tangazo

tangazo

Thursday, November 26, 2015

Jaji Mkuu awafunda waandishi habari za mahakama.

Waandishi wa habari za mahakama wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kushindwa kuelewa baadhi ya maneno ya kitaalamu yanayotumiwa na majaji, mahakimu na wanasheria wakati wa kuendesha kesi na hukumu.

Akifungua mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari za mahakama jijini Dar es Salaam jana, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande, alisema mahakama kwa kutambua mchango wa waandishi wa habari imeandaa mafunzo hayo ili kuwasaidia kuelewa maana ya maneno muhimu ili kuondoa upotoshaji wakati wa kuripoti habari za mahakama.

Alisema wakati wa mafunzo hayo, waandishi wa habari wataelimishwa juu ya maneno ya kisheria yanayotumika mara kwa mara mahakamani pamoja na taratibu ili kuboresha habari na taarifa za vyombo vya habari nchini kuhusiana na mashauri mbalimbali yaliyopo mahakamani.

“Habari zilizotolewa na vyombo vya habari juu ya matukio ya mahakama na kesi unalazimu niongelee juu ya uandishi wa habari taswira au unaolenga kuhukumu kwa macho ya jamii (trial by media)," alisema.

Jaji Chande alisema habari kama hizo  zina muhukumu mshitakiwa kabla hajatiwa hatiani kihalali kwani atakuwa ameshahukumiwa mbele ya mahakama ya maoni ya jamii na kwamba kwa kufanya hivyo waandishi watakuwa wamejivika majoho ya jaji au hakimu jambo ambalo si sawa.

Alitoa mfano wa vichwa vya habari habari zinavyowatia hatiani watuhumiwa ni kama; ‘Tanesco wakamata mwizi wa umeme, mahakama ya rufani yamwachia jambazi sugu’.

“Habari zinazohukumu na jamii itamtazama hivyo mhutumiwa hata kama jamhuri au serikali imeshindwa kutoa ushahidi wa kutosha au kuthibitisha kesi bila shaka yoyote ambayo kisheria ni jukumu lao na si la  mshtakiwa.

Aidha, Jaji Chade alisema kumekuwa na habari za mahakamani ambazo huandikwa zikiishia hewani bila kufanya mwendelezo wake jambo ambalo huwafanya wananchi wasielewe kinachoendelea au hatma ya kesi husika.

"Wasomaji wamekuwa wakisubiri kuona  mwendelezo wa habari za mahakamani lakini waandishi wengi  wamekuwa wakitoa taarifa nusunusu au kutomaliza kabisa," alisema.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment