tangazo

tangazo

Wednesday, December 2, 2015

CHAMA CHA WANANCHI CUF CHAPATA MSHTUKO MKUBWA BAADA YA KUFANYIKA MABADILIKO YA GHAFLA KATIKA UONGOZI WA PBZ

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Chama Cha Wananchi (CUF) kimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kufanyika mabadiliko ya ghafla ya uongozi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ambayo yametangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita na mwanzoni mwa wiki hii.

Mabadiliko hayo ya ghafla yalianza wiki iliyopita, pale Mheshimiwa Omar Yussuf Mzee alipotangaza kufuta uteuzi wa Ndugu Ali Abdalla Suleiman, Prof. Mohamed Warsame, na Ndugu Ahmed Amani Abeid Karume, kuwa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa PBZ na kutangaza kuteua watu wengine kuchukua nafasi zao.

Hatua hiyo ikafuatiwa na taarifa ya Ikulu iliyotolewa juzi, tarehe 30 Novemba 2015, ambayo ilisema Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein amefuta uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Ndugu Juma Amour Mohamed, na nafasi yake kuteuliwa Ndugu Juma Ameir Hafidh.

CUF imepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za mabadiliko hayo kwa sababu zifuatazo:

1.      Mabadiliko hayo yamefanywa na watu ambao vipindi vyao vya uongozi vimemalizika kikatiba:-

(i)     Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Ibara ya 28(2) Rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano tokea tarehe alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais. Dk. Ali Mohamed Shein alishamaliza muda huo tarehe 2 Novemba, 2015 baada ya kutimiza miaka mitano tokea siku aliyoapishwa ambayo ni tarehe 3 Novemba, 2010.

(ii)    Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Ibara ya 42(2), Mawaziri ni lazima wawe wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Ibara ya 48(b) inaeleza kwamba nafasi ya Waziri, Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Naibu Waziri itakuwa wazi iwapo mjumbe ameacha kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa sababu nyengine zaidi ya kuvunjika kwa Baraza hilo. Katiba hiyo hiyo, Ibara ya 90(1) imetoa nafasi ya kipindi cha baina ya kuvunjika Baraza la Wawakilishi na kuitishwa Baraza jipya kuwa si zaidi ya siku tisini. Baraza la Wawakilishi lililopita lilivunjwa tarehe 13 Agosti, 2015 na hivyo siku tisini zimemalizika tarehe 12 Novemba, 2015. Kwa kutilia nguvu zaidi, Ibara ya 92(1) inasema kwamba “Maisha ya Baraza la Wawakilishi yataendelea kwa muada wa miaka mitano tangu tarehe ile ulipoitishwa Mkutano wake wa kwanza baada ya kuundwa, ila tu pale iwapo Baraza la Wawakilishi limevunjwa mapema kutokana na sababu mbali mbali zilizoelezwa katika Katiba hii.”  Ukizichukua Ibara zote hizi kwa pamoja ni kwamba kwa sasa Baraza lililopita halipo tena kwa sababu zimeshapita siku tisini tokea lilipovunjwa na pia Baraza la Wawakilishi jipya lililochaguliwa tarehe 25 Oktoba, 2015 halijaitishwa. Kwa hivyo basi, Mawaziri waliokuwepo hawana uhalali tena wa kuendelea kuwa Mawaziri kikatiba. Kwa msingi huo, Mheshimiwa Omar Yussuf Mzee, kama ilivyo kwa waliokuwa Mawaziri wote, hana sifa wala uhalali kikatiba wa kuendelea kuwa Waziri.

2.      Kwa sababu waliofanya mabadiliko hayo wameshamaliza vipindi vyao vya uongozi kikatiba, mabadiliko hayo yanaweza kuja kupingwa uhalali wake. Hali hiyo inaweza kuja kuitia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika msukosuko mkubwa kisheria na pengine hata hasara ya mabilioni ya shilingi iwapo walioteuliwa kuchukua nafasi hizo watatekeleza madaraka waliyopewa na kufanya maamuzi, na kukatokea mtu au watu ambao wataweza kuja kudai kuwa wameathirika kutokana na maamuzi waliyoyafanya.

3.      Mshtuko wetu unazidi unapoangalia kwamba taasisi yenyewe inayohusika ni benki ya kibiashara ambayo inahudumia maelfu ya wateja ndani na nje ya nchi na inafanya uhaulishaji wa fedha hadi kimataifa (international transactions). Katika hali hiyo, zikija zikitokea kesi za kimataifa basi tutakuwa tumeiweka Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) na Serikali ambayo ndiyo mmiliki wake katika hali ngumu kisheria.

4.      Mbali na hoja hizo za kikatiba na kisheria, CUF tunapata mshtuko mkubwa zaidi tunapoangalia mazingira ya mabadiliko hayo. Akiwa Mkurugenzi Mtendaji, Ndugu Juma Amour ndiye aliyefanya kazi kubwa ya kuifufua benki hiyo baada ya kuikuta katika hali mbaya sana iliyoachwa na uongozi wa Awamu ya Tano ya SMZ ambapo ilifikia hatua ya kutaka kufutiwa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

5.      Wajumbe watatu wa Bodi ya Wakurugenzi walioondolewa ndiyo wajumbe waliokuwa na utalaamu na uzoefu wa hali ya juu ambao hapana shaka yoyote ni sehemu ya mafanikio ya PBZ katika kipindi ambacho benki hiyo imeshuhudia mafanikio makubwa. Wajumbe hawa waliteuliwa Novemba 2014 na kipindi chao ni miaka mitatu ambayo ingemalizika Novemba 2017.

6.      Mshtuko mkubwa zaidi ni wakati huu ambapo mabadiliko hayo ya ghafla ya uongozi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) yamefanyika. CUF na wananchi wa Zanzibar kwa ujumla tuna mashaka makubwa na wasiwasi kwamba lengo la kuwaondoa viongozi hao wa PBZ ni kutaka kulazimisha Serikali kukopa kinyume na taratibu kwa kiasi kikubwa cha fedha kutoka benki hiyo, fedha ambazo ni za wateja, na pengine uongozi uliokuwepo ulionekana ni kikwazo cha kufanikisha malengo hayo. Tunajiuliza kwamba lengo ni kukopa fedha ili kugharimia uchaguzi wa marudio unaopigiwa chapuo na viongozi wa CCM Zanzibar?

7.      Hali hii inatia wasiwasi baada ya kuona taasisi nyengine iliyokuwa imepata mafanikio makubwa yaani Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) ambao unatunza fedha za wafanyakazi wa Serikali na wale wa sekta binafsi kufikishwa katika hali mbaya kifedha baada ya SMZ kuchukua fedha zake na kugharimia miradi ambayo haina tija kiuchumi kama ule wa Viwanja vya Kufurahishia Watoto Unguja na Pemba na miradi mingine kama hiyo. Je, baada ya ZSSF sasa watu wanaelekea PBZ?

Kutokana na sababu hizo, CUF haikubaliani na mabadiliko hayo ambayo dalili na ishara zote hazioneshi kwamba yana malengo mema kwa wananchi wa Zanzibar ambao kupitia Serikali yao ndiyo wamiliki wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ).

CUF tulitegemea kwamba Zanzibar tungejifunza kutokana na hatua anazochukua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli, za kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali, matumizi mabaya ya fedha za umma na matumizi mabaya ya madaraka. Hata hivyo, kwa hatua hizi zinazoendelea kufanywa na viongozi ambao wamemaliza vipindi vyao vya kuwepo madarakani hapa Zanzibar, haionekani kwamba tuna malengo yanayofanana katika kuwahudumia wananchi.

Tunaamini kwamba mwanya huu unaotumiwa na viongozi hawa utaondoka pale Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) itakapokamilisha kazi ya kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Urais wa Zanzibar, kumtangaza mshindi na kutoa nafasi kwa vyama vya CUF na CCM kuunda Serikali mpya ya Umoja wa Kitaifa kuundwa ili kuipa Zanzibar uongozi mpya wenye dira ya kututoa katika mkwamo huu uliopo ambao unapelekea kuendelea kufanya maamuzi yasiyo na misingi ya Katiba na Sheria za nchi.


HAKI SAWA KWA WOTE


ISMAIL JUSSA

MKURUGENZI WA MAWASILIANO – CUF

No comments:

Post a Comment