tangazo

tangazo

Sunday, November 15, 2015

MWENYEKITI WA CHADEMA GEITA AUWAWA

Kifo chake chahusishwa na chuki za kisiasa, kampeni za Lema zatawaliwa na vilio
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, ameuawa baada ya kushambuliwa kwa mapanga na watu wasiojulikana.

Mauaji hayo yamehusishwa na chuki za kisiasa. Mawazo ambaye alikuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Busanda, kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu  2015, anadaiwa kuvamiwa jana majira ya saa 6 mchana na watu wasiofahamika na kumshambulia kwa kumkata na panga katika maeneo mbalimbali ikiwemo kichwani.

Mjumbe wa baraza la utendaji wa Chadema, Jimbo la Busanda, Himbizi Madata, alidia kuwa kabla ya umauti kumkuta, alikuwa kwenye shughuli za kisiasa kwa ajili ya hitimisho za kampeni za uchaguzi wa marudio ya udiwani wa kata ya Ludete.

Alidai kuwa kabla ya kuelekea kwenye mkutano huo walikutana kama kikao cha ndani na baada ya kumalizika kikao hicho  katika kijiji cha Katolo, Mawazo alitoka akiwa na wenzake wawili na kuchukua usafiri wa bodaboda kuelekea kata ya Ludete kwa ajili ya uchaguzi mdogo.

Alidai kuwa Mawazo alikutana na watu ambao alianza kuzozona na kutokea vurugu ambapo walimpiga kichwani na panga hali iliyosababisha kumwagika kwa damu nyingi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Geita  Dk. Adam Sijaona alisema marehemu alikutwa na majeraha makubwa kichwani yanayoonyesha amepigwa na kitu chenye ncha kali,  hali iliyochangia kupoteza maisha.
Dk. Sijaona, alisema inawezekana damu ilivilia kwenye ubongo.

Wafuasi zaidi ya 200 wa Chadema kutoka maeneo mbalimbali walifika hospitalini hapo na kukuta Mawazo ameshafariki.

Jeshi la Polisi lilipofika hospitalini hapo liliwatawaya wafuasi hao. Wafuasi hao walikuwa wakidai kuwa kifo hicho kinahusishwa na masuala ya siasa huku wakikituhuma chama cha CCM kuhusika katika mauaji hayo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita,  Mwabulambo Mponjoli, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa waliohusika hawajajulika na polisi inaendelea na uchunguzi.

VILIO, SIMANZI VYATAWALA KAMPENI ZA LEMA
Simanzi ilitawala jana baada ya Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, kutangaza  kuuawa kwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita.

Katika mkutano mkubwa wa hadhara wa uliofanyika viwanja vya Ngarenaro, kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, baadhi ya wanachama na viongozi wao walionekana wakibubujikwa machozi.

Miongoni mwa walionekana kujawa na simanzi ni mgombea ubunge Lema ambaye alisema marehemu Mawazo alikuwa akiishi naye.

Akimwita mke wake jukwaani, Lema alisema, “Mungu tufundishe cha tufanye nini.”

“Hiki walichofanya kwa Mawazo…Mungu tufundishe tufanye nini, wamemuua na wanataka kutumaliza.

“Tunataka kurudisha enzi zetu za zamani za ujasiri,” alisema na kuongeza, “mimi nimechoka na mkisikia watu wanajitoa mhanga usikimbilie kulaumu kabla ya kutafakari.”

Mbunge mteule wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia, alisema, “leo (jana)
tuna majonzi makubwa kwa sababu uhai wa Mawazo umekatizwa ghafla na hilo ni jambo la kusikitisha.

Alisema Tanzania ni ya kila mmoja, ni mali ya Watanzania wote, na sio mali ya mtu mmoja au chama kimoja.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment