Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baghresa Group Bwana
Said Salim Baghresa akimueleza Balozi Seif juhudi zinazofanywa na Kampuni yake
za kujenga Kisiwa cha Mji Mpya Mtoni Marine.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi
Zanzibar { ZIPA } Nd. Salum Khamis Nassor akimueleza Balozi Seif
hatua zinazochukuliwa na Taasisi yake katika kuona taratibu za uwekezaji
zinachukuliwa kwa wanaowekeza vitege uchumi vyao Nchini.
Balozi Seif akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Baghresa Group Bwana Said Salim wakitembelea kuona mradi
wa Ujenzi wa Majengo Mapya ya Hoteli ya Mtoni Marine ambayo iko chini ya
Kampuni hiyo kwa hivi sasa.
Mradi mkubwa wa Kimataifa wa ujenzi wa kisiwa cha Kitalii
ambacho kitatengezezwa kwa mfumo wa ufukiaji Bahari umeanza rasmi katika
eneo la Hoteli ya Utalii iliyopo Mtoni Marine kaskazini Magharibi ya Mji wa
Zanzibar.
Hata hivyo gharama kamili za Mradi huo bado
hazijafahamika wakati utakapokamilika rasmi ujenzi wake hapo
baadaye.
Mradi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Kizalendo ya
Baghresa Group utahusisha ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa ya Ghorofa Tano
ya Daraja la Tano { Five Star + },
utengenezaji wa eneo la wazi la mapumziko { Public Beach } pamoja na
kutengeneza Kisiwa cha Mji mpya .
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alishuhudia harakati za ujazaji wa mchanga katika eneo linalofukiwa ambazo
hufanywa kwa utaalamu wa hali ya juu.
Mhandisi wa Mradi huo Bwana Ahmed Shamsi alimueleza Balozi
Seif kwamba chombo maalum kinachotumika kwa kazi ya uchimbaji wa mchanga
Baharini kina uwezo wa kunyonya na kusafirisha mchanga kutoka ndani
ya Bahari sambamba na kukata Majabali.
Mhandisi Shamsi alisema kazi hiyo inafanyika kwa saa 12 kila
siku ambapo takwimu zinaonyesha wazi kwamba uchimbaji huo wa mchanga
unaokwenda zaidi ya mita 15 chini ya Bahari unafikia Tani 600 za
mchanga kwa saa Moja.
Alifahamisha kwamba harakati za uchimbaji na kufukia mchanga
katika eneo hilo zilizoanza Mwezi uliopita wa Novemba zinatarajiwa kukamilika
mwezi Januari mwaka ujao.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baghresa
Group Bwana Said Salim Baghresa alisema kwamba ujenzi wa mradi huo muhimu
kwa uchumi wa Nchi utasaidia mapato ya Taifa pamoja na kutoa ajira kubwa kwa
vijana Wazalendo hapa Nchini.
Bwana Baghresa alisema mfumo wa ufukiaji Bahari kwa ajili ya
kuanzisha miradi ya Kiuchumi ni mfumo unaotumiwa na Mataifa mbali mbali Duniani
ambapo kwa Afrika mradi kama tayari umeanza kutumiwa katika Kisiwa cha
Seycheles.
Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi ameupongeza Uongozi wa Baghresa Group kwa uamuzi uliochukuwa wa
kuanzisha mradi huo mkubwa wa Kimataifa.
Balozi Seif alieleza kwamba kukamilika kwa mradi huo
mkubwa ambao umeshazoeleka katika Mataifa yaliyoendelea utasaidia
kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla Kiutalii Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi
huo wa Baghresa Group kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila
msaada unaohitajika katika kuona mradi huo unafikia malengo uliojipangia.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamui wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment