tangazo

tangazo

Sunday, November 15, 2015

UBAGUZI HUU MPAKA LINI?

UBAGUZI HUU MPAKA LINI LAKINI?
Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binaadamu halikutofautisha haki za wazungu na mataifa mengine, wote kwa mujibu wa tamko hilo wana haki sawa haijalishi awe Muingereza, Mmarekani, Mkenya au Mtanzania wote kwa mujibu wa tamko la Haki za Binaadamu ni sawa, tofauti ya Mataifa haina uhusiano wowote.
Moja ya Haki kubwa ya binaadamu ni kuishi, hivyo tukio lolote la kukusudia litakalopelekea kukatisha maisha yake itakuwa amedhulumiwa haki yake ya kuishi.
Nimesukumwa kuyasema haya kutokana na namna Ulimwengu ulivyopokea tukio la mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea usiku wa Ijumaa katika maeneo sita tofauti katika jiji la Paris, nchini Ufaransa ambapo mpaka naandika makala haya idadi ya watu waliofariki ni 159 huku zaidi ya 350 wakiwa wamejeruhiwa baadhi yao vibaya sana.
Kama binaadamu wa kawaida mwenye uwezo wa kufikiria kamwe siwezi kuunga mkono mauaji haya ya 'kishenzi', ni tukio baya ambalo linapaswa kulaaniwa na kila mmoja wetu, hatuwezi kufurahia maafa yaliyowakuta wenzetu.
Lakini nimepata mshangao mkubwa kwa namna ambavyo Ulimwengu umelipa uzito mkubwa tukio hili huku wakisahau mamia ya raia wasio na chembe ya hatia wakiendelea kukatishwa maisha yao karibu kila uchao na mashambulizi ya kigaidi, turudishe kumbukumbu zetu za mauaji yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa hadi asubuhi ya leo katika mataifa haya;
Libya, Nigeria, Somalia, Kenya, Burundi, Sudan ya Kusini, Congo DRC, Syria, Afghanistan, Pakistan, Iraq, Lebanon, Palestina nk.
Mataifa yote hayo niliyoyataja na ambayo sikuyataja ni waathirika wa mashambulizi ya kigaidi mpaka leo na mamia kwa maelfu ya watu wasio na hatia wamepoteza maisha yao huku idadi kubwa wakiachwa na ulemavu wa kudumu.
Mfano nchini Kenya, turudi katika mashambulizi ya Westgate Mall, hapa zaidi ya watu 200 waiuawa wakiwemo watoto wadogo na 'makumi' kujeruhiwa, lakini halikuwa tukio lililopewa uzito kama wa Ufaransa, hapo hapo nchini Kenya, tukio la kuvamiwa na kuuawa 'kishenzi' kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Garissa, ni shambulizi la kigaidi sawa na lililotokea Paris, lakini halikupewa uzito na Ulimwengu.
Tangu usiku wa Ijumaa, vyombo vya habari vya Kimataifa, CNN, BBC, Aljaazera, DW, CCTV, France24 nk. wamevunja utaratibu wa vipindi vyao vyote kwa ajili ya 'live coverage' ya mashambulizi ya Paris, sina tatizo na hilo ila najiuliza hivi damu ya mzungu ina thamani kubwa kuliko watu wa mataifa mengine? Kwa sababu hili si tukio kubwa kuwahi kutokea kiasi cha kutuaminisha kuwa wenzetu wamekumbwa na maafa makubwa.
Kwamba binaadamu waliokufa Westgate, Garissa, na wanaoendelea kufa karibu kila siku katika mataifa ya Ukanda wa Ghaza, Syria, Afghanistan, Pakistan, Iraq, Lebanon, Libya, Nigeria nk. hawa hawana uzito wa kuileta dunia pamoja na kuungana kuwanusuru? Tunaambiwa mpaka 'profile pictures' zetu tubadilishe ili tuwaombee Wafaransa, Wafaransa? Hawa wa mataifa mengine je, thamani ya damu yao ni tofauti na wazungu?
Shambulizi la kigaidi la Westgate nchini Kenya ni kubwa kuliko lililotokea Paris, watu wanaokufa Nigeria kwa mashambulizi ya kigaidi haimithiliki, Yemen wamekufa watu wengi mno kwa mashambulizi kama ya Paris, iweje leo dunia nzima ihubiri Paris wakisahau yanayotokea kwa mataifa mengine.
Hakuna haja ya kujitoa fahamu hapa, wanaokufa wote ni watu, thamani ya damu yao haina tofauti na ya wafaransa au wamarekani, kama tunataka kuonesha Umoja wa Ulimwengu lazima tuwaangalie na hawa wenzetu wa Mataifa mengine, unafiki wa kufikiri damu ya wazungu ina thamani zaidi kuliko waarabu, 'waeshia' au waafrika ni umbumbumbu wa kiwango cha 'uzamivu'.
Siungi mkono mashambulizi ya Paris na kwa hili nalaani kwa nguvu zote, lakini dunia KAMWE haiwezi kuwa salama kama tutajifanya 'hayawani' kusema thamani ya damu ya mzungu ni kubwa kuliko raia wa mataifa mengine, eti badilisha 'profile pictures' yako kuwaombea watu wa Ufaransa! Vipi Somalia, Pakistan, Palestina, Nigeria, Kenya, Syria, Iraq au wanaokufa huku ni kunguni?
Naomba kuwasilisha!
Ally Mohammed,
Zanzibar,
Tanzania,
Email : allymohammed01@gmail.com,
Simu ya mkononi : + 255 655 572 594,
Simu ya mezani : + 255 732 940 023.


No comments:

Post a Comment