elimu watu wake bila ya malipo kumekuwa na changamoto nyingi zinazokwaza azma hiyo. Hoja za hapa chini ni miongoni mwa hoja za kuonyesha changamoto hizo.    
3.1       Hoja ya ufinyu wa Bajeti vis as vis mahitaji:
Japokuwa serikali hutenga asilimia ishirini (20%) ya bajeti yake ya matumizi kila mwaka kwa ajili ya elimu nchini, lakini kiwango hiki kinaonekana kuwa ni kidogo sana kukidhi mahitaji ya elimu yetu. Asilimia kubwa ya bajeti ya elimu inayotengwa na serikali huwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na mishahara ya walimu ambao bado wanalipwa mishahara duni na isiokidhi mahitaji yao. Ithibati ya hayo ni hii inayoonyeshwa na jedwali hapa chini   
S/N
MWAKA
BAJETI YA SHUGHULI ZA KAWAIDA
BAJETI YA MAENDELEO
1.
2012/13
7I,050,000,000/-
5,100,000,000/-
2.
2013/14
80,200,000,000/-
5,350,000,000/-
3.
2014/15
86,201,500,000/
3,300,000,000/-
CHANZO;  HOTUBA ZA WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI......  (2012-2015)

Sote tunajua kuwa elimu ni uwekezaji na ndio uwekezaji wa msingi katika taifa. Kwa hivyo ni dhahiri kuwa kwa uwekezaji huu tuko mbali na kufika huko tunakostahili kufika. Kwa ufupi ni kuwa pamoja na kuwa serikali hutenga asilimia ishirini ya bajeti yake kwa mwaka kwa ajili ya elimu nchini kiwango hicho ni kidogo sana, kwani sehemu kubwa ya fedha hizo huwa ni kwa matumizi ya kawaida na ni chache sana zinazowekezwa katika maendeleo ya elimu. 
3.2       Uchache wa fedha halisi zinazopatikana kutoka hazina
Hoja ya pili ni uchache wa fedha zinazotolewa na hazina kwa wizara pamoja na kuwa Baraza hili limepitisha Bajeti yake. Wizara ya elimu imekuwa ni moja ya wizara zinazopokea fedha pungufu za bajeti yake kutoka hazina. Hali hii inapelekea kwa kazi nyingi zinazopangwa katika sekta ya elimu kukwama. Jedwali hapa chini linatoa taswira ya hali halisi;
S/N
MWAKA
TAASISI AU IDARA
ASILIMIA YA FEDHA ZA MAENDELEO ZILIZOPATIKANA
ASILIMIA YA FEDHA ZA MATUMIZI YA KAWAIDA ZILIZOPATIKA
1.
2012/13
WIZARA ELIMU
80.3%
-
2.
2012/13
           “
59.2%
95.3%
3.
2013/14
           “
31.0%
83.7%
CHANZO; HOTUBA ZA WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI......  (2012-2015)
Kuna baadhi ya maeneo ya wizara ambayo hukosa fedha kwa kati ya zaidi ya themanini asilimia 80% hadi asilimia mia moja (100%). Mifano halisi ni hotuba ya bajeti ya 2014/15, ambayo ilionyesha upatikanaji wa fedha kutoka hazina kwa miradi mbalimbali. Ifuatayo ni miradi ikiwa na asilimia ya bajeti iliyopatikana kutoka hazina kwenye mabano;
4        Mradi wa uimarishaji wa Chuo kikuu cha Taifa SUZA              (43%)
5        Mradi wa uimarishaji elimu ya msingi                                        (18.0%)
6        Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Kiislamu                                      ( 0%)
7        Mradi wa uimarishaji wa Elimu mbadala na amali                  (15%)
8        Mradi wa uimarishaji wa elimu ya lazima                                 (35%)
9        Mradi wa uimarishaji wa elimu ya maandalizi                         (13%)
CHANZO; HOTUBA YA WAZIRI WA ELIMUNA MAFUNZO YA  AMALI ....(2014/15)
3.3         Utegemezi na upatikanaji usio muafaka wa fedha za wafadhili

Zanzibar kama zilivyo chini nyengine zinazoendelea zimepewa ahadi ya uhakika wa misaada ya fedha kutoka nchi zilizoendelea na mashirika ya kimataifa kwa ajili ya kuendeleza elimu na kufikia malengo ya maendeleo ya melenia, na hasa lengo la elimu kwa wote. Lakini kuna ushahidi kuwa matarajio ya serikali ya kupata fedha hizo huwa hayafikiwi. Katika hotuba za bajeti kwa karibu miaka mitatu iliyopita imeonyesha kuwa kile kiwango kinachopangwa na kutarajiwa kutoka kwa wafadhili hupatikana chini ya makisio

S/N
MWAKA
ENEO LILILOLENGWA MSAADA
MSHIRIKA WA MAENDELEO
FEDHA ZA MAENDELEO ZILIZOTARAJIWA
FEDHA ZILIZOPATIKA
1.
2012/13
i)                    Mpango wa maendeleo ya elimu



ii)                  Uimarishaji elimu ya maandalizi

iii)                Uimarishaji wa elimu ya msingi

AfDB, BADEA, WB SIDA , UNESCO na UNICEF

UNICEF



SIDA na UNICEF






419,200,000/-



4,969,938,000/-
21,585,548,444/-   (45%)




51,264,700/-   (11%)


359,576,800/-   (08%)
2.
2012/13
i)                    Uimarishaji SUZA

ii)                  Uimarishaji elimu mbadala na amali

iii)                Uimarishaji elimu ya maandalizi
 BADEA


AfDB




UNICEF
4,332,959,000/- 

1,994,098,000/- 



491,200,000/-
594,833,392/-   (13.7%)

1,230,070,040/-  (61.7%)



23,357,300/-   (22.9%)
3.
2013/14
iv)                Mpango wa maendeleo ya elimu

v)                  Uimarishaji wa elimu ya msingi


vi)                Uimarishaji elimu mbadala na amali
AfDB, BADEA na WB

Sida ,UNICEF UNESCO GPE na USAID

AfDB         
0



7,212,032,000/-



1,529,906,000/-
6,223,274,932/-  (20.6%)



2,881,271,948/-  (40.0%)


93,321,600/-      (15%)
CHANZO; HOTUBA ZA WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI......  (2012-2015)
3.4       Uwepo wa kodi mbalimbali ambazo zimekosa uratibu mzuri wa matumizi yake
Kwa sasa kuna kodi na michango mbalimbali rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya kuendesha elimu nchini. Hali hiyo ya kuwa na michango iliyo rasmi na ile ambayo haipo rasmi na wala mahesabu yake hayako wazi, inaweza kupelekea upotevu wa rasilimali za umma na kuwaruhusu wale wasio waaminifu kujinufaisha kwa fedha hizo.

Kwa upande wa michango rasmi ni pamoja na kodi zifuatazo:
i)                    Kodi ya maendeleo ya ujuzi “skill development levy” ambayo huwa inakusanywa kutoka kwa waajiri wote wakubwa na wadogo wa sekta ya umma na sekta binafisi
ii)                  Mchango wa madawati kwa wasafiri wanaosafiri kupitia bandari za Zanzibar.
Kwa upande wa michango isiyo rasmi ni pamoja na michango ifuatayo:
i)                    Michango ya wazazi maskulini ambayo pamoja na kuwepo kwa muongozo juu ya michango hii kila skuli imekuwa na kiwango chake ambacho kamati ya wazazi huwa wanakubaliana
ii)                  Michango ya walimu wenyewe wanayoitoa kwa hiyari kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiskuli.
iii)                Michango inayochangishwa na baadhi ya taasisi za elimu nchini mfano michango ya wanafunzi inayokusanya na Taasisi ya Sayansi na teknolojia ya Karume na Chuo cha Kiislamu

3.5      Umuhimu wa kuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya mahitaji na maendeleo ya elimu
Hoja nyengine ya kuwa na kodi ya elimu, ni haja na umuhimu wa kuwa na fedha za kutosha,   kwa ajili ya maendeleo na mahitaji ya elimu nchini. Kutokana na fedha kidogo isiokidhi mahitaji, walimu wamekuwa ndio waajiriwa wa umma wanaodai fedha nyingi serikalini kuliko waajiriwa wengine wowote. Mfano halisi ni kuwa Walimu wanadai kutoka kwa mwajiri wao malimbikizo ya posho ya likizo, huku wengine wakifika kusubiri fedha hizo kwa miaka mitatu, muda ambao mzunguko wao wa kupewa tena fedha hizo unakuwa umefika.
Zaidi ya fedha za likizo walimu pia wanadai fedha za stahiki mbalimbali kutoka kwa mwajiri zikiwemo stahiki za safari za kikazi, malimbilikizo ya madeni ya mishahara baada ya kurudi masomoni. Madai ya stahiki baada ya kushinda kesi mbalimbali na kadhalika.

3.6        Utekelezaji wa sera ya elimu
Hoja nyengine ya kusisitiza kuwepo kwa kodi ya elimu nchini ni utekeleza wa sera ya elimu ya mwaka 2006. Katika sera ya elimu iliyotajwa hapo juu, imeelekezwa kuwa  kutaanzishwa kwa kodi ya elimu nchini. Sura ya 9, Kifungu nambari 921 kinaeleza “Mfuko wa elimu utaanzishwa kisheria”
3.7       Nia ya serikali ya kutoa elimu bila malipo kwa wananchi wake ili kuwapa fursa sawa
Hoja nyengine ni nia ya serikali kuendelea kutoa elimu iliyo bora kwa wananchi wake

4.0              MAPENDEKEZO
Kutokana na hali ya hapo juu, Chama cha Walimu Zanzibar Kinapendekeza yafuatayo:
i)                    Serikali kufanya tathmini ya kina, juu ya mahitaji halisi ya gharama za utoaji wa elimu nchini, ili kujua kiasi halisi cha fedha kinachohitajika, badala ya hali ya sasa ambapo inaonekana kuwa serikali inatumia kulingana na kinachopatikana na sio kinahitajika.
ii)                  Kufanya tathmini ya kina juu ya michango mbalimbali iliyopo sasa kama vile michango ya madawati, kodi ya maendeleo ya ujuzi, pia michango inayokusanywa na vyuo, ili kujua ni kwa kiasi gani michango hii imekuwa ikigharamia elimu.
iii)                Kuandaa muswaada wa sheria utakaolenga kuikusanya kodi na michango yote chini ya mfuko mmoja utakaokuwa na wigo mpana zaidi na nguvu zaidi ili kukidhi mahitaji ya kifedha zinazohitajika katika elimu.
iv)                Kuanzisha kodi ya elimu kisheria ambayo itakuwa na udhibiti wa Ofisi ya Rais kodi ambayo italenga kubeba gharama za elimu nchini.
Naomba kuwasilisha    


No comments:

Post a Comment