Picha na Makeme Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein akimtunuku Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Kemia Khamis Mohammed Saidi kwenye mahafali ya kumi na moja yaliyofanyika Kampasi ya Tunguu Mkoa Kusini Unguja.
Mwanafunzi aliefanya vizuri zaidi katika Mahafali ya kumi na moja ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar Rauhiya Ahmed Hamdun akipokea zawadi maalum kutoka kwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein akiutangazia mkusanyiko uliokuwepo kiwanja cha Kampasi ya Tunguu kuwa ni Mahafali ya kumi na moja ya Chuo hicho, (kulia) Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Said Bakari Jecha na kushoto Makamu Mkuu wa chuo Prof. Idriss Ahmad Rai.
Maandamano ya wahitimu wa Mahafali ya kumi na moja ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) yakiingia katika kiwanja cha Mahafali hayo yaliyofanyika Kampasi ya Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja. Picha na Makeme Mshenga-Maelezo Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amekitaka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kuendelea
kufanya tafiti kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo na kuhakikisha kuwa matokeo ya
tafiti hizo yanasambazwa kwa taasisi na sekta zinazohusika na yanatumika
ipasavyo katika mipango ya maendeleo.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA),
kiliopo Tunguu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja katika Mahafali ya Kumi
na Moja ya Chuo hicho baada ya kuwatunuku vyeti wahitimu 699 katika fani 15
wakiwemo 7 wa Shahada ya Uzamili ya Sayasi katika Kemia.
Katika maelezo yake
Dk. Shein alisema kuwa ameridhishwa sana na dhamira na juhudi zinazoendelea
kuchukuliwa na SUZA hivi sasa za kuimarisha shughuli za utafiti na ubunifu
kwani amekuwa akihimiza ufanyaji wa utafiti kila mahali na ndio maana
akaanzisha Idara za utafiti kwa kila Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Dk. Shein alisema kuwa
kwa kufanya hivyo itakuwa ni rahisi kutimiza dhamira ya chuo hicho ya kukifanya
kuwa kinaongoza katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa utoaji wa taaluma bora,
ufanyaji wa tafiti na kukuza ubunifu katika fani mbali mbali.
“Matunda ya jitihada
zenu tayari yanaonekana tukijua kwamba wakati vyuo vyengine vinakosa waombaji
wa kujiunga na masomo, SUZA imepata zaidi idadi inayohitajika tena wakiwa na
sifa nzuri zaidi ya viwango vilivyowekwa”,a lsiema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alikitaka
chuo hicho kuendeleza utamaduni wa kuzishirikisha taasisi za Serikali katika
mafunzo mbali mbali yanayotolewa Chuoni kupitia miradi iliyopo kila
inapotokezea fursa za aina hiyo kwani utamaduni huo utasaidia sana juhudi za
Serikali za kuwajengea uwezo watumishi wa Umma.
Dk. Shein pia,
alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa SUZA pamoja na wahitimu kwa ongezeko
la wahitimu wa fani nyengine tatu mpya ambazo ni Stashahada ya Usimamizi wa
Urithi wa Kale na Utalii, Stashahada ya Ukutubi na Shahada za Uzamili ya Kemia.
Alisema kuwa kupata
wahitimu katika kiwango cha Shahada ya Uzamili, katika masomo ya Sayansi kwa
mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar ni tukio
kubwa na la kutia moyo.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alisema kuwa sekta ya utalii hivi sasa ndiyo sekta kiongozi kwa uchumi wa
Zanzibar hivyo matumaini yake ni kuwa wahitimu wa fani ya Usimamizi wa Urithi
wa Kale na Utalii watakuwa ni chachu ya mabadiliko na watasaidia kukabiliana na
vyema na changamoto za usimamizi wa maeneo ya urithi wa kale.
Aidha, wahitimu wa
diploma ya ukutubi watasidia kwa kiasi kikubwa kufikia azma ya Serikali ya
kuanzisha maktaba katika skuli zote za Sekondari na msingi na kutoa wito kwa
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kufanya jitihada za kuwaajiri na kuwaenzi
vijana hao pale hali itakaporuhusu ili waweze kutoa mchango wao katika fani
hiyo.
Dk. Shein alisema kuwa
amevutiwa na taarifa za maandalizi ya kuanzisha masomo ya fani mbali mbali
katyika ngazi ya Uzamili kama vile Usimamizi wa Mali Asili na Tabianchi pamoja
na ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni.
Alisema kuwa ni wazi
kwamba licha ya mafanikio hayo yaliopatikana hadi sasa, uongozi wa chuo
unahitaji kuendelea kuongeza kasi kwa kufanya kazi kwa umakini na ubunifu wa
hali ya juu, kwani Serikali na wananchi wanategemea maendeleo makubwa zaidi
katika Chuo hicho.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alsiema kuwa Wizara Ya Elimu pamoja na Uongozi wa Chuo wamefikia hatua
nzuri ya kulifanyia kazi agizo la Serikali la kuziunganisha na SUZA taasisi
tatu za elimu ya juu ikiwemo Chuo cha Taalamu za Sayansi za Afya kiliopo
Mbweni, Chuo cha Uongozi wa Fedha na Chuo vcha Utalii Maruhubi.
Katika hotuba yake
hiyo pia, Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake na juhudi za SUZA za kuimarisha
fursa za elimu kwa wanawake kwani katika mahafali hiyo sehemu kubwa ya wahitimu
ni wanawake ambao ni sawa na asilimia 64.2 ambapo pia mwanafunzi wa kike kwa
mara nyengine tena ndie aliyefanya vizuri katika masomo ya sayansi.
Dk. Shein pia,
aliueleza uongozi wa SUZA kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zao ili
malengo ya kuanzishwa kwa Kampasi ya Benjamin William Mkapa iliyopo Mchanga
Mdogo Pemba, yaweze kufikiwa huku
akiwataka wananchi wa Pemba waitumie fursa hiyo huku Serikali ikiwa na nia ya
kuanzisha Chuo Kikuu kisiwani humo.
Katika nasaha zake kwa
wahitimu hao, Dk. Shein aliwataka kila mmoja kuhakikisha anajiwekea malengo
ambayo yatakuwa na tija kwake mwenyewe, familia, jamii na nchi kwa jumla
sambamba na kupanga mikakati ya kuyafikia malengo hayo.
Pia, aliwataka
wahitimu kuendelea kuwa waadilifu na wazalendo kwa nchi yao na kuwahimiza hasa
kwa wale wote walioomba mikopo Serikalini na wakakopeshwa, kufanya juhudi za
kurejesha mikopo hiyo kwa mujibu wa sheria na makubaliano yaliopo ili fedha
hizo ziweze kuwasaidia wanafunzi wengine wanaotaka kujiendeleza.
Pia, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Fedha, Wizara ya Elimu pamoja na Tume ya
Mipango kukaa pamoja na kuhakikisha katika mahafali kama hiyo hapo mwakani inafanyika katika ukumbi maalum badala ya
maeneo yanayofanyika hivi sasa.
Nae Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali, Mhe. Ali Juma Shahuna alieleza juhudi zinazofanywa na
Serikali kupitia Wizara yake katika kutoa mashirikiano na chuo hicho na
kumpongeza Dk. Shein kwa uongozi wake na juhdui zake za kukisimamjia na
kukionoza chuo hicho akiwa Mkuu wa Chuo hicho.
Nae Makamu Mkuu wa
Chuo hicho Profesa Idrisa Ahmada Rai, alimueleza Dk. Shein mikakati iliyowekwa
na chuo hicho sambamba na mafanikio yaliopatikana ikiwa ni pamoja na kuanzisha televisheni ya
chuo hico (SUZA TV) itakayotumika kutoa taaluma ya masomo ya sayansi kwa skuli
za Sekondari za Zanzibar sambamba na kuitumia TEHAMA kwa kufundishia.
Pamoja na hayo,
alieleza azma ya ujenzi wa daghalia kwa mashirikiano ya ZSSFna PBZ pamoja na
majengo mengine ya chuo hicho. Aidha, alieleza mafanikio ya wanawake chuoni
hapo na kupongeza kwa jinsi wanavyofanya vizuri katika masomo yao.
No comments:
Post a Comment