Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman, amepiga marufuku uuzwaji wa maji na matunda katika Kisiwa cha Kojani baada ya kukumbwa na ugonjwa kipindupindu.
Aidha, amewaagiza viongozi wa shehia zote za Kojani, kufanya msako wa nyumba hadi nyumba ili kuzibaini familia zinazouza biashara za maji na kuziangamiza kwa lengo la kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Alisema kila sheha pamoja na kamati zake anatakiwa kuhakikisha biashara za maji haziuzwi katika kisiwa hicho wakati huu wa mlipuko wa ugonjwa huo.
Alitoa amri hiyo wakati alipotembelea kambi ya kipindupindu katika kisiwa hicho na kuelezea kusikitishwa na baadhi ya wananchi kuendelea kuuza biashara hizo ambazo tayari zimepigwa marufuku.
Akiwa amefuatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, aliwataka masheha kuondoa muhali katika kufanikisha agizo hilo, na kuhakikisha wanawachukulia hatua za kisheria wanaokaidi kutekeleza agizo hilo.
Aidha, aliwataka wazazi kushirikiana na kuelimishana kufukia kinyesi na kuwazuia watoto wao kutumia fukwe kwa haja kubwa, kutokana na fukwe hizo kuwa karibu na makazi ya watu.
Afisa wa afya kitengo cha magonjwa ya mlipuko, Said Khatib Juma, alisema tayari timu ambayo imeundwa na wizara ya afya kwa kushirikiana na masheha imeanza msako wa nyumba ambazo zinauza biashara hizo.
Mkuu wa kambi hiyo, Khamis Mbarouk Rashid, alisema kunahitajika juhudi za ziada kuwaelimisha wakazi hao ili waweze kutambua athari za ugonjwa huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir Ali, alisema ni lazima wananchi wa Kojani watambue kwamba kusambaza maradhi ni kosa la jinai na sheria zipo.
Katika kambi hiyo idadi ya wagonjwa wa kipindupindu inaendelea kupanda hadi jana watu 24 walikuwa wamelazwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment